Ads (728x90)



Baadhi ya waumini wa Kiislamu wakitoka katika Ibada ya swala ya Ijumaa katika msikiti wa Baraa Bin Azb Isanga Mbeya.
Baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu wakiwa katika Ibada ya swala ya Ijumaa leo mchana.

MATAJIRI wa Kiislamu wametakiwa kutojifaharisha kwa utajiri wao bali wametakiwa kuutumia utajiri waliopewa na Mwenyezi Mungu ili kuwasaidia wasio na uwezo.
Akizungumza katika ibada ya swala ya Ijumaa katika msikiti wa Baraa Bin Azb uliopo Isanga Jijini Mbeya Imamu wa Msikiti huo Shekhe Ibrahim Omar Bombo alisema kuwa utajiri na umaskini umekuwepo ili kuweka uwiano wa maisha.
‘’Kama wasingekuwepo matajiri na maskini dunia isingeweza kwenda, matajiri wamekuwepo ili wawasaidie wasio na uwezo, nao matajiri hawawezi kujivunia utajiri wao kama hakuna wa kuwasaidia,’’alisema Shekhe Bombo.
Alibainisha kuwa ili kuona matajiri na wasio matajiri wanategemeana ni pale tajiri anayemiliki magari ya usafirishaji ambaye anatumia fursa hiyo kuwaajiri wasio na uwezo ili nao wapate kipato kutokana na utajiri wa mmoja.
‘’Hizi ni kudra za Mwenyezi Mungu kumpa amtakaye na kumnyima amtakaye, asiye nacho hapaswi kusikitika sana na aliyenacho hapaswi kujifaharisha kwamba ni mjanja kuliko asiyenacho,’’alisema.
Akinukuu baadhi ya aya za Koran na Hadith za Mtume Muhammad (SAW) Shekhe Bombo alisema kuwa mwezi Mtukufu wa Ramadhani umekuja ili kuwapima watu uchamungu na kujiweka karibu na Mwenyezi Mungu.
Alisema kuwa kipindi hiki cha Mwezi wa toba ndicho ambacho waumini wa dini ya Kiislamu wanatakiwa kuoneana huruma na kukirimiana na kuwa uchamungu unamweka mja karibu na Mola wake.
Naye Mwenyekiti wa Taasisi ya Kiislamu ya Dhiynurayn Shekhe Dormohamed Issa alisema kuwa, Mwezi wa Ramadhani umewafanya waislamu kuwa pamoja kwa kipindi kirefu katika ibada hivyo ni fursa pekee kwa waumini hao kutubu madhambi yao kwa kukithirisha kufanya ibada usiku na mchana.
‘’Hii ni fursa pekee kwa waumini kutubu madhambi, wapo waliotangulia mbele ya haki kabla ya Mwezi huu, hakuna aliyetoa hongo kwa Mwenyezi Mungu ili abaki, turejee kwa mola wetu atusamehe madhambi yetu,’’alisema Shekhe Issa.

Post a Comment

Post a Comment