Bajaj zikichukua nafasi ya daladala zilizogoma katika utoaji wa huduma za usafirishaji Jijini Mbeya |
Daladala pekee zinazoendelea kutoa huduma ni zile zinazoelekea Mwanjelwa, Mbalizi hadi TAZARA |
Bajaj zikisubiri abiria baada ya daladala kugoma Jijini Mbeya |
Magari aina ya Canter na Bajaj yameonekana yakitoa huduma za usafirishaji |
Pilika pilika zikiendelea katika kituo cha Daladala cha Kabwe huku magari binafsi yakiendelea kutoa huduma kwa wananchi |
SIKU tatu
baada ya kuendelea kwa mgomo wa wasafirishaji wa abiria Daladala Jijini Mbeya,
Sumatra kanda ya Mbeya imetoa onyo kwa wasafirishaji hao kwamba iwapo
watandelea na mgomo wao zaidi ya siku ya kesho watafutiwa leseni zao.
Akizungumza
kwa njia ya simu kutokea Jijini Dar es salaam, Meneja Sumatra kanda ya Mbeya
Petro Chacha iwapo wasafirishaji hao wataendeleana mgomo wa kutoa huduma za
usafirishaji katika Jiji la Mbeya hadi kesho, watalazimika kuwafutia leseni zao
za usafirishaji wa abiria Jijini humo.
‘’Wameanza
mgomo kwa madai ambayo si ya msingi, wao wanataka kuondolewa kwa route ya
mzunguko kupitia Moon Dust na kutokea Soweto, kuingilia OilCom na kutokea
Kabwe, hili limetusaidia kupunguza msongamano wa magari kati ya Mafiat hadi
Soweto nyakati za jioni,’’alisema.
Alifafanua
kuwa utaratibu huo ulipangwa baada ya vikao vya kamati ya ulinzi na usalama
mkoa wa Mbeya baada ya kuona kuna kukwama kwa shughuli za kiuchumi katika Jiji
la Mbeya kutokana na msongamano ambao umetokana na muingiliano wa magari
yanayoenda safari ndefu na haya yanayosafiri ndani ya Jiji la Mbeya.
Chacha
alisema kuwa kutokana na hali hiyo Sumatra iliweka utaratibu kuepusha
msongamano na kuwa katika njia ambazo daladala zimekuwa zikipita kumekuwa na
ongezeko la abiria ambao wanashuka na kupanda bila bugudha na hivyo kuongeza
kipato kwa wasafirishaji hao na kuwa mgomo wao hauna sababu za msingi.
‘’Tumefanya
utafiti wa kina tumebaini njia tulizoziongeza zimekuwa karibu na wananchi na
Machinga, ambao awali walikuwa wakiweka bidhaa zao barabarani, kupeleka
daladala upande huo tumewasaidia kuwafikia abiria wengi wanaofuata bidhaa kwa
machinga waliohamishiwa upande huo,’’alisema Chacha.
Alibainisha
kuwa baada ya kuibuka kwa mgomo huo baadhi ya magari binafsi na Bajaj
zimeruhusiwa kubeba abiria ili kupunguza kadhia ya wananchi kukosa huduma hizo
kwa kipindi ambacho Daladala zimeamua kugoma kusafirisha abiria.
‘’Tutatoa
siku moja tu ya kesho kutwa iwapo wasafirishaji hao wataendeleza mgomo,
tunawafutia leseni zao za usafirishaji wa abiria Jijini Mbeya,’’alisisitiza.
Mgomo huo wa
Daladala umedaiwa kuitishwa na baadhi ya daladala zinazofanya shughuli zake kupitia
njia za Stendi Kuu na Uyole, Isyesye na
Ituha hali ambayo ilisababisha kuwepo kwa msongamano wa abiria wanaohitaji
kuwahi shughuli zao za kila siku.
Hata hivyo
kuibuka kwa wasafirishaji mbadala wa Bajaj na magari binafsi ambayo ndiyo
yanayotoa huduma za usafirishaji hadi sasa kumeondoa adha hiyo na kurejesha
hali ya shughuli za wananchi kama kawaida.
Inaelezwa
kuwa wasafirishaji waliogoma walihitaji kuongeza nauli kutoka Sh.400 ya kawaida
hadi sh.500 kwa madai ya kufidia mzunguko ulioongezwa na Sumatra, na kwamba
madai hayo ya ongezeko la nauli yanaweza kufidia gharama.
Aidha wakati
magari yanayosafirisha abiria kwa njia za Uyole. Sokomatola na Stendni Kuu
yameingia katika mgomo, yale yanayofanya safari kati ya Mbalizi, Sokomatola,
Stendi Kuu na Mwanjelwa yanaendelea na utoaji wa huduma za usafirishaji kama
kawaida.
Baadhi ya
wananchi waliozungumza na mtandao huu wamedai kuwa ni vyema uamuzi mgumu
ukachukuliwa dhidi ya watoaji huduma hao waliogoma ikiwa ni pamoja na kufutiwa
leseni zao za usafirishaji na kwamba Jiji la Mbeya linazidi kupanuka hivyo huduma
zinahitajika katika maeneo ya pembeni badala ya kuendelea kung’ang’ania njia
walizozoea awali.
Naye Mkazi
wa Kabwe Jijini Mbeya alisema kuwa ni vyema wasafirishaji wakawa waelewa kwa
kuwa Halmashauri ya Jiji inaendelea kupanuka hivyo ni muhimu wakajua kuwa
kitendo hicho cha kuongeza safari za daladala ni kuendelea kutoa huduma kwa
wananchi.
Huduma za
usafirishaji katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Mbeya zinaendelea huku Bajaj,
magari aina ya Noah, Canter, Landcruiser na Teksi zimekuwa ziwahudumia wananchi
kwa nauli ya Sh. 500 kwa kila mtu kati ya Stendi kuu na Sae huku yale
yanayoelekea Uyole yakitoza nauli ya Sh.600.
Post a Comment
Post a Comment