Ads (728x90)


‘’TULINYESHEWA mvua pamoja, tulipigwa na baridi tukiwa pamoja, kuna maeneo mengine tulipigwa mawe na hata kuzomewa tukiwa sote, tuliwakiwa na jua tukalala porini, leo hii Jakaya yuko Ikulu sisi bado tupo barabarani!!!
‘’ Nazungumza haya kwa uchungu mkubwa , tunatumika sisi mnapofanikiwa mnatusahau kama mafanikio yenu yametokana na sisi, CCM haiwezi kujivunia mafanikio yake bila kututaja sisi,tumekuwa ndiyo nembo ya chama hiki, tumeingia humu kukiwa giza totoro, hakukuwa na mshahara wala chochote wengine tulilazimishwa hata kuacha kazi kwa ajili ya hiki chama!!
‘’Mzee Kinana unakumbuka wakati ule unatufundisha kule jeshini kwmaba lazima tuwe wakweli, na mimi nasema ukweli  uliopo ndani ya moyo wangu sikwepeshi maneno, jamani!! Eeh tukumbukeni hata angalu tunapostaafu, tustaafu vizuri, angalieni hawa wasanii wameingie leo katika chama, mnajua hii kwao ni gharama kubwa kazi zao za usanii zitakuwa katika mazingira magumu iwapo hamtawaenzi na kuwawekea mazingira mazuri.
‘’Ukweli ni kwamba kwa kuwa wamejionesha wao ni CCM sasa hivi kazi zao zitanunuliwa na wanaCCM tu, lakini tukumbuke kuwa CCM sio Watanzania wote, watajengewa chuki na uadui na kazi zao zitakuwa ngumu kuuzika!!
‘’Mwangalieni huyu kijana anaitwa Maro aliipigia kampeni sana CCM wakati ule wa uchaguzi mkuu leo hii yuko wapi anaishi katika mazingira magumu kwa kuwa alijiweka wazi, tuambieni CCM mmemfanyia nini kijana huyu? Ni baadhi ya maneno yaliyogusa hisia ya Kapteni John Komba alipoamua kutoa dukuduku lake wakati wa hafla fupi iliyoandaliwa na CCM kati ya waandishi wa habari na Wasanii kwenye ukumbi wa Mkapa jijini Mbeya jana usiku.
Kapteni John Komba alienda mbali zaidi na kumueleza Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana kwamba wao Bendi ya TOT imekuwa ikitumika kwa kampeni kwa miaka mingi bila mafanikio yoyote kwa wasanii wa bendi hiyo na kuwa tangu wakati wa Mzee Mwinyi, Mkapa na sasa Rais Jakaya Kikwete hakuna manufaa yoyote kwa wasanii hao ambao wamechangia kwa asilimia kubwa ushindi wa CCM.
Alisema yeye binafsi hana matatizo sana bali kinachomuuma ni mustakabali wa wasanii ambao ndio kwanza wanachipukia na wanategemea kipato chao kwa kazi za usanii na kuwa kuna jitihada za CCM kuangalia vyema wanaosaidia kukifikisha hapo chama hicho watazamwe kwa jicho la yakini.
Huku akishangiliwa na wasanii ilhali Katibu Mkuu wa CCM Kinana akiwa amejiinamia kwa tafakari juu ya maneno hayo yalaiyowagusa wasanii wengi waliohudhuria hafla hiyo, Kapteni Komba alichukua fursa hiyo pia kuwasemea waandishi wa Habari ambao nao wamekuwa wakitumika kwenye kampeni baadaye wanasahauliwa.
‘’Hata Waandishi wa Habari, wamefanya kazi kubwa sana kuwafikisha hapo mlipo lakini leo hii mko kwenye neema mnaweza kusema kuna jambo gani kubwa walionufaika nalo? Alihoji Kapteni Komba.
Naye Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Nape Nnauye alisema kuwa kuna haja ya chama hicho kuangalia namna nyingine ya kuwajali wale wanaosaidia kukifikisha hapo CCM na kutolea mfano wakati wa makatibu wakuu waliopita kwa kuwataja majina akina marehemu Horace Kolimba,Philip Mangula, Yusuf Makamba,Wilson Mukama na sasa Kinana.
Alisema tangu alipoingia Kinana kumekuwa na mwanga kidogo wa mafanikio hivyo kwa kuwa anayo fursa ya kuzungumza na Mwenyekiti wa CCM Taifa (JK) amueleze kilio hicho na kuwa hiyo ndiyo hali na mazingira halisi inayowakumba watu wanaotumiwa kuisaidia CCM kwa kampeni na kuifikisha hapo ilipo.
Katika maadhimisho ya miaka 37 ya CCM wasanii wa Bongo Movie Single Mtambalike( Richie) JB,Irene Uwoya,Amanda, Omar Mrisho(SLIM),Haj Rajab,Banana Zorro, Haj Rajab na Wastara Juma walijiunga na chama hicho na kukabidhiwa kadi na Mwenyekiti wa CCM Taifa Rais Jakaya Kikwete.

Mjumbe wa NEC na Mbunge wa Mbinga Kapteni John Komba katika moja ya vikao vya Bunge mjini Dodoma
Msanii wa Bongo Movie Banana Zorro akiwa katika uwanja wa Sokoine jana, Banana na wasanii wenzie walijiunga na CCM na kukabidhiwa kadi na Mwenyekiti wa CCM Taifa Rais Jakaya Kikwete

Wastara Juma na JB pamoja na wasanii wenzie wa Bongo Movie wakiwa katika uwanja wa Sokoine ambako walikabidhiwa kadi na Rais Jakaya Kikwete.

Post a Comment

Post a Comment