Wananchi wa Kata ya Ijombe - Mbeya
Vijijini watoa kilio chao kuhusu huduma duni za kijamii kutokana na uongozi
mbovu
Mtandao wa Jinsia
Tanzania (TGNP), ni shirika lisilo la kiserikali linalopigania usawa wa
kijinsia, haki za binadamu na ukombozi wa wanawake kimapinduzi. TGNP kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali inapambana na mifumo kandamizi ikiwemo mfumo
wa kibepari, kibeberu, utandawazi na mfumo dume. Kuanzia mwaka 2008, TGNP
imeelekeza nguvu zaidi katika ujenzi wa TAPO (vuguvugu) ngazi za kijamii, kama
sehemu ya kutambua na kuchambua masuala ya vipaumbele kwa wanawake na wanaume
walioko pembezoni.
Kuanzia tarehe 21
hadi 31 Mei 2012, kikundi cha waraghbishi kutoka TGNP wamefanya mchakato
shirikishi wa uraghbishi katika vijiji vya Nsongwi Juu, Ifiga, Iwalanje,
Nsongwi Mantanji na Ntangano Ijombe,Kata ya Ijombe, Wilaya ya Mbeya Vijijini
mkoani Mbeya.
Wakazi wa Kata ya
Ijombe wameelezea kero mbalimbali ikiwemo ya ukosefu wa masoko kwa mazao
wanayolima, ambapo madalali hununua mazao kwa bei ndogo na kwenda kuuza kwa
wafanyabiashara wakubwa bila wao kupata faida. Sambamba na hilo, ushuru pia ni
kero kubwa.
Kuna ushuru wa aina
mbili ukiwemo ushuru wa mazao shambani na ushuru wa mazao yakifika sokoni,
ambao wanalipa bila stakabadhi kutolewa. Kwa ushuru wa shambani kila gunia ni
shilingi 1000/- na ushuru wa mazao sokoni ni shilingi 200/- kwa mchuuzi. Wakati
huo huo, wakazi wa Ijombe wamedai katika Kata yao hakuna utawala bora kwani
baadhi ya viongozi hawaweki wazi taarifa za mapato na matumizi na huu ni uvunjaji
wa sheria.
Vilevile, wanawake
wamedai kuwa wanakabialiana na ukatili wa kijinsia toka kwa wanaume ikiwa ni
pamoja na kuuza mazao kinyemela, kutokuhudumia familia, kutolipa ada za shule
kwa watoto, wanawake kupigwa kutokana na ulevi uliopindukia wa waume zao.
Huu umekuwa ni mzigo
mkubwa kwa wanawake wa Ijombe na wameuomba uongozi husika hasa katika ngazi za
vitongoji, vijiji na Kata waweze kufuatia kero hizi na kuweka sheria
zitakazowabana wanaume kutokana na vitendo vyao. Pia wakazi wa Ijombe wameomba uongozi
kufuatilia na kudhibiti muda wa kuuza pombe. Wanapendekeza vilabu vifunguliwe
kwa muda maalum uliopangwa. Kisheria vilabu vinapaswa kufunguliwa saa kumi
jioni na kufungwa saa tatu usiku, na sio kufunguliwa saa moja asubuhi kama
ilivyo kwa sasa.
Kero nyingine
waliyotoa ni mimba za utotoni kutokana na ukosefu wa mabweni kwa wasichana
wanaosoma katika Shule ya Sekondari ya Kata ya Iwalanje.
Shule ya Iwalanje
imekuwa mbali sana na makazi ya walio wengi. Wanafunzi wanatembea umbali wa
kati ya kilometa 4 hadi 8 kutoka vijiji vinavyotumia shule hiyo.
Tatizo hili la
umbali limepelekea baadhi ya wanafunzi kupanga vyumba vinavyojulikana kwa jina
maalum la ‘GHETO’.
Wakazi wa Kata hiyo
wamedai kuwa kutokana na kuishi kwenye magheto kwa muda mrefu kumepelekea
wasichana wengi kutokufanya vizuri katika masomo yao.
Wasichana walio
wengi, wamegeuka kuwa wapishi na wanasaka maji, kuni kwa ajili ya kujipikia
chakula.
Kwa maana hiyo
wasichana wamekuwa wakitumia muda wao mwingi zaidi kufanya kazi zilizo nje ya
masomo tofauti na watoto wa kiume ambao muda mwingi wamekuwa wakijisomea.
Zaidi ya hayo wakazi
wa Ijombe wamekiri kuwa wasichana wengi wamepata mimba za utotoni kwa kukosa
ulinzi kwani baadhi ya magheto wanaishi watoto wa kike na wakiume.
Pia kuna hatari kubwa
ya kuongezeka kwa maambukiza ya magonjwa hatarishi kama vile Ukimwi.
Vilevile, wakazi wa
Kata ya Ijombe wamedai kuwa michango ya shule imekithiri. Kwa mfano michango
inayotolewa ni shilingi 10,000/- kwa kila kichwa kwenye kaya. Kwa wale ambao
wanaoshindwa kutoa mchango huo, kwa ajili ya maisha kuwa magumu hukamatwa na
kupelekwa mahakamani; na ili waachiliwe huru wakazi hao hutakiwa kutoa shilingi
67,000/=.
Pia wakazi wa Ijombe
hutoa shilingi elfu ishirikini (20,000/=) kwa mwaka kwa wanafunzi wanaoishi nyumbani
na kwenye magheto. Michango yote kwa mwaka kwa mtoto anayeanza sekondari ni
zaidi ya shilingi laki tatu na elfu hamsini (350,000/-), zikijumuisha fedha za
madawati, vitambulisho, bima za afya, tahadhari, sare za shule,madaftari na
rimu za karatasi. Michango hii inakuwa ni kikwazo kwa wazazi ambao kipato chao
ni kidogo.
Kwa wanafunzi
wanaoishi mashuleni wanalipa laki nne na nusu (450,000/-) tu kwa mwaka.
Vilevile, Kata ya
Ijombe hasa kijiji cha Iwalanje kuna tatizo la maji kwa muda mrefu . Wakazi wa Iwalanje
wamedai kuwa kijiji chao kimekuwa kikitoa mchango kwa ajili ya kupata maji kwa
takribani miaka kumi na nne iliyopita bila mafanikio.
Wanawake ndio
waathirika wakubwa wa tatizo hili. Wanawake wa eneo hili wamesema wamekuwa
wakiamka saa kumi alfajiri kwenda kusaka maji na kurudi saa tatu asubuhi,
wakati huo huo wanawake wanapata kipigo toka kwa waume zao kutokana na
kuchelewa kurudi.
Wanawake wa Ijombe
wameiomba serikali kufuatilia kwa karibu tatizo hili kwani linawakosesha mapato
kutokana na kutoweza kushiriki katika kazi za uzalishaji.
Mwisho wakazi wa
Ijombe wamekiri kuwa kero zote zilizokithiri katika Kata yao, zinatokana na
uongozi mbovu, hasa viongozi kutokufuatilia kwa karibu masuala yanayowagusa
wananchi wao na kuwepo kwa ubinafsi zaidi, kuchanganya masuala ya kisiasa na
masuala ya kimaendeleo.
Pia viongozi
wametakiwa kujua wajibu wao kila mmoja katika nafasi yake
Wakazi hao wameomba
viongozi wawe na mawasiliano na wananchi kwa kujadili kero zinazowakabili na
kutafuta ufumbuzi wa matatizo yao kwa pamoja.
Imetolewa na
Waraghbishi, Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP)
Kwa niaba ya
Mkurugenzi Mtendaji, TGNP
Post a Comment
Post a Comment