MTOTO ALIYETUMBUKIZWA CHOONI AKIPEWA HUDUMA KATIKA HOSPITALI YA WILAYA VWAWA MBOZI |
WAKAZI WA VWAWA WILAYANI MBOZI WAKIWA NJE YA HOSPITALI YA VWAWA MBOZI KUSHUHUDIA MTOTO ALIYEOKOLEWA KUTOKAA SHIMO LA CHOO |
CHOO AMBACHO MTOTO HUYO ALIDUMBUKIZWA |
Na,Rashid Mkwinda, Mbozi
WAKATI akina
mama wengine wakihaha kwa waganga kutafuta dawa kwa ajili ya kupata watoto,
wengina wanaichezea bahati yao kwa kufanya matukio ya unyama kama ilivyotokea
kwa msichana mmoja aliyetambulika kwa jina la Esther kuamua kumtupa mtoto wake wa
kiume mwenye umri wa miezi mitatu katika shimo la choo kinachotumika kwa nia ya
kumuua.
Tukio hilo
la kinyama limetokea mwishoni mwa wiki katika kitongoji cha Ilolo kilichopo
mjini Vwawa wilayani Mbozi ambapo msichana huyo alivaa roho ya unyama na kuamua
kutekeleza ukatili huo bila hata roho ya huruma huku sauti ya kitoto chake
kichanga ikilia kwa kubembeleza ili kionewe huruma ya kuuliwa bila hatia.
Kama vile
haitoshi msichana huyo anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 15 aliziba masikio
yake kwa pamba na kuamua kukitumbukiza kitoto hicho ndani ya shimo na kutokomea
kusikojulikana.
Sauti za
kilio za mtoto yule zilihanikiza hewani bila kupatiwa msaada wowote ambapo
hatimaye kilio chake kikasikika hadi kwa wasamaria wema ambao ndio watumiaji wa
choo hicho.
Mmoja wa
wasamaria hao aliyejitambulisha kwa jina la Mbwagile Kitaja mkazi wa Ilolo
mjini vwawa alisema kuwa tukio hilo limetokea wakati wakiwa msibani majira ya
saa 8 mchana ambapo walikuja wajukuu
zake kumueleza kuwa ndani ya choo cha jirani kuna sauti ya mtoto analia.
Alisema
majirani walifika katika eneo hilo la tukio na kuamua kukivunja choo hicho ili
kukiokoa kitoto hicho ambacho kwa muda huo mwili wake wote ulianza kuzingirwa
na funza wa chooni.
Walibomoa
choo hicho kwa tahadhari wakihofia kumdhuru mtoto ambapo mmiliki wa choo hicho
aliyejitambulisha kwa jina la Orasmo Nyingi (Pompi)alitoa taarifa kwa
Mwenyekiti wa mtaa huo Ephraimu Mwakiteba alisema kuwa walifanya jitihada za
kumtoa kwa kutumbukiza ngazi mbili ndani ya shimo na kisha kumtoa na kumsafisha
uchafu.
Alisema kuwa
walimfikisha mtoto huyo katika hospitali ya wilaya iliyopo Vwawa wilayani Mbozi
ambapo alipewa huduma ya kwanza ambapo katika baadhi ya sehemu zake za mwili
alianza kuunguzwa na joto la uchafu wa chooni lakini hata hivyo walifanikiwa
kumpa matibabu na kisha kuruhusiwa ambapo mama Kitaja alichukua dhamana ya
kumlea.
Aidha katika
hatua nyingine babu wa mtoto huyo ambaye alijitambulisha kuwa ni Ofisa
Maendeleo ya jamii wa wilaya ya Mbozi Philimon Adrat alisema kuwa binti yake
ndiye mwenye mtoto huyo na kwamba anashindwa kuelewa sababu ya kumtumbukiza
chooni mwanaye kwa kuwa ni yeye mwenyewe aliyebeba ujauzito bila kushinikizwa
na mtu.
Alisema kuwa
mara baada ya kupata ujauzito alimtunza na kulea ujauzito wakehadi
alipojifungua mwezi Julai ambapo mtoto huyo alikuw akiendelea vyema.
Alifafanua
kuwa kabla ya kumtumbukiza mtoto huyo chooni binti yake alifukuzwa na mama yake
na kuambiwa aje kwa baba yake ndipo alipofika nyumbani na kukaa siku mbili na
kuelezea mkasa wa kutimuliwa na mama yake ambapo hata hivyo siku ya tukio
hakujua kama mwanaye anaweza kuamua kufanya unyama wa aina hiyo.
Akizungumzia
hatima ya tukio hilo Mwenyekiti wa serikali ya kitongoji cha Lami mtaa wa Ilolo ambako ndiko lilikotokea
tukio hilo Bw.Mwakiteba alisema kuwa mara baada ya kutokea kwa tukio hilo
walipeleka taarifa kituo cha polisi ambapo hata hivyo binti huyo hajulikani
aliko hadi sasa.
Babu wa
mtoto huyo Bw. Adrati alisema kuwa hajui aliko binti yake na kwamba wanafanya
utaratibu wa kumchukua mtoto huyo kutoka kwa wasamaria wema ambao wanamtunza
mara baada ya kutokea tukio hilo.
Post a Comment