Ads (728x90)



HATIMAYE Ramadhan Mtoro Ongala hatunaye tena duniani ameaga dunia usiku wa kuamkia leo jijini Dar,alizaliwa miaka 63 iliyopita katika mkoa wa Kivu nchini DRC wakati huo ikiitwa Belgian Congo kabla ya kuitwa Zaire ambayo sasa ni DRC, familia ya Dkt.Remmy ambao ni wazazi wake waliamua kuhamia Kisangani wakitokea katika eneo lililoitwa Kindu ambalo si mbali na mpakani mwa Tanzania.

Zipo taarifa nyingi zinazohusiana na uzawa wa Dkt. Remmy ambaye jina hilo la Dkt,lilishamiri zaidi alipoingia Tanzania lakini historia ya jina hilo inaelezwa kuwa kabla ya kuzaliwa kwake mama yake alipata ujauzito mara kadhaa ambapo mara zote watoto waliozaliwa walifariki dunia.

Kutokana na hali hiyo mama huyo aliamua kujihami kwa kuhangaika kwa waganga wa kienyeji ili apate ufumbuzi wa tatizo lake ili mtoto atakayezaliwa aendelee kuishi, inadaiwa kuwa mganga huyo alimpa masharti kwamba wakati wa kujifungua asiende hopitali bali akajifungulie vichakani,na kumwambia kuwa mtoto atakayezaliwa asimkate nywele zake,(ndio asili ya Dkt.Remmy kuwa na nywele nyingi kwa muda mrefu).

Aidha Dkt. Remmy mwenyewe alikuwa akisema kuwa awali wakati anakua alikuwa akijisikia aibu kuwa na nywele ndefu (rasta) lakini baadaye alianza kuzipenda baada ya kuibuka kwa mtindo wa RASTA ulioasisiwa na mfalme wa Raggae duniani Hayati Robert Nesta Marley maarufu kwa jina la Bob Marley.

Dkt Remmy alianza kuikubali hali hiyo na kuizoea na hata kujivunia kuwa katika hali hiyo kutokana na wimbi la vijana kuiga kwa kasi mtindo huo wa nywele sehemu kubwa katika nchi za Afrika na kwingineko duniani.

Kadhalika kulingana na taarifa kutoka vyanzo mbalimbali vya habari inadaiwa kuwa Dkt.Remmy alizaliwa akiwa na meno mawili ya mbele hali ambayo ilitafsiriwa na jamii ya watu wa DRC kuwa baadaye angekuwa mganga na hiyo ndiyo hasa sababu ya kuendelea kuitwa jina hili la Dkt.Remmy Ongala katika muziki, ingawa hakujihusisha na mambo ya uganga kama ilivyobashiriwa kutokana na uzawa wake.

Inaelezwa kuwa asili ya yeye kuwa mwanamuziki imetokana na urithi kutoka kwa baba yake mzazi Mzee Ongalla ambaye ndiye alimfundisha mambo ya muziki tangu akiwa mdogo na aliamini kuwa alizaliwa ili awe mwanamuziki na kujiendeshea maisha yake kwa njia ya muziki na hivyo ndivyo ilivyokuwa hadi kifo chake usiku wa kuamkia leo Disemba 13 2010.

Lakini matunda ya mafunzo aliyoyatoa kwa mwanawe,Mzee Ongala hakuweza kuyafaidi kwani wakati Dkt. Remmy akiwa na umri wa miaka sita tu mzee huyo alifariki dunia akiwa ameshaaza shule ya msingi huko Kisangani,kama ilivyokuwa ada kwa familia za kimaskini mara baada ya baba yake kufariki dunia mama yake alishindwa kumuendeleza mwanaye kimasomo na hivyo kulazimika kukatisha masomo.

Dkt.Remmy alijeindeleza mwenyewe katika mambo ya muziki hadi miaka ya 60 ambapo tayari alikuwa na uwezo wa kupiga gitaa.

Wakati anatimiza miaka 17 tu tangu azaliwe mwaka 1964 Dkt. Remmy alipata pigo jingine katika maisha yake ambapo mtu pekee aliyemtegemea kama mlezi na muangalizi mkuu wa maisha yake yeye pamoja na wadogo zake, mama yake mzazi naye alifariki dunia na hivyo kumuachia simanzi na majonzi tele ambayo yaliyoaambatana na kuachiwa dhamana kubwa ya kuilea familia aliyoachiwa na wazazi wake yeye akiwa ndiye kinara akisimamia wadogo zake.

Ikumbukwe kuwa Dkt.Remmy alikatisha masomo na hakuwa na ujuzi wowote na hivyo kulazimika kuhaha huku na huko akijitafutia riziki bila kuwa na ujuzi wala elimu yoyote ambapo njia pekee aliyoiona inaweza kumuendeshea maisha yake ni kupitia muziki,ule msemo maarufu usemao kuwa kila mwenye kujitahidi hufanikiwa,ulidhihiri kwa Dkt.Remmy ambaye kwa kutumia ujuzi wake wa kulicharaza gitaa na kupiga ngoma wananchi wa Zaire alimudu kuteka hisia za mashabiki wa muziki kwa kutoa burudani na kukubalika miongoni mwa wapenda muziki wa nchini Zaire.

Alipata fursa ya kutumbuiza katika hoteli mbalimbali na kupata mialiko sehemu nyingine nchini humo akiwa na bendi yake iliyokusanya vijana wenzake iliyojulikana kwa jina la Bantu Success, kwa miaka mingi iliyofuatia Dkt.Remmy alijijengea umaarufu katika nchi ya Zaire.

Dkt. Remmy pamoja na sehemu kubwa ya ujuzi wa kupiga gitaa uliotokana na utundu wake alipata kusema kuwa muziki maarufu kutoka nchini Cuba ambao ulivuma wakati huo barani Africa ndio ulimuwezesha kujifunza mbinu mpya na ya kipekee katika upigaji wa gitaa.

Tofauti na wanamuziki wengine ambao tumezoea kusikia kuwa walianzia kuimba nyimbo za dini, Dkt.Remmy alipata kusema kuwa uimbaji wa Franco na Kabasele ulimfanya apate mtindo wa uimbaji ambao ndio huo aliokuwa nao hadi anakumbana na kifo chake Disemba 13 2010.

Historia inaonesha kuwa Dkt. Remmy aliingia jijini Dar es salaam kwa mara ya kwanza alipoitwa na mjomba wake Mzee Makassy ambaye alikuwa na bendi yake maarufu jijini Orchestra Makassy mwaka 1978 ili aje ajiunge na bendi maarufu ya wakati huo,Orchestra Makassy.

Bendi hiyo ya Orchestra Makassy ilimilikiwa na mjomba wake Dkt.Remmy, na hiyo ndiyo ikawa safari yake ya maisha akiwa nchini Tanzania na kwa mara ya kwanza aliandika wimbo na kuuimba ujulikanao kama ''SIKU YA KUFA'' ikiwa ni kumbukumbu ya rafiki yake mpendwa aliyefariki dunia na hivyo kujipatia umaarufu mkubwa katika muziki.

Akiwa nchini Dkt.Remmy alidumu katika bendi ya mjomba wake kwa miaka mitatu hadi mwaka 1981 na baadaye kuhamia katika bendi ya Super Matimila iliyokuwa na makazi yake mjini Songea mkoani Ruvuma ambayo kwa wakati huo ndio kwanza ilikuwa inachipukia.

Wakati Dkt.Remmy akihamia Super Matimila mjomba wake Mzee Makassy alihamishia bendi yake nchini Kenya, Bendi ya Super Matimila ilijipatia umaarufu mkubwa chini ya Dkt.Remmy,ikiwa chini ya Dkt.Remmy aliibadilisha jina na kuiita Super Matimila badala ya Orchestra ambapo jumla ya nyimbo zake zilikuwa ni zile za kijamii zilizokuwa zikitoa mafunzo.

Watanzania watamkumbuka Dkt.Remmy kwa umahiri wa kutunga mashairi ya nyimbo zake katika kutoa ujumbe mahsusi kwa umma na kujenga uzalendo na uhalisi wa Mtanzania katika harakati za maendeleo ya kila siku.

Dkt Remmy alianza kupata mialiko mbalimbali ya ndani na nje ya nchi ambapo aliwahi kusema kuwa aliwahi kumpa zawadi ya kanda ya nyimbo zake rafiki yake mzungu aliyekuwa anarejea kwao Uingereza kutokea nchini ambapo naye alipofika kule aliwapatia jamaa watu wa World Of Music Arts and Dance (WOMAD) ambalo ni shirika linalokuza vipaji vya wanamuziki na wasanii mbalimbali kutoka katika nchi zinazoendelea.

WOMAD walivutiwa na nyimbo za bendi hiyo na hivyo kutoa mwaliko katika maonesho ya mwaka 1988 yaliyofanyika barani Ulaya,baada ya kurudi huko Super Matimila ilitoa nyimbo kadhaa zikiwemo zile maarufu katika albamu ya NALILIA MWANA ambako kulikuwa na nyimbo kadhaa kama vile MNYONGE HANA HAKI,USIWE NDUMILA KUWILI.

Mialiko kutoka kwa WOMAD iliendelea ambapo mwaka uliofuata wa 1989 Super Matimila walialikwa tena Ulaya ambapo pia walipata fursa ya kurekodi katika studio za kisasa kwenye studio maarufu iliyokuwa ikimilikiwa na mwanamuziki maarufu nchini humo Peter Gabriel ya Real World Studios ambapo zilisikika nyimbo za KIPENDA ROHO ambayo inadaiwa kuwa ilikuwa maalumu kwa mkewe mzungu raia wa Uingereza ambaye kwa wakati huo tayari walikuwa wamezaa watoto watatu.

Kuanzia hapo ubora wa muziki wake ulisababisha kuanzisha safari nyingine za kurekodi nyimbo katika studio za Real World Studio ambapo walirekodi albamu iliyojulikana kwa jina la MAMBO ambao ulikuwa na nyimbo kama MAMBO ulioimbwa kwa lugha ya kiingereza,No ,Money No Life, One World.

Dkt.Remmy hakuishia hapo aliendelea kukonga nyoyo za wasikilizaji wake kwa rika tofauti baada ya kutoka na kibao maarufu kilichojulikana kwa jina la KWA SOKSI ambao pamoja na kupigwa vita na baadhi ya watu lengo lake lilikuwa ni kuhimiza matumizi ya mipira ya kiume kwa ajili ya kujikinga na gonjwa hatari la UKIMWI.

Safari ya kimuziki wa kidunia wa Dkt.Remmy ilimalizika na kuamua kujiingiza katika nyimbo za Injili kutokana na kile kilichoelezwa kuwa umegubikwa na mambo ya kidunia ambayo hayana sura nzuri mbele za Mungu akaamua kuokoka na kutubu dhambi zake na hatimaye akaanza kuimba nyimbo za kumuabudu Mungu.

Hadi kifo chake Dkt.Remmy alikuwa amekwishatoa albamu aliyoiita KWA YESU KUNA FURAHA ambapo alikuwa mbioni kutoa albamu yake ya pili.

Hayati Remmy Ongala alikuwa anaishi jijini Dar es salaam katika eneo la Sinza kwa REMMY ambako umaarufu wa eneo hilo umetokana na yeye kuishi maeneo hayo.

Bwana alitoa na Bwana Ametwaa...

Post a Comment

  1. "Siku ya kufa wandugu kwaheri...siku ya kufa nakuwa nyama ya udongo,marafiki zangu watanikimbia....".

    Kifoo kifoo kifo hakina huruma, ni kama vile aliimba miaka mingi nyimbo aliimba miaka mingi lakini zote zilikuwa na ujumbe unaofanana juu ya kifo, aliimba kwa hisia na ufasaha wa hali ya juu akielezea namna kifo kilivyokuwa kikiwatenganisha watu wapendanao...leo hii hatunaye Dk.Remmy Ongala hatutamuona tena maisha yote

    ReplyDelete