Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro akiweka udongo katika kaburi la Shekhe wa wilaya ya Mbeya |
Imamu wa msikiti wa Baraa Bin Azb Ibrahimu Bombo akimwaga machozi wakati akizungumza kwa hisia juu ya kifo cha Shekhe Mketo |
Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro akitoa nasaha mara baada ya mazishi ya Shekhe wa Wilaya ya Mbeya Abubakar Mketo |
SHEKHE wa
wilaya ya Mbeya (BAKWATA)Abubakari Mketo amefariki ghafla mwishoni mwa wiki baada
ya kuanguka wakati akitoa mawaidha makaburini.
Tukio hilo
la aina yake limetokea katika makaburini ya Nonde Jijini Mbeya wakati wa mazishi
ya Mayasa Salmini( Bibi Majuto) aliyefariki katikati ya wiki iliyopita na
mazishi yake kufanyika katika katika makaburi hayo.
Mashuhuda wa
tukio hilo wamedai kuwa mara baada ya kumaliza kuusitiri mwili wa marehemu Bibi
Majuto ndani ya kaburi, Shekhe huyo alisimama na kuanza kutoa mawaidha kwa
waombolezaji waliohudhuria mazishi hayo.
Imeelezwa
kuwa Shekhe Mketo alianza kwa kusema kuwa ‘’kila nafsi lazima itaonja mauti’’
na kuwa si ajabu hata yeye (Shekhe) anayeongea wakati huo anaweza kufa wakati
baada ya kumaliza mazungumzo mbele ya macho yao.
Shuhuda huyo
anaeleza kuwa mara baada ya kumaliza kauli hiyo Shekhe huyo alianguka ghafla na
kukimbizwa katika hospitali ya Rufaa Mbeya ambako ilithibitika kuwa alikuwa
ameshafariki dunia.
Katika mazishi
ya Shekhe huyo ambayo yalihudhuriwa na Mkuu wa mkoa wa Mbeya umati wa watu
waliohudhuria walikuwa na taharuki na kuibua maswali juu ya mazingira ya kifo
hicho.
Mashekhe
mbalimbali waliohudhuria mazishi hayo walisema kuwa kifo hicho kinafundisha
waumini kujiandaa na safari ya kifo ambacho kinaweza kukuta wakati wowote bila kutarajia.
Shekhe wa
msikiti wa Isanga Ibrahimu Bombo alisema kuwa tukio hilo ni dalili pekee ambazo
zinapaswa kuwafundisha waumini wa dini hiyo kujiandaa kwa kufanya matendo mema
kwa kuwa kifo kinaweza kumkuta binadamu mahala popote.
‘’Tujiwekee
maandalizi ya safari ya akhera, hakuna anayejua saa wala tarahe ya kuondoka
kwake duniani, kifo cha Shekhe wetu kitupe mafundisho,’’alisema Shekhe Bombo.
Kwa upande
wake Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro aliwataka kutohusisha kifo hicho na
imani zozote za ushirikina bali waamini kuwa kimetokana na mipango ya Mungu na
kuwa kila mtu ataondoka duniani kwa njia zake.
‘’Nawasihi
ndugu zangu, tusitumie msiba huu kuleta mgongano, yatazungumzwa mengi juu ya
kifo hichi lakini tuamini kuwa Mungu ndiye aliyeamua kumchukua Shekhe wetu kwa
njia hii,’’alisema Kandoro.
Alisisitiza
kuwa jambo linalopaswa kufanywa ni kumuenzi marehemu kutokana na matendo yake
mema ambayo alikuwa akisisitiza kudumisha mshikamano amani na utulivu.
Post a Comment
Post a Comment