SAKATA la walimu
wa shule ya sekndari Forest ya Jijini Mbeya kudaiwa kufungua jela ya mateso kwa
wanafunzi limechukua sura mpya baada ya kundi la wanafunzi wa shule hiyo
kufanya maandamano kwa nia ya kumshinikiza Mkuu wa shule hiyo kujiuzulu.
Kundi hilo la
wanafunzi lilikuwa na mabango ya kushinikiza kuondolewa wa Mkuu wa shule hiyo
Secilia Kakela na walimu wawili Faustin Robert na Josephat Mwasote ambao wote
wawili walikamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU kwa
tuhuma za kukusanya fedha kwa wanafunzi na kutoa adhabu za kijeshi.
Hata hivyo
maandamano ya wanafunzi hao yalikatishwa na askari wa kutuliza ghasia FFU kwa
kukamatwa kwa mabango hayo na kuwazuia kuandamana kwa kuwa maandamano hayo
hayakuwa na kibali cha Polisi.
Wakizungumza
shuleni hapo baadhi ya wanafunzi walidai kuwa walidhamiria kuandamana hadi kwa
Ofisa Elimu wa Mkoa ili kushinikiza kutimuliwa kwa walimu hao kutokana na
kujihusisha na adhabu za kijeshi na kwamba wanashangazwa na kitendo cha kurejea
kwa walimu hao mashuleni pamoja na kukamatwa na TAKUKURU.
‘’Tunashangazwa
walimu hawa kurejea shuleni,usalama wetu uko wapi, sisi tulikuwa mashahidi wa
TAKUKURU walikamatwa na vidhibiti,hatuamini kama kiwango chao cha ufundishaji
kitaturidhisha,’’alisema mmoja wa wanafunzi wa kidato cha tatu.
‘’Tangu waachiwe
tumekuwa hatuna amani hapa shuleni, wanajigamba kwamba hatuwawezi, tunashindwa kusoma kwa amani,’’alisema
mwanafunzi mwingine aliyejitambulisha kuwa ni wa kidato cha pili.
Aidha katika
madai yao wanafunzi hao walisema kuwa hawaamini kama saikolojia ya walimu na
wanafunzi itaimarisha taaluma shuleni hapo hivyo walimuomba Ofisa elimu wa Mkoa
wa Mbeya kuwaondoa walimu hao ili kujenga nidhamu ya kitaaluma.
Wanafunzi
walipanga kuandamana kuelekea kwenye Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Mbeya ambako
ndiko ilipo Ofisi ya Ofisa elimu lakini kabla hawajaanza kutekeleza maandamano yao askari polisi wapatao saba waliokuwa
katika gari aina ya Landcruiser waliwasili shuleni hapo na kuwanyang’anya
mabango wanafunzi hali ambayo iliibua taharuki na kuwajengea hofi wanafunzi.
Hata hivyo Ofisa
elimu wa Mkoa wa Mbeya Bw. Juma Kaponda alifika shuleni hapo kusikiliza kilio chao
na kuwataka wawe watulivu kwa kuwa matatizo ya walimu wao yanafanyiwa uchunguzi
na TAKUKURU.
Alisema kuwa
kulingana na taratibu yeye kama Ofisa Elimu haruhusiwi kuingilia mamlaka ya
TAKUKURU kwa kuwa upelelezi dhidi ya makosa ya walimu hao yako kisheria hivyo
anasubiri sheria ichukue mkondo wake huku walimu hao wakiendelea kufundisha
kulingana na mkataba wa ajira yao.
Kwa upande
wake Kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Mbeya Daniel
Mtuka alisema kuwa walimu waliokamatwa kwa tuhuma za kutoa adhabu za kijeshi
kwa wanafunzi kushinikiza kupewa rushwa waliachiwa kwa dhamana huku upelelezi
dhidi ya makosa yao ukiendelea kwa ajili ya kuwafikisha mahakamani.
‘’Watuhumiwa
hawa wameachiwa kwa dhamana, upelelezi utakapokamilika watafikishwa mahakamani
kujibu tuhuma za rushwa’’alisema Bw. Mtuka.
Kwa upande wao
baadhi ya wazazi waliozungumza na gazeti hili walisema kuwa wazazi wamedhamiria
kufanya mkutano shuleni hapo siku ya Jumamosi kwa nia ya kuelezea uhalali wa
walimu hao kuendelea kufundisha hapo huku wakiwa na tuhuma zinazowakabili.
‘’Kiuhalisi
walimu hao walitakiwa wasiwepo hapo shuleni,kwa vyovyote vile ufundishaji wao
utashuka na wanafunzi watajenga hofu ya kupokea masomo kwa walimu hao, wazazi
tutakuwa na mkutano siku ya Jumamosi’’alisema Bw. Moses Mwasubila mmoja wa
wazazi wa wanafunzi shuleni hapo.
Awali walimu wa
shule hiyo walituhumiwa kuanzisha jela ya mateso kwa wanafunzi hao
waliyoipachika jina la Guantanamo ambako wanafunzi huadhibiwa kwa adhabu
iliyopachikwa jina la ‘’Kuibeba Dunia’’ kichwa chini makalio juu na kwamba
walimu hao walikuwa wakiwatoza wanafunzi sh. 500 kwa kila mwanafunzi ili
kujiokoa na adhabu hiyo.
Maofisa wa TAKUKURU walifika shuleni
hapo na kuwakamata walimu wawili ambao walikutwa na orodha ya majina ya
wanafunzi huku wakiwa na jumla ya sh. 68,000 ambazo walikusanya kwa wanafunzi
hao.
|
Post a Comment
Post a Comment