Ofisa Ufundi wa TAHA Isaac Ndamanhyilu akiwa katika moja ya mashamba ya Nyanya ambalo TAHA limesaidia mafunzo na teknolojia |
Mkulima wa mbogamboga na matunda Daniel Wabare akiwaonesha wakulima wa mboga mboga na matunda namna ambavyo alifanikiwa katika kilimo cha Nyanya kwa msaada wa Shirika la TAHA |
Mtaalamu wa kilimo kutoka TAHA kanda ya Mashariki Annania Bansimbile akiwaelekeza wakulima namna ambavyo umwagiliaji kwa mfumo wa matone unavyoleta tija kwa kilimo cha Mbogamboga na matunda |
Katibu Tawala wa wilaya ya Mbarali Alfred Mzurikwao akiwapa nasaha wakulima kwenye kilele cha siku ya wakulima Shambani katika kijiji cha Ilaji wilayani Mbarali |
Ofisa Ufundi TAHA Isaac Ndamanhyilu akiwapa zoezi la uelewa wakulima waliohudhuria katika maadhimisho ya siku ya wakulima Shambani katika kijiji cha Ilaji wilayani Mbarali. |
WAKULIMA wa
mbogamboga na matunda mkoani Mbeya wametakiwa kuutumia vyema uwanja wa ndege wa
Kimataifa wa Songwe kwa kuzalisha na kusafirisha mazao yenye ubora ili waweze kujiinua
kiuchumi.
Kauli hiyo
imetolewa na Ofisa Ufundi wa Shirika lisilo la Kiserikali linalojihusisha na
utaalamu na mafunzo ya uzalishaji mazao ya mbogamboga, matunda, maua na viungo (TAHA)
Isaac Ndamanhyilu wakati wa kuadhimisha siku ya wakulima shambani
kijiji cha Ilaji wilayani Mbarali mkoani Mbeya.
Ndamanhyilu alisema kuwa wakulima wa
mbogamboga, maua na matunda mkoani Mbeya wanayo fursa ya nzuri ya masoko kwa
kuutumia uwanja wa Kimataifa wa Songwe kwa kushindana na masoko ya Kimataifa
kuzalisha kwa ubora.
‘’Ardhi ya
mkoa wa Mbeya ni rafiki kwa mazao yote, ikitumiwa vyema kwa kilimo cha
mbogamboga na matunda itakuwa ni mkombozi wetu kiuchumi,’’alisema.
Ndamanhyilu
alisema kuwa kwa kuthamini mpango wa shirika hilo katika kuchangia maendeleo ya
kilimo cha mbogamboga na matunda nchini serikali imetoa ruzuku ya sh.bilioni
1.4 ili kusukuma jitihada za wakulima kujiinua
na kuongeza tija.
Alisema
matarajio ya TAHA ni kuongezeka kwa hamasa ya kilimo na matumizi ya teknolojia
ya umwagiliaji na kilimo cha Matone kwa kutumia mfumo wa usambazaji maji kwa
kutumia mpira katika matuta, ‘’Drip Irrigation’’ ambao humsaidia mkulima kuzalisha
kwa tija.
Naye Mkulima
wa mboga mboga katika kijiji cha Ilaji wilayani Mbarali Daniel Wabare alisema
kuwa kwa kipindi kisichozidi miezi mitatu amemudu kuandaa shamba la nyanya kwa
kutumia utaalamu unaozingatia vigezo vya maandalizi bora ya shamba la
Mbogamboga.
Alisema
ameweza kuandaa shamba la hekari moja kwa gharama ya sh milioni 2.5 ambapo
anatarajia kukusanya zaidi ya sh. milioni 8 na kuwa mafanikio hayo yametokana
na uchaguzi wa mbegu bora, maandalizi ya vitalu, matumizi ya mbolea, maji na
dawa za kuulia wadudu.
Awali
akizungumza katika maadhimisho hayo Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbarali Alfred
Mzurikwao alisema kuwa wakulima wa mbogamboga na matunda wanapaswa kuzingatia
utaalamu kutoka kwa maofisa ugani na kuwataka maofisa ugani kutokaa maofisini
na badala yake watembelee mashambani kukutana na wakulima.
‘’Watumieni
vyema maofisa ugani walioko katika maeneo yenu, nanyi maofisa ugani msikae
maofisini watembeleeni wakulima ili mjue changamoto wanazokutana nazo katika
kilimo,’’alisema.
Post a Comment
Post a Comment