Ads (728x90)





Wafuasi wa Chadema wakielekea katika uzinduzi wa kampeni ya uchaguzi wa jimbo la Arumeru Mashariki jana.
*Ni kwa sababu ya unyenyekevu wetu siyo woga
*Uzinduzi warushwa `live` kupitia Tv na mitandao

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kinaenda kushinda uchaguzi mdogo wa kiti cha ubunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki kwa sababu ya unyenyekevu wao na sio kwa woga na kimewataka polisi kutowapa upendeleo wa aina yoyote isipokuwa kusimamia haki.

“Tunakwenda kushinda Arumeru Mashariki kwa sababu ya unyenyekevu wetu na sio kwa woga kwa kuwa fujo sio jadi yetu bali sisi ni jasiri wa kutetea haki,” alisema hayo Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe ambaye pia ni mbunge wa Hai.

Alisema hayo katika siku ya uzinduzi wa kampeni ya uchaguzi wa jimbo hilo uliofanyika katika kiwanja cha Liganga kilichopo Usa River, wilayani Arumeru jana wakati akimnadi mgombea ubunge wa chama hicho Joshua Nasssari .
“Polisi simamieni haki, tendeni haki na leo ninatangaza hatupendi upendeleo wo wote wa polisi-simamieni haki na mkishindwa kusimamia haki Chadema isilaumiwe,” alisema.

Alisema uchaguzi wa Arumeru Mashariki sio wa jimbo wala wilaya bali ni uchaguzi wenye muono wa kitaifa na ndio sababu Watanzania wanaangalia Arumeru na dunia nzima inaangalia Arumeru.

Hata hivyo, alishangaa kuona magari mengi ya polisi zaidi ya 40 na magari ya washawasha manne na idadi kubwa ya askari polisi ambao wameletwa jimboni hapa katika kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi ingawa Rais Jakaya Kikwete hajatangaza kama kuna hali ya hatari.

“Rais Kikwete hajatutangazia kama kuna hali ya hatari Arumeru, lakini sasa hivi tunashuhudia kuona magari ya askari yanazidi kufurika hapa, kuna nini,” alihoji.

Akinukuu maneno ya Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, Mbowe alisema, “Serikali inayotumia nguvu ya kijeshi kujiweka madarakani inafundisha wapinzani wake matumizi ya nguvu ya kupinga utawala ule.”

Katika hatua nyingine, Mbowe alimrushia madongo Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa kuhusu matumizi makubwa ya fedha waliyotumia CCM katika chaguzi za kumpata mgombea wao.

Alidai uchaguzi wa kwanza wa kumtafuta mgombea wa CCM katika jimbo hilo walitumia Sh. milioni 100 na katika uchaguzi wa pili wa marudio chama hicho kilitumia Sh. milioni 120, wakati Sheria ya Uchaguzi inataka matumizi ya fedha kwa ajili hiyo yasizidi Sh. Milioni 80.

Alisema Chadema kilitumia Sh. milioni 6.2 tu kwa uchaguzi wa kumpata mgombea wao. Mbowe alisisitiza kuwa wanakwenda kwenye uchaguzi huo huku wakiwa wamesimama na Mungu wakati CCM ikiwa imesimama kwa fedha, mabomu na magari ya washawasha.

Alisema wenzetu wana fedha nyingi lakini kama ni za dhuluma wao hawajui isipokuwa kwa upande wao wanasimama na thumuni zao katika kuchangia kampeni za uchaguzi huo.

Alisema katika kila mikutano mingi watakayoifanya katika jimbo hilo watakuwa wakitoa sadaka ya kuendesha kampeni ya uchaguzi huo.

“Tunataka kurudisha chama hiki kwenye mikono ya watu maskini ili kulikomboa taifa hili bila kutegemea fedha za mafisadi na ruzuku za serikali,” alisema.

Alitangaza namba za simu ili watu waweze uchangia ukombozi wa Arumeru kwa sababu mchango huo utasaidia kuleta ukombozi wa taifa hili, Voda 0757755333, 0763744334, Airtel 0684425222, Tigo 0655783333.

“Sadaka hii itaendelea kwenye kila mkutano wa kampeni hizi na tutashinda bila kutegemea fedha za mafisadi,” alisema. Wakati huo huo maelfu ya wanachama na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wamehudhuria kwa mbwembwe uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo wa mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, hatua ambayo inadaiwa kuleta hofu ndani ya Chama Cha Mapinduzi, (CCM).

Mapema Katibu Mwenezi wa Chadema Wilaya ya Arusha, Hilary Mkonyi, alisema uzinduzi huo umeleta hofu kwa CCM. Uzinduzi wa CCM utafanyika Jumatatu wilayani hapa.

Mbwembwe zilianzia majira ya asubuhi pale misururu ya magari, pikipiki na baiskeli yakiwa yamepambwa na bendera za chama hicho yakitokea mjini Arusha na wilaya jirani za Mkoa wa Kilimanjaro na kufanya sehemu ya barabara eneo la Usa River kupitika kwa shida.

Helikopta ya chama hicho ilianza kuonekana ikiruka eneo la Usa River majira ya saa 6 mchana, huku mamia kwa maelfu ya wafuasi wa chama hicho wakianza kukusanyika katika kiwanja cha Liganga, kilichopo eneo hilo. Uzinduzi huo ulifanyika kuanzia 8:00 mchana hadi saa 12 jioni.

Majira ya saa 8:45 alasiri hivi helikopta hiyo kwa jina maarufu kama Chopa iliwasili ikiwa imembeba mwenyekiti wa taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe, pamoja na mgombea uchaguzi wa jimbo hilo, Joshua Nassari.

Mbwembwe ziliongezeka pale farasi maalum alipotumika kuupokea ugeni huo wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe na kuwakaribisha hadi kwenye jukwaa lililotengwa kwa ajili ya wageni hao.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na karibu wabunge wote wa chama hicho pamoja na madiwani kutoka Halmashauri za Manispaa ya Moshi, Arusha Mjini, Musoma Mjini,

halmashauri za wilaya za Karatu, Hai na Hanang, ulizinduliwa na Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Mbowe (Hai).

Kwa upande wa Wabunge wakitanguliwa na Rose Kamili, Mbunge Viti Maalum Wilaya ya Hanang’i alisema kuwa yeye ni kiboko ya Mary Nagu anayeleta ubinafsishaji, hivyo anaomba akina mama kutoa kura zao kwa mgombea wa Chadema.

Joyce Mukya Mbunge Viti maalum Arusha Mjini alisema kuwa, Nassari ni chumvi ambayo inahitajika kwa chama hicho ili kuleta chachu bungeni.

Peter Msigwa Mbunge wa Iringa Mjini alisema kuwa matatizo ya Arumeru Mashariki hayawezi kutatuliwa na CCM ambao wameleta matatizo yaliopo, hivyo suluhu ya maisha ya wana jimbo wachague Nassari.

Joseph Mbilinyi Mbunge wa Mbeya Mjini, naye aliwaomba wapiga kura kumchagua Nassari ili kuongeza idadi ya wabunge bungeni ili kupunguza kuzomewa na wabunge wa CCM pale wanapotoa hoja za msingi kwa Taifa.

Kwa Upande wa Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema, alisema kuwa tayari ushindi ni kwao kwa sababu wazee wamechukizwa na kitendo cha mgombea wa CCM, Siyoi Sumari kutoboa sikio na kuwaomba polisi

kulinda haki na amani bila kutumia mabavu kwa sababu hakuna silaha iliyowahi kushindwa na nguvu na amani.

Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Taifa (BAVICHA), John Heche alisema kuwa yeyote anayetaka kuishi maisha magumu zaidi katika maisha yake achague CCM ila kama wameshindwa waepukane na kumchagua mgombea wa CCM.

Aliwaomba polisi kutopendelea CCM na pale watakapothubutu kupendelea, vijana watafanya kazi yao, hivyo ili kuepukana na uvunjifu wa amani watoe nafasi kwa watu wote.

Mchungaji Natse Israel, Mbunge wa Karatu , ambaye pia ni Meneja Kampeni wa uchaguzi huo, alisema kuwa aliwaomba viongozi wote kuombea uchaguzi huo na kuombea Taifa, ambalo limegubikwa na migomo hasa mgomo wa madaktari unaosababishwa na kutotenda haki.

Alisema kuwa Taifa litambue Taifa lisilotenda haki matokeo yake ni aibu, ila aliomba wapiga kura wale CCM na kura zao wapeleke Chadema. Aidha alisema kuwa Jaji Daniel Lubuva alimwomba kutenda haki katika uchaguzi huo bila kupendelea chama tawala.

Naye Meneja Kampeni mwingine, Vicent Nyerere alisema kuwa, yeye ni mpole lakini si mnyonge ila anaamini hata polisi wamechoshwa na unyanyasaji wa CCM kwa kuwapeleka wastaafu wa jeshi hilo kuwa wakuu wa Wilaya na Mikoa.

“Hivyo naomba sana Polisi mtuachie ngoma hii tucheze wenyewe na CCM na sio kutuingilia” alisema Nyerere.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Kabwe alisema kuwa Chadema wanahitaji ongezeko la mbunge wa 49 Nassari ambaye atawasemea matatizo yao bungeni.

Alisema kuwa watumie fursa hiyo kumchagua kiongozi atakayewatatulia matatizo yao ya maji na ardhi ambalo ni sugu kwa Wilaya hiyo.

Kabwe alisema ongezeko la Mbunge huyo litawapa nguvu kubwa katika kutetea haki kwa wanyonge japo wapo wachache lakini sauti yao wanapaza kupitia bungeni na sauti hizo zinasikika kwa Taifa zima.

“Nawaomba msithubutu kuchagua CCM tumieni sanduku la kura na yule aliyepoteza shahada yake ya kura fikeni katika vituo vya kura waoneni mawakala na ombeni fomu namba 17 ili mpate haki yenu ya kupiga kura na kwa kutumia fomu hii itawaingiza choo cha kike CCM wanaonunua shahada,” alisema Kabwe.

Kabwe alisema kuwa kwa kutumia fomu namba 17 itawasaidia wapiga kura wote kupata haki zao za kupiga kura na wasitetereke. Pia alisema kuwa siku ya kupiga kura ni siku ya wajinga duniani, hivyo wasirubuniwe na matangazo yoyote watakayoelezwa kwamba mgombea wao amejitoa, wasiamini wapuuze na kwenda katika sanduku la kupiga kura.

Kwa upande wake Nassari alisema akiwa mbunge atatatua matatizo ya ardhi katika jimbo hilo ambayo kwa asilimia kubwa inamilikiwa na wawekezaji.

“Wakazi wengi wa jimbo hili hawana mashamba ya kulima au kujenga nyumba kwa sababu maeneo makubwa yanamilikiwa na wawekezaji…nikichaguliwa nitapigania ardhi hii kurudishwa kwa wazawa,” alisema.

Kuhusu kero ya maji alisema ataondoa tatizo hilo kumilikiwa na watu wachache wanaotumia maji kunyweshea farasi na viwanja vya gofu na kunywesha viboko huku maelfu ya wakazi wake wakikosa huduma hiyo muhimu. Kwa upande wa elimu alisema ataondoa kero kwa wazazi kuchangishwa fedha kila mwaka kwa ajili ya kununulia madawati ya shule.

Mapema Mkurugenzi wa Chadema wa taifa na masuala ya Bunge taifa, John Mrema, aliwataka wakazi wa Jimbo la Arumeru Mashariki, kuachana na basi la CCM na kupanda basi la Chadema kwa sababu basi hilo limeharibika.

“Nasema hivi kwa sababu huyu Vicent Nyerere (Musoma Vijijini Chadema), alikuwa ndani ya CCM na ameishi Ikulu, lakini alipoona tu basi la CCM limeharibika na hakuwa na mzigo ndani ya basi hilo, alishuka na kupanda basi la Chadema, sasa nyie wana Arumeru kwa nini mkatae kushuka ndani ya basi hilo wakati hakuna mnachonufaika nacho,” alisema Marema.

Aidha aliwataka wananchi wa jimbo hilo, kumtafuta kwa simu yake ya kiganjani pale watakaposhuhudia ununuzi wa shahada na utoaji wa rushwa kwa lengo la kuvuruga kura aweze kutuma kikosi cha kushughulikia wahusika katika kata na vijiji vyote.

Mrema alisema kwa mara ya kwanza chama chao kimeamua kuonyesha uzinduzi huo moja kwa moja kupitia kituo cha televisheni cha Star TV ili wananchi walioko maeneo mengine waone na kushuhudia.

Pia uzindizi huo umerushwa moja kwa moja kupitia kituo cha Radio cha Sunrise Fm cha jijini Arusha, na kupitia mtandao wa intaneti wa www.jamiiforums.com na hivyo kuwawezesha watu hata walio nje ya nchi kuona kinachoendelea katika viwanja vya Usa River ambako mkutano wa uzinduzi ulikuwa unafanyika…CHANZO GLOBAL PUBLISHERS.

Post a Comment

Post a Comment