Mwananchi wa kijiji cha Songwe Asajile Kandonga akichangia hoja kwenye mkutano wa hadhara wa kijiji hicho kuhusu mgogoro wa ardhi wa mashamba ya Kaloleni
WANANCHI wa
kijiji cha Songwe Kati kilichopo katika kata ya Songwe wilaya ya Mbeya mkoani
Mbeya wamewataka watendaji wa Halmashauri ya kijiji hicho waachie ngazi
kutokana na kuruhusu upotevu wa fedha zaidi ya sh. milioni 50 zinazotokana na
fidia ya mashamba ya kijiji hekari 15.
Wakizungumza
kwenye mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na Diwani wa Kata hiyo Ayasi Ramadhani
walidai watendaji hao ikiwemo kamati ya ufuatiliaji wa fidia walishindwa
kufanya tathmini ya hekari za mashamba ya kijiji ambazo ni hekari 15.4 na
badala yake wamefanya tathmini hekari 5.6.
‘’Hekari
hizo 5.6 tumepata kiasi cha sh mil 27, lakini tulikuwa na jumla ya hekari 21,
hekari zingine 15.4 hazijulikani zimepotelea wapi na watendaji wa kijiji
walitathmini namna gani,’’ alisema Asajile Kandonga mkazi wa kijiji hicho.
Naye Cletus
Nyilela alisema kuwa wakazi wa kijiji hicho walikuwa na hekari za mashamba
ambazo zilikuwa zinakodishwa kwa wananchi na fedha zake zinatumika kwa ajili ya
maendeleo ya kijiji lakini watendaji hao wa kijiji wameachia kiasi cha hekari
15.4 na hivyo kukikosesha kijiji zaidi ya milioni 50.
Alisema kuwa
kamati hiyo imetumia fursa hiyo kuhujumu mashamba ya kijiji kwa manufaa yao
hivyo kutokana na hali hiyo wanapaswa kuachia ngazi na kuchukuliwa hatua za
kisheria, ‘’ Hawa ni wabadhirifu na wahujumu wa uchumi wachukuliwe hatua za
kuhujumu mali ya kijiji,’’ alisema Kipenda John mkazi wa kijiji hicho.
Awali
akisoma taarifa za mapato na matumizi ya kijiji hicho Mwenyekiti wa Kamati ya
Uchumi na Fedha Paulo Mwasuka alisema kuwa jumla y ash mil 28.9 zilitokana na
mapato mbalimbali ya kijiji ambapo kati ya hizo kiasi cha sh mil 27.7
kilitokana na fidia ya mashamba hekari 5.6.
Baada ya
taarifa hiyo wananchi walikuja juu ya kudai kuwa kiasi hicho cha hekari za
mashamba si halisi kwa kuwa eneo lao la mashamba ni kubwa ukilinganisha na
ukubwa huo wa hekari 5.6.
Diwani wa
kata hiyo Ayasi Ramadhan alidai kuwa alienda kupima eneo hilo akiongozana na
baadhi ya wazee wa kijiji hicho kwa hatua za miguu na kukuta jumla ya hekari 28
na baadaye walipima kwa futi kisha wakapima kwa kipimo cha GPS na kukuta jumla
ya hekari 33.83.
Ramadhani alisema kuwa kutokana na hali hiyo alibaini kuwa kuna udanganyifu uliofanyika
hivyo alilazimika kuunda kamati ya watu 7 watakaofuatilia tatizo hilo huku
Halmashauri ya kijiji na wafuatiliaji wa fidia wa awali wakilazimika kukaa
pembeni kupisha uchunguzi wa kamati hiyo ambayo itafanya kazi kwa siku 14.
|
Post a Comment
Post a Comment