Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya Godfrey Zambi akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa kikao cha Halmashauri Kuu ya chama hicho |
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya Godfrey Zambi akijadili jambo na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Mbozi Aloyce Mdalavuma baada ya kumalizika kikao cha Halmashauri Kuu ya chama hicho wilayani humo. |
Madiwani wakijadiliana mustakabali wao baada ya kutakiwa kutoka nje ya ukumbi kupisha kujadiliwa. |
Baadhi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu CCM Wilaya ya Mbozi wakitoka kwenye ukumbi wa Mkutano. |
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mbeya Godfrey Zambi akizungumza na Mwandishi wa habari wa gazeti la Jambo Leo kuhusu kikao kilichojadili kuwataka madiwani wa chama hicho wajiuzuru |
MSUGUANO
mkali umeibuka katika kikao cha Halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya
ya Mbozi Mkoani Mbeya ulioshinikiza kujiuzuru kwa Madiwani wote wa Chama hicho kutokana na
Halmashauri ya wilaya hiyo kupata hati ya mashaka kwa miaka mitatu mfululizo.
Hatua ya kikao
hicho cha chama ilifuatia kuibuka kwa malalamiko yaliyotolewa katika kikao
kilichopitia hoja za Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali ambapo Mkuu
wa wilaya ya Mbozi Dkt. Michael Kadeghe alihusishwa na ubadhirifu wa fedha za
Halmashauri hiyo.
Kikao hicho
kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa chama hicho wilayani humo
uliowahusiha viongozi wa chama wilayani humo na Mwenyekiti CCM mkoa wa Mbeya ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mbozi Godfery Zambi na Mwenyekiti wa chama wilayani humo Aloyce Mdalavuma.
Madiwani wa
chama hicho pamoja na watendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo akiwepo
Mkurugenzi na wakuu wa idara walionekana kuwekwa kiti moto na chama hicho kwa
kile kilichoelezwa kuwa wameshindwa kutekeleza ilani ya chama tawala na
kusababisha kupatikana kwa hati za mashaka kwa miaka mitatu mfululizo.
Kikao hicho
ambacho kilivuta hisia za wakazi wengi wa wilayani humo na mkoa kwa ujumka ambapo ambacho waandishi wa
habari hawakuruhusiwa kuingia,kilidaiwa kumlenga Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo
Elick Ambakisye ajiuzuru nafasi yake kwa shinikizo la viongozi wa chama wilaya
kwa kile kilichoelezwa kuwa alishindwa kuisimamia Halmashauri hiyo ipasavyo.
Hata hivyo
taarifa zaidi zilidai kuwa kumekuwepo na mvutano wa muda mrefu juu ya viongozi
wa chama hicho, kutokana na kile kilichoelezwa kuwa harakati za kuwania nafasi
ya Ubunge kwa mwaka kesho kumeongeza chafu ya kupangua safu ya uongozi wa chama
hicho wilayani humo.
Mvutano
ndani ya kikao hicho uliibuliwa na wajumbe wa kikao hicho ambao kila mmoja
alitoa maoni yake ambapo baada ya kuelekezwa shutuma kwa Mkuu wa wilaya ya
Mbozi Dkt. Kadeghe aliyedaiwa kuhujumu fedha za halmashauri hiyo, kibao
kiliwageukia Madiwani ambao walielezwa kushindwa kuisimamia vyema Halmashauri
hiyo.
‘’Tatizo
lipo kwa Madiwani wetu, wameshindwa kuisimamia vyema Halmashauri, ni vyema
wangejiuzuru wote ili tujipange upya, hakuna haja ya kuwepo kwa Baraza la
Madiwani ambalo halina maslahi na Wilaya na Chama chetu’’alisema mmoja wa
wajumbe ambao sauti yake ilisikika hadi nje ya ukumbi.
Mjumbe
mwingine wa kikao hicho alielekeza tuhuma zake kwa Mwenyekiti wa Halmashauri
Ambakisye akidai kuwa anapaswa kujiuzuru kwa kuwa yeye ndiye msimamizi mkuu wa
Halmashauri hiyo na kuwa iwapo kungekuwa na usimamizi makini hati za mashaka
zisingeweza kutokea.
‘’Kama ni
kujiuzuru, meza hiyo hapo mbele wote mnatakiwa kujiuzuru tukianzia na Katibu
wa CCM wilaya ndipo wafuate Mwenyekiti na Madiwani, hili jambo ni fedheha kubwa
kwa Halmashauri yetu,’’alisema Edward Mwamudi aliyejitambulisha kuwa mjumbe wa
Halmashauri kuu.
Hatimaye maoni
mbalimbali ya wajumbe ya Mkutano huo yalisababisha watendaji wa Halmashauri
hiyo waruhusiwe kutoka nje ya ukumbi na baadaye Madiwani wote walitakiwa kutoka
nje ili wajumbe wajadili aina ya adhabu itakayofaa kwa Madiwani hao.
Baada ya
kikao cha takribani saa moja wazee wawili walitoka nje na kumuita pembeni Mwenyekiti
wa Halmashauri Ambakisye na kumtaka atumie busara ya kujiuzuru nafasi yake
ambaye alikataa na kudai kikao kinapaswa kufuata kanuni ili kuridhia kuondolewa
kwake madarakani na si vinginevyo.
Mwandishi: Nasikia umeitwa ili utamke kujiuzuru
nafasi yako ya Mwenyekiti wa Halmashauri.
Ambakisye: Wameniita na kunishauri nitamke ili
nijiuzuru, nimegoma, wanapaswa kufuata taratibu siwezi kujiuzuru kienyeji,
sioni sababu ya kujiuzuru, kwa kosa lipi, kwanini nijiuzuru kuna nini nyuma
yake?
Aidha
Ambakisye alisema kuwa tuhuma hizo zimeelekezwa kwake binafsi na si vinginevyo
na kuwa hii inatokana maslahi ya kisiasa ya baadhi ya viongozi wa chama hicho.
Mwenyekiti wa
CCM wilaya ya Mbozi Mdalavuma alisema kuwa kikao hicho kiliketi kujadili
mustakabali wa chama kuelekea uchaguzi wa serikali za Mitaa mwezi Octoba na
uchaguzi mkuu 2015 na kuwa dosari za kuwepo kwa hati za mashaka zingeweza
kukipunguzia uaminifu kwa wananchi.
Alisema
baada ya kutafakari kwa kina waliamua kuwaita madiwani pamoja na watendaji ili
kuwekana sawa ambapo yaliibuka mengi yanayoonesha udhaifu wa usimamizi wa
madiwani hao hivyo wajumbe walitoa mapendekezo mbalimbali juu ya hatima ya
madiwani hao.
Alifafanua
kuwa wapo waliotaka Madiwani hao wajiuzuru na waapo waliosema kuwa Mwenyekiti
wa Halmashauri pamoja na madiwani wote wanapaswa kujiuzuru lakini wilaya
ilishindwa kuchukua maamuzi hayo kwa kuwa haina mamlaka ya kufanya hivyo.
Mwandishi: Hebu nieleze Mheshimiwa Mwenyekiti wa
Wilaya, kikao chenu kilimalizika kwa
msimamo upi juu ya hatima ya mwenyekiti na Madiwani wa chama chenu.
Mdalavuma:Kulikuwa na mjadala mrefu juu ya
suala la kujiuzuru kwa Mwenyekiti na Madiwani, lakini tulibanwa na kanuni,
kikao hakina mamlaka ya kuwasimamisha bali kina uwezo wa kutoa mapendekezo
kwenye kikao cha juu cha Halmashauri ya Mkoa na baadaye mkoa utapeleka kwenye
kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ili ijadili.
Mwandishi:Kulikuwa na taarifa za kutaka
kujiuzuru kwa Mwenyekiti wa Halmashauri na baadhi ya wazee walitoka nje na
kumuomba Mwenyekiti ajiuzuru, utaratibu huu ukoje?
Mdalavuma: Kama nilivyokueleza awali taratibu
na kanuni zetu zinatubana, Mwenyekiti hawezi kulazimishwa kujiuzuru labda aamue
mwenyewe kufanya hivyo, mwanzo alikiri kuwa Madiwani walishindwa kuisimamia
Halmashauri, lakini kitendo cha yeye kuamua kujiuzuru kingethibitisha kuwa ana
makosa, hivyo taratibu zinapaswa kufuatwa ili kuweka uhalali wa kujiuzuru kwao.
Kwa upande
wake Mwenyekiti wa CCM mkoa Godfrey Zambi alisema kuwa mkutano huo ulitokana na
yaliyojiri kwenye kikao cha Baraza la Madiwani kilichopita ambacho kilikuwa kikipitia
hoja za Mkaguzi na Mdhibiti wa Fedha za Serikali (CAG) ambapo Halmashauri hiyo
ilipata hati ya mashaka miaka mitatu mfululizo.
Zambi ambaye
pia ni Mbunge wa jimbo la Mbozi Mashariki na Naibu Waziri wa Kilimo Chakula na
Ushirika alisema kuwa kumekuwa na maneno yanayozungumzwa yanayoelezea hisia za
viongozi wa chama kuwa na maslahi yao na kuwa uzushi huo si wa kweli bali
kilichoendelea ni utendaji na uwajibikaji wa kawaida ndani yaa chama.
‘’Kikao cha
leo tumechukua mapendekezo tutayapeleka kwenye kikao cha Maadili, hakuna
maslahi ya yeyote kati ya viongozi wa kisiasa, mimi binafsi sijamshambulia kwa
maneno Mwenyekiti wa Halmashauri nilishawahi kumsimamia asiondoke wakati wa
mgawanyiko wa wilaya za Mbozi na Momba,’’alisema Zambi.
Alisema wapo
walioonesha nia yao ya kugombea Ubunge kama vile Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya
Taifa CCM wilaya hiyo George Mwenisongole,na kuwa yeye hajawahi kulalamika
popote ijapo kuwa anachokifanya kiko kinyume na taratibu za chama.
Mwandishi:Mheshimiwa Mwenyekiti wa Mkoa, Zipo
taarifa kuwa wewe umekuwa chanzo cha migogoro ndani ya Chama, tangu uingie
madarakani chama kimekuwa katika migogoro na hivi karibuni kuna baadhi ya
viongozi wa Ileje na Tunduma mmewasimamisha, hili unalisemaje?
Zambi: Kwanza naomba niseme kuwa si kweli
kuwa mimi nimekuwa chanzo cha Mgogoro, mie nimesimamia vizuri chama, huko nyuma
watu walizoea kufanya kazi kwa mazoea, ufuatiliaji wangu wa karibu umesababisha
baadhi ya watu kuona kero.
Mwandishi: Zipo taarifa kuwa jambo hili
limetokana na msukumo wa kisiasa, kwa baadhi ya watu walioonesha nia ya kuwania
nafasi ya Ubunge ambayo wewe unayo hadi sasa hapo mwakani, hili nalo
unalisemaje?
Zambi:Mimi ni Mbunge wa Jimbo hili vipindi
viwili, iwapo wananchi wataona nimefanya vyema Chama kinaweza kunisimamisha
tena kipindi cha tatu, suala la jambo hili kuwahusisha wanaotaka kuwania Ubunge
si la kweli, bali wanayo nafasi ukifika muda kuingia katika kinyang’anyiro
atakayefaa ndiye atakayepeperusha bendera ya chama chetu.
Kadhalika
katika kikao hicho ambacho kilianza majira ya saa 2:30 asubuhi na kumalizika
majira ya saa 12:00 jioni kiliamua madiwani hao wafikishwe kwenye kamati ya
maadili ya chama hicho ili hatimaye ikiwezekana maamuzi magumu ya kuwaengua
madiwani hao yapitishwe.
Jimbo la Mbozi Mashariki limebakiwa na Kata 18,baada ya kumegwa kwa wilaya mpya ya Momba ambazo ni Msiya,
Halungu, Itaka, Bara, Nyimbili, Isansa, Igamba,Myovizi, Ihanda, Ipunga, Isandula,Mlangali,Ruanda,
Iyula,Nanyala na Nambizo ambazo zipo chini ya Madiwani wa CCM na kata mbili zilizopo kwenye kata za mjini za Vwawa na Mlowo zinashikiliwa na CHADEMA.
Post a Comment
Post a Comment