Ads (728x90)

Kocha wa timu ya Yanga Hans Pluijm akiwa amejishika kichwa baada ya Yanga kuwa nyuma kwa bao 2-1 dhidi ya Prison hadi dakika ya 86.

Kocha wa Yanga Pluijm akiwa amechanganyikiwa asijue la kufanya baada ya washambuiliaji wa Yanga kukosa magoli mara kadhaa  wakiwa wamebaki na golikipa wa Prison ana kwa ana.


Mshabiki mashuhuri wa Yanga almaarufu Mama Yanga a,kiwa ameanguka baada ya timu yake kufungwa bao la pili na kukimbizwa na gari la wagonjwa Hospitali ya Rufaa Mbeya.

Mshabiki mashuhuri wa Yanga Ali Yanga akimwangalia mshabiki mwenzie Mama YANGA wakati akipakizwa kwenye gari la wagonjwa na kupelekwa hospitali ya Rufaa Mbeya.

Kocha wa Yanga Pluijm akijaribu kuwaelekeza wachezaji wake akiwa kwenye benchi la ufundi la timu yake.




Kikosi cha timu ya Yanga

Kikosi cha timu ya Prison
Almanusura histroria ya mwaka 2003 ijirejee jana katika uwanja wa kumbukumbu ya Sokoine ambapo timu ya Prison iliwachezesha kwata vijana hao wa mtaa wa Jangwani kwa mabao 2-0, mabao yaliyofungwa na Paul Mokiwa ambaye kwa sasa ni Afande wa Jeshi la Magereza mkoani Mbeya.
Katika mchezo wa jana hali haikuwa kama ilivyotarajiwa ambapo wanajangwani walishajijengea mazoea ya kujinyakulia pointi zote tatu kila wanapokutana uso kwa uso na timu ya Prison hali iliyowafanya mashabiki wahisi kuwa timu ya Prison ni tawi la Yanga.
‘’Prison anaweza kukaza kwa Simba hata kuifunga ila ikija Yanga haina ubavu wowote lazima ifungwe hata kama iko kwenye hatari ya kushuka daraja,’’ alisema mmoja wa mashabiki wa Soka Jijini Mbeya aliyejitambulisha kwa jina la Mwaijande.
Katika mchezo wa jana kwenye uwanja wa kumbukumbu ya Sokoine Yanga ndiyo iliyokuwa ya kwanza kupata goli, ikicheza chini ya washambuliaji mahiri akina Donald Ngoma,Harun Niyonzima,Amis Tambwe,Isoufou Boubacar na  Vicent Bossou.
Ilikuwa ni dakika ya 36 ya mchezo Niyonzima alipoichonga krosi safi upande wa kulia na kuunganisha mpira uliotua kichwani kwa  Tambwe aliyekuwa kwenye boksi na kuusindikiza mpira wavuni akimuacha golikipa wa Prison Beno Kakolanya akichupa bila mafanikio.
Hata hivyo goli hilo la Yanga lilishangiliwa kwa takribani dakika 4 tu ambapo iliamsha hamasa na munkari wa washambuliaji wa timu ya Prison akina Lambert Sabiyanka, Freddy Chudu, Mohamed Mkopi na Jeremiah Juma wakilishambulia goli la Yanga kama nyuki.
Mashambulizi ya Prison dhidi ya Yanga yalizaa matunda mnano dakika 41 ambapo mchezaji Jeremiah Juma alifunga bao zuri la kichwa baada ya kuunganishiwa pasi ya Mohamed Mkopi kutoka upande wa kushoto.
Hadi mapumziko timu zote zilitoka sare ya bao 1-1.
Kipindi cha pili kilianza kwa mwendo wa wastani huku ikionekana kama timu zikitegeana kwa mashambulizi, walinzi  wa Prison Laurian Mpalile, Jumanne Elfadhil,Nurdin Chona na James Mwasote walikuwa na kazi ya ziada ya kuokoa mashuti ya wachezaji wa Yanga ambao mara kadhaa walilikaribia eneo la hatari na mipira ya kuokolewa.
Dakika ya 63 Mohamed Mkopi aliipatia Prison bao la pili lililotokana na faulo aliyofanyiwa mchezaji wa Prison Juma Seif Kijiko na hivyo kuifanya Prison iongoze kwa bao 2-1.
Goli hilo lilisababisha wapenzi na wanazi wa Yanga kuanza kukata tamaa ya ushindi kwa siku hiyo huku wachezaji wa timu ya Prison wakionesha ari kubwa ya kuuwania ushindi dhidi ya Yanga wakitamani kurejesha  historia ya miaka 12 iliyopita mwaka 2003 ambapo Yanga ililala kwa bao 2-0.
Tafrani ya kufungwa ilisababisha mshabiki mmoja maarufu wa Yanga Mama Yanga kuanguka chini na kupoteza fahamu na kuchukuliwa na gari la wagonjwa kukimbizwa Hospitaliu ya rufaa Mbeya huku mshabiki mkubwa wa Yanga maarufu kwa jina la Ali Yanga akionekana kuhaha kila kona mithili ya mtu aliyechanganyikiwa akili.
Dakika zilizidi kusonga huku Yanga ikionekana kukata tama ilhali timu ya Prison ikijionea mwanga wa matumaini ya ushindi ndipo zikiwa zimesalia dakika 4 kabla ya kumalizika mchezo mnamo dakika 86 mlinzi wa Prison James Mwasote aliunawa mpira eneo la adhabu na hivyo refarii wa mchezo huo kutoa penati iliyopigwa na Simon Msuva na kufunga goli.
Goli hilo lilileta uhai kwa benchi la ufundi la Yanga lililokuwa chini ya Kocha Hans Pluijm na kocha msaidizi Juma Mwambusi ambao kwa muda wote wa mchezo walikuwa wanashindwa kukaa kwenye benchi wakihaha kila kona kuwapanga wachezaji wao waliokuwa butu safu ya ushambuliaji.
Hadi Kipyenga cha mwisho kinapulizwa Prison 2 Yanga 2.

Post a Comment

Post a Comment