‘’TULINYESHEWA
mvua pamoja, tulipigwa na baridi tukiwa pamoja, kuna maeneo mengine tulipigwa
mawe na hata kuzomewa tukiwa sote, tuliwakiwa na jua tukalala porini, leo hii
Jakaya yuko Ikulu sisi bado tupo barabarani!!!
‘’
Nazungumza haya kwa uchungu mkubwa , tunatumika sisi mnapofanikiwa mnatusahau
kama mafanikio yenu yametokana na sisi, CCM haiwezi kujivunia mafanikio yake
bila kututaja sisi,tumekuwa ndiyo nembo ya chama hiki, tumeingia humu kukiwa
giza totoro, hakukuwa na mshahara wala chochote wengine tulilazimishwa hata
kuacha kazi kwa ajili ya hiki chama!!
‘’Mzee
Kinana unakumbuka wakati ule unatufundisha kule jeshini kwmaba lazima tuwe
wakweli, na mimi nasema ukweli uliopo
ndani ya moyo wangu sikwepeshi maneno, jamani!! Eeh tukumbukeni hata angalu
tunapostaafu, tustaafu vizuri, angalieni hawa wasanii wameingie leo katika
chama, mnajua hii kwao ni gharama kubwa kazi zao za usanii zitakuwa katika
mazingira magumu iwapo hamtawaenzi na kuwawekea mazingira mazuri.
‘’Ukweli ni
kwamba kwa kuwa wamejionesha wao ni CCM sasa hivi kazi zao zitanunuliwa na
wanaCCM tu, lakini tukumbuke kuwa CCM sio Watanzania wote, watajengewa chuki na
uadui na kazi zao zitakuwa ngumu kuuzika!!
‘’Mwangalieni
huyu kijana anaitwa Maro aliipigia kampeni sana CCM wakati ule wa uchaguzi mkuu
leo hii yuko wapi anaishi katika mazingira magumu kwa kuwa alijiweka wazi,
tuambieni CCM mmemfanyia nini kijana huyu? Ni baadhi ya maneno yaliyogusa hisia
ya Kapteni John Komba alipoamua kutoa dukuduku lake wakati wa hafla fupi
iliyoandaliwa na CCM kati ya waandishi wa habari na Wasanii kwenye ukumbi wa
Mkapa jijini Mbeya jana usiku.
Kapteni John
Komba alienda mbali zaidi na kumueleza Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana
kwamba wao Bendi ya TOT imekuwa ikitumika kwa kampeni kwa miaka mingi bila
mafanikio yoyote kwa wasanii wa bendi hiyo na kuwa tangu wakati wa Mzee Mwinyi,
Mkapa na sasa Rais Jakaya Kikwete hakuna manufaa yoyote kwa wasanii hao ambao
wamechangia kwa asilimia kubwa ushindi wa CCM.
Alisema yeye
binafsi hana matatizo sana bali kinachomuuma ni mustakabali wa wasanii ambao
ndio kwanza wanachipukia na wanategemea kipato chao kwa kazi za usanii na kuwa
kuna jitihada za CCM kuangalia vyema wanaosaidia kukifikisha hapo chama hicho
watazamwe kwa jicho la yakini.
Huku
akishangiliwa na wasanii ilhali Katibu Mkuu wa CCM Kinana akiwa amejiinamia kwa
tafakari juu ya maneno hayo yalaiyowagusa wasanii wengi waliohudhuria hafla
hiyo, Kapteni Komba alichukua fursa hiyo pia kuwasemea waandishi wa Habari
ambao nao wamekuwa wakitumika kwenye kampeni baadaye wanasahauliwa.
‘’Hata
Waandishi wa Habari, wamefanya kazi kubwa sana kuwafikisha hapo mlipo lakini
leo hii mko kwenye neema mnaweza kusema kuna jambo gani kubwa walionufaika
nalo? Alihoji Kapteni Komba.
Naye
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Nape Nnauye alisema kuwa kuna haja
ya chama hicho kuangalia namna nyingine ya kuwajali wale wanaosaidia
kukifikisha hapo CCM na kutolea mfano wakati wa makatibu wakuu waliopita
kwa kuwataja majina akina marehemu Horace Kolimba,Philip Mangula, Yusuf
Makamba,Wilson Mukama na sasa Kinana.
Alisema
tangu alipoingia Kinana kumekuwa na mwanga kidogo wa mafanikio hivyo
kwa kuwa anayo fursa ya kuzungumza na Mwenyekiti wa CCM Taifa (JK)
amueleze kilio hicho na kuwa hiyo ndiyo hali na mazingira halisi
inayowakumba watu wanaotumiwa kuisaidia CCM kwa kampeni na kuifikisha
hapo ilipo.
Katika
maadhimisho ya miaka 37 ya CCM wasanii wa Bongo Movie Single Mtambalike(
Richie) JB,Irene Uwoya,Amanda, Omar Mrisho(SLIM),Haj Rajab,Banana Zorro, Haj
Rajab na Wastara Juma walijiunga na chama hicho na kukabidhiwa kadi na
Mwenyekiti wa CCM Taifa Rais Jakaya Kikwete.
Mjumbe wa NEC na Mbunge wa Mbinga Kapteni John Komba katika moja ya vikao vya Bunge mjini Dodoma |
Msanii wa Bongo Movie Banana Zorro akiwa katika uwanja wa Sokoine jana, Banana na wasanii wenzie walijiunga na CCM na kukabidhiwa kadi na Mwenyekiti wa CCM Taifa Rais Jakaya Kikwete |
Wastara Juma na JB pamoja na wasanii wenzie wa Bongo Movie wakiwa katika uwanja wa Sokoine ambako walikabidhiwa kadi na Rais Jakaya Kikwete. |
Post a Comment