Ads (728x90)












Mbwembwe!! kejeli na vibweka vya michezo katika ligi kuu ya Vodacom vilijiri jana wakati wa mechi kati ya wenyeji Mbeya City na Yanga ya Dar es salaam kwenye uwanja wa kumbukumbu ya Sokoine Jijini Mbeya jana.
Ilikuwa ni hamasa ya aina yake kwa wapenzi na mashabiki wa kila timu hususani kwa mashabiki wa timu wenyeji ambao kwa takribani siku nne walikuwa katika maandalizi ya kuhakikisha wanashinda mechi hiyo ili kuwakoga wenyeji wenzao Prison ambao walkitandikwa mabao 3-0 na timu hiyo kutokea mtaa wa Jangwani.
Kama ilivyo ada kwa timu mbili zenye ushindani mkubwa zinapokutana,, umati mkubwa wa mashabiki walijipanga foleni kuanzia saa tano asubuhi ili kujipatia tiketi za kuingia uwanjani kushuhudia kandanda hiyo iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa na wapenzi wa soka mkoani Mbeya.
Mamia ya wapenzi wa Mbeya City kutoka katikati ya Jiji na vitongoji vyake walijiandaa kwa mechi hiyo kwa muda mrefu ili kuishuhudia timu yao ya Mbeya City ikivunja mwiko wa kufungwa na Yanga katika msimu wa ligi kuu iliyopita ambapo walifungwa goli 2-1 jijini Dar es salaam na kutoa sare katika mechi iliyogubikwa na vituko lukuki katika uwanja wa kumbukumbu ya Sokoine.
Hata hivyo mbinu mbalimbali za kimichezo na zile ambazo zinashabihiana na ushirikina vilionekana kuchukua nafasi katika mchezo huo wa jana ambapo awali siku moja kabla ya mchezo huo wachezaji wa Mbeya City waliingia uwanja wa Sokoine kwa ajili ya kufanya mazoezi majira ya saa moja asubuhi ambapo inaelezwa kuwa walionekana wakifanya mambo yaliyoonekana kama ni vitendo vya ushirikina.
Nao wachezaji wa Yanga ambao waliingia uwanjani humo majira ya saa nne kwa ajili ya mazoezi inadaiwa kuwa walifanya baadhi ya mambo ambayo nayo yanaonekana kuhusiana na mambo ya ushirikina hali ambayo ilitafsiriwa kuwa huenda mechi hiyo ingekuwa na tashwishwi ya aina yake.
Siku ya mechi kama ilivyo ada kwa wapenzi wa Mbeya City walilitawala Jiji kwa mbinja na mavuvuzela kuanzia vitongoji vya Mbalizi, Uyole na maeneo mengine ya pembezoni wa Jiji la Mbeya kama vile Kyela,Rungwe,Chunya, Mbozi na Tunduma.
Maandamano makubwa yalifanywa na mashabiki kutokea maeneo ya Uyole na Mwanjelwa na kusababisha barabara kufungwa kwa muda kutokana na wingi wa watu barabarani.
Hadi kufikia majira ya saa nane mchana uwanja ulikuwa umefurika huku maelfu ya watazamaji wakiwa nje kwenye foleni ya kuingia uwanjani.
Ndani ya uwanja hakukuwa na nafasi hata ya kutema mate kwa jinsi uwanja ulivyojaa huku mageti yote manne ya uwanja huo yakiwa yamefurika mashabiki na wengine wakiminyana milangoni na kuumizana.
Hata hivyo matokeo ya mechi hiyo ambayo yaliwafanya wapenzi na mashabiki wa Mbeya City kufunga midomo yao iliisha kwa bao 3-1.
Mpira ulianza kwa kasi kwa kila upande kulishambulia goli la mwenzie huku Mbeya City wakionekana kucheza kwa kasi zaidi ya Yanga ambao walionekana kama vile wakiwasoma mchezo Mbeya City.
Kasi hiyo ya Mbeya City ilileta patashika katika lango la Yanga ambapo katika dakika ya 6 mchezaji Paul Nonga wa Mbeya City alitikisa wavu wa Yanga lakini kabla hajafunga bao hilo alikuwa ameunawa huku wachezaji wengine wa Mbeya City wakiwa wameotea.
 Ilikuwa ni katika dakika ya 19 ya mcheza mchezaji wa Yanga Simon Msuva aliwainua mashabiki wa timu hiyo ambaop walikuwa wameketi upande wa kusini wa jukwaa la uwanja huo kwa kufunga bao kutokana na pasi kutoka kwa Niyonzima aliyepata krosi kutoka kwa Andrew Cotinho.
Hata hivyo bao hilo liliamsha hasira kwa wapenzi na mashabiki wa Mbeya City walioketi upande wa kaskazini mwa uwanja kwa kurusha chupa za maji uwanjani na kuibua taharuki katika mchezo huo.
Baada ya bao hilo Mbeya City walionekana kama vile wameaamka na kuanza kulishambulia lango la Yanga bila mafanikio ambapo wachezaji wake Paaul Nonga,Abdalla Seif,Deus Kaseke na Rafael Alpha hawakuweza kulifikia lango la yanga baada ya kudhibitiwa na walinzi wa Yanga Juma Abdul,Oscaar Joshua, Kelvin Yondani na Nadir Canavaro.
Hadi kipenga cha mapumziko cha mwamuzi Athumani Lazi kutoka Mji kasoro bahari Moro kinapulizwa Yanga alikuwa kifua mbele kwa bao 1-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Yanga wakiwa wamekwisha wasoma wapinzani wao Mbeya City ilihali Mbeya City wakihitaji kusawazisha bao na kuongeza.
Ilikuwa ni dakika ya 61 mchezaji Halfani Ngasa aliipatia Yanga bao la pili baada ya kuunganishiwa krosi kutoka kwa Niyonzima ambapo golikipa wa Mbeya City David Burhani aludaka mpira na kuuchezea kisha akautema ndipo Ngasa akausindikiza wavuni.
Bao hilo liliwafanya wachezaji wa Mbeya City kukosa maelewano wakicheza bila mpangilio bhali ambayo iliwafanya timu ya Yanga kuutawala mchezo kwa muda mrefu,
Hata hivyo ilikuwa ni dakika ya 70 mchezaji wa Mbeya City Peter Mapunda aliwainua mashabiki wa timu hiyo kwa kufunga bao zuri la kichwa baada ya kupata krosi kutoka kwa winga wa kulia Themi Felix na kurejesha uhai kwa mashabiki waliokuwa wamenyamaza kwa muda mrefu pamoja na wachezaji ambao walikuwa wameanza kukosa matumaini.
Kwa kipindi hicho mchezo ulikuwa ni mkali huku rafu za hapa na pale zikitawala uwanjani na kusababisha refarii Lazi kuwazawadia kadi ya Njano Juma Abdul wa Yanga aliyemfanyia madhambi Abdallah S eif wa Mbeya City ambapo pia mchezaji wa Mbeya City Richard Peter naye alizwadiwa kadi ya njano kwa kumchezea rafu Cotinho ambaye alitoka uwanjani kwa maumivi na nafasi yake kuchukuliwa na Danny Mrwanda.
Mchezaji mwingine aliyezawadiwa kadi ya njano ni Peter Mapunda wa Mbeya City aliyemfanyia madhambi Danny Mrwanda.
Yanga wakiwa wakitaka kuongeza goli na Mbeya City walijitahidi kulinda goli lao huku wakitafuta upenyo wa kulisogelea goli la Yanga bila mafanikio.
Ilikuwa ni dakika ya 80 ambapo mchezaji wa Yanga Amis Tambwe alipoandika bao la 3 na la kufunga karamu ya magoli kwa siku hiyo baada ya kupokea pasi kutoka kwa Niyonzima na kusababisha baadhi ya mashabiki wa Mbeya City kukata tamaa na kuanza kutoka uwanjani.
Hadi Kipyenga cha mwisho kinapulizwa Yanga walikuwa kifua mbele kwa bao 3 dhidi ya 1 la Mbeya City.

Post a Comment

Post a Comment