Eva Kleruu akiwa na Mwandishi wa makala haya alipokuwa Mbeya |
Eva Kleruu na Amani Mwamwindi baada ya kukutana |
SIMANZI na machozi yalibubujika wakati
familia mbili za Dk Wilbert Kleruu na Said Mwamwindi zilipokutana juzi mjini
Iringa kwa ajili ya maridhiano yaliyoondoa tofauti zao.
Dk Kleruu aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa
Iringa aliuawa kwa kupigwa risasi ya kichwa Desemba 25, 1971 na Mamwindi
aliyekuwa mkulimaa maarufu wa mahindi katika kijiji cha Isimani, wilayani
Iringa.
Tangu kifo cha mkuu wa mkoa huo kitokee
miaka 43 iliyopita, kabla ya kukutana juzi, familia hizo mbili hazikuwahi
kukutana.
Watoto wa kwanza wa familia hizo, Eva
Kleruu (56) na Amani Mwamwindi (63) ambaye pia ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya
Iringa kwa niaba ya familia zao walikutana na kufanya maridhiano hayo.
Maridhiano hayo yalifanyika katika ofisi
ya Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa, mjini Iringa juzi.
Mtoto wa kwanza wa Dk Kleruu, Eva alisema;
“tumekuwa tukikumbuka historia ya maisha yetu na jinsi marehemu baba yetu
alivyouawa.”
Huku akitetemeka na kuongea huku akitokwa
na machozi, Eva alisema tukio hilo lilikuwa likiifaanya familia ya Dk Kleruu
iogope kuja Iringa.
“Pamoja na hofu hiyo niliweka nadhiri
kwamba ipo siku nitafika Iringa na kutembelea sehemu ambayo marehemu baba yangu
aliuawa katika shamba la Mwamwindi,” alisema.
Alisema baada ya kutembelea eneo hilo
alipanga kukutana na watoto wa Said Mwamwindi ili kuweka maridhiano
yatakayofanya watumie tukio lile la mauaji ya Dk Kleruu kuwaunganisha.
Kwa kupitia Katibu wa CCM Mkoa wa
Iringa, Hassan Mtenga, Eva alisema waliweza kukutana na kufanikisha azma yao
hiyo.
“Ile siku imefika na leo nimekutana na
mtoto wa kwanza wa Said Mwamwindi, Meya Amani Mwamwindi na kumaliza tofauti zao
zilizosababishwa na mauaji hayo,” alisema.
Eva alisema baada ya kukutana na
Mwamwindi na kuziweka kando tofauti za kihistoria baina ya familia zao
anajihisi ni sehemu ya maendeleo ya mkoa a Iringa.
Alisema kwa kupitia kampuni yao ya Power
Supply Cooperation wako tayari kuhakikisha kwamba miradi midogo ya uzalishaji
umeme inajengwa katika maeneo mbalimbali mkoani Iringa ili kufikisha nishati
hiyo kwa watu wengi zaidi.
Katika kikao chao hicho kilichomtoa
machozi pia Amani Mwamwindi, walikubaliana kukutana na familia zao na kutoa
taarifa ya maridhiano hayo.
Kwa upande wake Mwamwindi aliyekuwa
akiongea kwa hisia inayoashiria uchungu fulani alisema; “nimefurahishwa
kukutana na dada yangu huyu na kuondoa tofauti zetu za kihistoria.”
Mwamwindi alisema; “kabla na baada ya
tukio tukio hilo litokee miaka 43 iliyopita familia zetu zilikuwa hazijuani vizuri.
Na sisi tulikuwa watoto, leo tunakutana tukiwa watu wazima, ni jambo la
kushukuru mwenyezi Mungu.”
Alisema baada ya kikao chao hicho
watapanga siku nyingine ambayo kwa pamoja familia hizo mbili zitakutana zikiwa
na wawakilishi wengi zaidi.(STORI YA NYONGEZA NA PICHA KWA HISANI YA BLOG YA FRANK LEONARD)
Hongereni sana kwa hili kuna mengi ya kujifunza kutokana na hili, mtakuwa waelekezi wazuri kama si waalimu wa kufanya maridhiano kwa watu walio / wanaohasimiana
ReplyDeleteAmani na kusameheana ndo jambo zuli
ReplyDeleteAmani na kusameheana ndo jambo zuli
ReplyDeleteAmani na kusameheana ndo jambo zuli
ReplyDelete