Na, Rashid
Mkwinda, Tunduma
WANAFUNZI 129
wanaosoma katika shule ya msingi ya Uhuru iliyopo Tunduma wilayani
Momba mkoani Mbeya wamelazimika kuketi sakafuni kutokana na shule hiyo kuwa na
madawati matano yanayokidhi mahitaji ya wanafunzi 20 kati ya wanafunzi 149 wa
shule hiyo.
Shule hiyo
yenye jumla ya madarasa matatu na walimu watatu ambayo ilianzishwa kutokana na
msongamano wa wanafun zi katika shule za msingi za Mkombozi,Umoja, Migombani na
Sogea ambazo zilifurika wanafunzi kiasi cha kuwa na uwiano wa mkondo mmoja
wanafunzi 100.
Waandishi wa
habari walitembelea shule hiyo mwishoni mwa wiki na kukuta vyumba vitatu
ambavyo ndani yake kumepangwa matofari ambayo kwa mujibu wa mwalimu wa darasa
la pili Bi. Adela Mtweve ni kwamba matofari hayo yanatumiwa na wanafunzi kama
madawati.
Bi. Mtweve
alisema kuwa darasa moja lenye wanafunzi 50 lina madawati matatu ambapo
wanafunzi wanaobaki wanakalia matofari na kusababisha kushindwa kuandika
vizuri.
‘’Hapa ndipo
wanapoketi wanafunzi na kuandika,anaweka daftari lake juu ya tofari na yeye
anakalia tofari jingine,’’alisema Mwalimu Mtweve huku akionesha namna ambavyo
wanafunzi hao wanaketi.
Akizungumzia
tatizo hilo Mwalimu mkuu wa shule hiyo Bi. Juni Mwandambo alisema kuwa shule
hiyo ina upungufu wa madawati, walimu na nyumba za walimu hali ambayo
inasababisha kudorora kwa taaluma.
Alisema kuwa
baadhi ya wazazi wanaotembelea shuleni hapo hulazimika kuwahamisha watoto wao
na kuwapeleka katika shule nyingine na kwamba wakati shule hiyo inaanzishwa
ilikuwa na jumla ya wanafunzi 175 ambapo
kwa sasa wamebaki wanafunzi 149.
‘’Takribani
wanafunzi 30 wamehamishwa na wazazi wao baada ya kuona mazingira yaliyopo,
wanafunzi wanaketi kwenye vumbi, ni hatari kwa afya ya wanafunzi,’’alisema
Mwalimu Mwandambo.
Naye
Mwenyekiti wa Mtaa wa Majengo mapya ambako shule hiyo ipo Bw.Lugano Mwakiboge
alisema kuwa, baada ya kuona kuna msingamano wa wanafunzi katika shule zilizopo
katikati ya mji wa Tunduma wananchi walihamasishwa kujenga shule hiyo.
Alisema kuwa
wazazi walichangia ujenzi na halmashauri ya mji wa Tunduma ilichangia mabati
ambapo kwa sasa wanatafuta ufadhili kutoka taasisi mbalimbali ili kusaidia
ujenzi wa shule hiyo.
Bw.Mwakiboge
alisema kuwa Benki ya Posta Tawi la Tunduma ilitoa jumla ya mifuko 100 ya
saruji yenye thamani ya zaidi y ash. milioni 1.7 ambayo itasaidia kusakafia
madarasa ya shule hiyo ambapo kwa sasa wanafunzi wanaketi kwenye vumbi.
Akizungumzia
msaada huo wa saruji kwa shule ya msingi Uhuru, Mhasibu wa Benki hiyo Bw. Felix
Mapunda ambaye alikabidhi msaada huo kwa niaba ya mkurugenzi mkuu wa benki ya
Posta nchini Bw.Sabasaba Moshingi alisema kuwa msaada huo ni sehemu ya huduma
za kibenki.
Alisema kuwa
faida itokanayo na huduma za kibenki za inarejeshwa kwenye maendeleo ya
wananchi ikiwemo ambazo ni huduma za kijamii kama vile, elimu, afya na maji.
|
Post a Comment