KAHAMA:
AMA
hakika duniani kuna mambo! Na lisemwalo lipo kama halipo basi laja. Ni
jambo ambalo ni vigumu kuliamini lakini ukweli wa mambo ni kwamba limetokea
mjini Kahama, Mkoa wa Shinyanga, kiasi cha kuleta mtafaruku kwa jamii.
Ni baada ya vikongwe viwili vinavyosadikiwa ni vichawi kunusurika kuuawa
na wananchi wenye hasira kali kufuatia kudondoka kutoka angani.
Tukio hili la aina yake ambalo mbali na kustaajabisha limeleta hofu kwa
baadhi ya wakazi mjini Kahama, lilitokea usiku wa kuamkia Aprili 3 mwaka huu
katikati ya Kata za Majengo na Mhongolo zilizo katika Halmashauri ya Mji wa
Kahama.
Vikongwe hivyo vilikutwa vikiwa taabani huku vikiwa vimetapakaa kinyesi.
Vikongwe hivyo, Mwajuma Samaka Mponi (70) mkazi wa kijiji cha Nduku katika Kata
ya Kinaga na Shija Nkwabi (80) mkazi wa kijiji cha Nyashimbi pia mkazi wa Kata
ya Mhongolo katika Halmashauri ya Mji wa Kahama, vilikumbwa na dhoruba la
kudondoka baada ya kugongana na wanga wenzao wengine watatu waliokuwa katika
shughuli zao angani.
Afisa Mtendaji wa Kata ya Mhongolo, Emmanuel Kalolo, anasimulia
kuwa vikongwe hivyo vilionekana vikiwa hoi havijitambui vikiwa vimelala ambapo
kimoja kilikuwa eneo la Kindi’s Bar katika barabara ya kwenda Mhongolo huku
mwingine akiwa mtaa wa Bariadi karibu na Café Latino.
Kalolo alisema kuwa Waendesha bodaboda (pikipiki) walianza kumshuhudia kikongwe
Mwajuma Mponi tangu alfajiri lakini hawakumjali kwa kudhani kuwa huenda ni
mlevi ama mwendawazimu. Hali iliendelea hivyo hadi alipotokea mtu mmoja
ambaye aliingiwa na mashaka baada ya kumwona akiwa uchi wa mnyama tena
akiwa ametapakaa kinyesi.
Msamaria huyo, Kulwa Samson, kwa jina maarufu’ KR’ ambaye ni Meneja
wa Café Latino, baada ya kumuona bibi huyo aliamua kumpatia msaada kwa
kumuombea nguo katika nyumba za jirani.
Samson alisema alibaini hilo wakati kienda Mhongolo kufuatilia
kreti za bia. Baada ya kumsaidia, bibi huyo alimweleza kuwa kuna
mwenzake mtaa wa pili. Walipomfuatilia walimkuta akiwa amezingirwa na
watu waliokuwa wamemshangaa.
Baada pia ya kumsitiri alimchukua hadi kwa mwenzake na kuwafanyia mpango wa
chakula.
Baada ya huduma hiyo aliwakabidhi kwa Kamanda wa Wanawake Kata ya
Majengo, Kuluthum Bujiku, ambapo walianza kuwasaili chanzo cha kuwa katika
madhia hayo. Nao bila kupepesa macho, vikongwe hivyo vilidai vilidondoka
vikiwa katika shughuli zao za kawaida za kila siku usiku.
Mashuhuda hao walisema kuwa vikongwe hivyo vilidai vilikuwa vikitoka
katika makao yao ya shughuli zao huko Nduku wakiwa na wenzao watano wakielekea
Dodoma kuhitimisha kilele cha sherehe za Pasaka. Walisema wakiwa angani
walipata ajali ya kugongana na wenzao waliokuwa wakitoka eneo jingine hivyo
wakajikuta wamedondoka ardhini.
Vikongwe hao vilieleza kuwa safari yao ya Dodoma ilikuwa ya kwenda na kurudi
usiku huohuo mara baada ya kukamilika kwa tafrija yao hiyo ya Pasaka. Kwa
bahati mbaya, walidai, wakiwa njiani kuelekea Dodoma walikumbwa na
dhoruba hiyo na kudai baada ya kugongwa “pikipiki” yao iliishiwa mafuta.
Walisema kuwa wenzao watatu ambao waliishawahi kukumbwa na dhoruba hiyo mara
nyingi, walitoweka katika mazingira ya kutatanisha na kuwaacha wao
wakitapatapa. Waliongeza kwamba shughuli hiyo ya usangoma
imewafikisha maeneo mbalimbali hapa nchini na walikuwa hawajawahi
kudondoka.
Baada ya maelezo hayo ambayo waliyatoa huku kukiwa na umati wa watu ambao
walitaharuki na kutaka kuwashushia kipigo, sangoma hao walinusurika baada ya
Samson kuwa tayari amewapigia simu polisi ambao hawakufanya ajizi kufika eneo
la tukio na kuwakuta watu wenye hasira wakiwa wamejipanga kuwatoa uhai vikongwe
hao.
Watu hao walipandishwa katika karandinga huku kikongwe Mwajuma akigoma
kuachia kifuko cheusi alichokuwa amekishika mkono wa kulia ambacho alidai ni
hazina yao muhimu. Vilevile, gari la oolisi lilipata wakati mgumu
kuondoka hapo kwani lilionekana kama vile gurudumu zake zinataka kuzama ardhini
bila sababu.
Polisi wilayani Kahama imethibitisha kuwa inawashikilia watu hao.
|
Post a Comment
Post a Comment