Milio ya Bundi nyakati za usiku, ndege aina ya Kware wakiashiria kumalizika kwa kipindi cha kiangazi sanjari na sauti za Njiwa nyakati za asubuhi ilikuwa ni ishara tosha kwamba maeneo hayo ni ya vijijini ambayo sifa ya watu waishio maeneo hayo ni wale wanaokosa fursa ya kupata huduma muhimu za kijamii.
Moja ya huduma muhimu wazikosazo wananchi wa maeneo hayo ambao asilimia themanini ni wakulima na baadhi yao wakiwa ni wafugaji ni kupata fursa ya kuutumia mhimili usio rasmi wa dola (Mhimili wa Nne) Vyombo vya Habari, hali iliyoonesha kama vile wanahabari hao waliamua kukutana na wanavijiji hao kwa nia ya kufanya Tambiko la Kihabari.
Tambiko la Kihabari linatafsirika kutokana na ukweli kuwa wanahabari hao wa Mbeya wameamua kufungua ukurasa mpya wa kukutana na wadau wasio nasauti katika maeneo ya vijijini.
Asilimia kubwa ya wanahabari na vyombo vyao vimekuwa vikiripoti matukio ya mjini huku wananchi hao wa vijijini wakikosa fursa hiyo adhimu ambayo kimsingi ni haki yao ya Kikatiba ya Uhuru wa kutoa Habari na kupata Habari.
Ujio wa wanahabari katika maeneo ya vijijini ulileta shauku wananchi hao kukutana na washika kalamu hao ili angalau waweze kutoa madukuduku yao ambayo kwa takribani miaka hamsini tangu Uhuru hawajawahi kupata fursa hiyo.
Wanahabari walipata fursa ya kusafiri mwendo wa takribani kilomita 150 hadi katika kijiji cha Kalangali kijiji am ambacho kimenakshiwa na mazingira ya asili na mandhari yanayosadifiu uumbaji wa asili uliotunza mazingira halisi chini ya Taasisi ya Mazingira wilayani Chunya (KAEA).
Takribani wanahabari 40 ambao waliongozwa na Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari wa mkoa wa Mbeya Bw. Christopher Nyenyembe walifanya ziara katika kijiji hicho na kuzoea makazi ya maeneo hayo kwa muda wa siku tatu ambazo walizitumia katika kuzoea hali halisi ya maeneo hayo na kuishi kama wanakijiji ikiwa ni pamoja na kubadilishana mawazo na wenyeji wa maeneo hayo kwa kuvaa uhusika halisi wa kijijini.
Wanahabari ambao kwa asilimia kubwa hutafuta habari za mijini pekee walipata fursa ya kukutana na mtu mmoja mmoja wa maeneo hayo na kubaini dosari zenye changamoto kwa wanahabari kutokana na kukosekana kwa habari nyingi za vijijini katika vyombo vya habari nchini.Aidha fursa hii ya wanahabari iliwapa morari ya kuona umuhimu wa kipekee kutembelea mara kwa mara maeneo ya vijijini bila kusubiri ziara za viongozi wa kiserikali na kudandia magari ya viongozi hao ili kufika huko.
Tathmini ya mtu mmoja mmoja kutoka maeneo ya vijijini yameakisi sura halisi ya maisha yao huku nchi yetu ikikaribia kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru ifikapo Disemba 9 mwaka huu, ambapo suala la miundo mbinu, maji safi na salama, elimu, afya, masoko ya bidhaa wanazozalisha na pembejeo za kilimo.
Post a Comment
Post a Comment