UMEIBUKA uvumi mkubwa katika miji ya Tunduma na Vwawa
wilayani Mbozi ambapo imedaiwa kuwa mwanamke mmoja ambaye ni mke wa mtu mkazi
wa maeneo ya Isangu mjini Vwawa wilayani humo amekutwa akiwa amenasa wakati
akifanya mapenzi na mwanamume wa nje.
Mwandishi wa habari hizi alifika mjini humo na kukuta
makundi makubwa ya wananchi wakiwa wanaelekea katika hospitali ya Wilaya ya
mjini Vwawa huku wakisikika wakisimulia mkasa huo ambao umedaiwa kuwakumba mke
wa mtu na mwanaume mkazi wa mjini Tunduma.
Wananchi hao ambao wengi wao walikuwa ni akina mama
walisikika wakieleza kuwa mwanamke huyo ni mfanyabiashara wa Maparachichi mkazi
wa kijiji cha Isangu kilichopo pembeni kidogo ya mji wa Vwawa wilayani Mbozi
ambaye hufanya biashara zake kati ya Tunduma na Vwawa.
Ilielezwa kuwa wapenzi hao mke na mwanaume huyo (majina yao
hayakufahamika) walikuwa wakionywa mara kadhaa kutoendelea na maapenzi yasiyo
halali ambapo mume wa mke huyo inadaiwa alibaini mahusiano ya wapenzi hao kwa
muda mrefu.
Ilidaiwa kuwa alipokuwa akimuonya mumewe alichukua shoka
tupu na kulikutanisha na mpini huku akimueleza kuwa kama kweli alikuwa
hashiriki mapenzi nje ya ndoa uthitisho utakuwa ni shoka na mpini huo ambao
aliuhifadhi chumbani kwao wanakolala chini ya uvungu wa kitanda.
Mashuhuda hao waliendelea kudai kuwa siku ya tukio mke huyo
aliondoka kama kawaida kuelekea katika biashara zake za maparachichi huko mjini
Tunduma mpakani wa Tanzania na Zambia ambako alikutana na Hawara yake.
Hata hivyo makundi hayo ya watu walishindwa kubainisha
ukweli juu ya tukio hilo kwa kueleza majina ya wahusika huku Daktari wa wilaya
ya Mbozi Dkt.Charles Mkombachepa alikanusha kuwepo kwa watu hao katika
hospitali hiyo na kueleza kuwa ni uvumi uliovumishwa tangu asubuhi.
Dkt. Mkombachepa alisema kuwa makundi ya watu yamekuwa yakimiminika hospitalini
hapo kwa siku nzima ya juzi kuanzia asubuhi hadi jioni wakiulizia tukio hilo
lisilokuwa na ukweli.
Aidha baada ya kubaini kuwa hakuna tukio hilo uvumi huo ukaendelea
kuenea kuwa watu hao wamehamishiwa katika hospitali ya Rufaa ya Mbeya kutokana
na hospitali ya Vwawa kushindwa kuwatenganisha hali ambayo pia ilikanushwa na
wauguzi na wafanyakazi wa hospitali ya Rufaa Mbeya.
Uvumi wa aina hiyo umekuwa ukienea mara kadhaa katika maeneo
mbalimbali nchini ambapo mwanzoni mwa miaka ya themanini Buguruni Jijini Dar es
salaam uliibuka uvumi wa mwanamke aliyemwekea dawa mumewe na kugeuka Nyoka
uvumi ambao hadi sasa uko vichwani mwa watu.
Kadhalika mwaka 2003 Jijini Mbeya uliibuka uvumi wa
kukamatwa kwa mganga mmoja aliyekuwa akihusika na kuwakata matiti wanawake
jambo ambalo pia halikuthibitishwa.
Post a Comment
Post a Comment