Wachezaji wa Mbeya City na kocha wao wakitaka kuwavamia waamuzi huku askari wa kutuliza ghasia wakiwazuia kufanya vurugu |
Wachezaji wa Mbeya City wakiwatupia maneno makali waamuzi wa mchezo kati yao na Prison katika uwanja wa Sokoine leo jioni, mechi hiyo ya kirafiki iliisha kwa sare ya 1-1 |
Askari wa kutuliza ghasia wakiwaongoza waamuzi wa mchezo huo |
Wachezaji wa Mbeya City wakiwazonga waamuzi baada ya kutoa penati kwa timu ya Prison,baada ya mchezaji wa Mbeya City Deogratius Julius kuunawa mpira eneo la hatari |
Waamuzi wa mechi kati ya Prison na Mbeya City Keffa Kayombo aliyechezesha katikati (kulia) John Kanyenye (katikati) Mirambo Shikungu |
Wachezaji wa MBEYA City wakipongezana baada ya kufunga goli lililokataliwa na mshika kibendera baada ya kuotea |
Utovu wa
nidhamu, vurugu na rabsha za hapa na pale zilizosababisha Polisi wa kutuliza
ghasia kuingia katikati ya Uwanja ni miongoni mwa matukio yaliyobeba hisia za
wapenzi wa soka Jijini Mbeya ambao walitarajia kuona burudani ya kandanda kati
ya timu zenye mashabiki wengi Mbeya City na Prison za Jijini hapa.
Mchezo huo
umezikutanisha timu hizo ikiwa ni takribani miezi mitatu tangu kumalizika kwa ligi hiyo mwezi
Aprili mwaka huu huku Prison ikikumbuka majeraha ya kufungwa na Mbeya City bao
1-0 katika mzunguko wa pili wa ligi hiyo.
Wakicheza
kwa kujiamini na kutarajia kushinda mechi hiyo timu ya Mbeya City walianza kuonesha utovu wa nidhamu pale
mchezaji wa timu hiyo Richard Peter alipofanikiwa kutingisha nyavu za Prison
katika dakika ya 25 ilhali mshika kibendera wa kulia mirambo Shikungu akiwa
amenyoosha kibendera kuashiria kuwa mchezaji huyo alikuwa ameotea.
Hali hiyo
ilianzisha lawama dhidi ya mshika kibendera huyo na kusababisha Mbeya kutoelewana vyema ilhali wenzao wa Prison wakijitahidi kutumia
fursa hiyo kuonesha kiwango kizuri cha kandanda.
Kwa
takribani dakika 14 mchezo huo ulikuwa ni wa kuviziana kati ya Mbeya City na
Prison ambapo kunako dakika ya 44 ya mchezo Winga wa kulia wa MBEYA City Deus
Kaseke aliambaa ambaa na mpira kuelekea katika lango la Prison.
Kaseke
alitoa pasi iliyomkuta Paul Nonga ambaye alipiga shuti lililombabatiza kipa wa
Prison Mohamed Yusuf ambaye bila tahadhari aliondosha hatari kwa miguu na
kumbabatiza mlinzi wa timu yake Lugano Mwangama na kujifunga goli, dakika ya 44.
Hadi mapumziko Mbeya City walitoka kifua mbele wakiongoza goli 1.
Kipindi cha pili kilianza kwa kila timu kufanya mabadiliko ambapo Prison walizalimika kucheza nusu baada ya mchezaji wao Jeremiah Juma kuzawadiwa kadi mbili za njano kwa mchezo mbaya na kulazimika kutoka nje ya uwanja.
Awali Prison walipata penati iliyolalamikiwa na wachezaji wa Mbeya City ambapo mchezaji wao Deogratius Julius aliunawa mpira eneo la adhabu na kusababisha wachezaji wa timu hiyo kumzonga mshika kibendera lakini hata hivyo penati hiyo iliyopigwa na Ibrahimu Mamba ilipaa juu ya mwamba.
Zikiwa zimesalia dakika chache kabla ya mechi hiyo kumalizika huku wachezaji wa Mbeya City wakiamini kuwa wameshinda mechi hiyo, wachezaji wa Prison walilisakama lango la Mbeya City kama nyuki na kusababisha goli lililofungwa kwa kichwa na Frank William.
Kipenga cha kumaliza mpira huo kilichopulizwa na mwamuzi wa kati Kayombo kilisababisha kundi la wachezaji wa timu hiyo kuvamia uwanja na kumzonga mshika kibendera Shikungu ambapo waamuzi wengine waliingilia kati kuzuia tafrani hiyo.
Hali hiyo ilisababisha askari polisi kuingilia kati na kulazimika kuwatoa nje ya uwanja waamuzi wakiwa chini ya ulinzi mkali.
Post a Comment
Post a Comment