Mkulima mwenye shamba bora la Chai nchini Bi. Josephine Njuwensi akiwa shambani kwake katika kijiji cha Bujesi wilayani Rungwe |
Mtendaji Mkuu wa Wakulima wadogo wa Chai Lebby Gabriel akifafanua jambo katika shamba la chai. |
Baadhi ya wakulima wa Chai wilayani Rungwe wakiwa katika kikao cha kamati ya chai kujadili mustakabali wa zao la chai. |
Umaarufu wa wilaya ya Rungwe
umeongeza ushindani katika Nyanja za kilimo husuani katika zao la Chai huku
wakulima wakihitaji msaada zaidi kutoka serikalini ili upatikane uwezeshaji wa
uwekezaji wenye tija kwa nia ya kuongeza pato la uchumi kwa mkulima mmoja
mmoja, vikundi, wilaya, mkoa na hata Taifa.
Umuhimu huu huongezeka zaidi pale
serikali inapomudu kuuza mazao yake nje ya nchi na kujiingizia fedha za kigeni
kutokana na mazao ya kibiashara yanayozalishwa nchini.
Hali ya hewa rafiki ya wilaya hiyo
inatoa fursa kuvutia wakulima wa mazao ya chakula na biashara na kuimarisha
uchumi wa wakazi wake wanaotegemea kujiinua kiuchumi na kuondokana na utegemezi
ambao unatishia umaskini wa kipato.
Fursa adimu na adhimu ya ardhi
wilayani humo inatoa tija kwa wakazi wake na kufika mahala kuwatoa ‘udenda’
baadhi ya wawekezaji wenye uchu na matajiri wageni kuitamani ardhi hiyo na
ikiwezekana kuihodhi na hata kupokonya kutokana na kuwa na rutuba
inayomea mazao lukuki yenye manufaa kwa wakulima.
Wilaya ya Rungwe ni moja kati ya
wilaya zenye mashamba makubwa ya chai ambapo asilimia kubwa ya wakazi wake
aidha wamelima chai ama familia zao zinategemea ama zimenufaika na zao hilo
kongwe wilayani humo.
Chai ni moja ya mazao makubwa ya
kibiashara wilayani humo ambayo yanachangia uchumi wa wilaya ijapokuwa kuna
changamoto lukuki zinazowakumba wakulima wa zao hilo kutokana na uhitaji wa
matajiri wakubwa kumiliki zao hilo na kuwafanya wakulima wa zao hilo kuwa kama
manamba katika mashamba yao.
Hali hiyo imewafanya wakulima
watafakari namna ya kujikwamua na ukiritimba wa wanunuzi na walanguzi wa chai
ambao huwaacha wakulima wakiendelea kulima bila kuwezeshwa kwa mahitaji muhimu
ya uzalishaji bora wa zao hilo kama vile wataalamu,pembejeo za kilimo na mbolea
ya ruzuku.
Kimsingi kulingana na sheria na
kanuni za tasnia ya zao la chai husimamiwa na Bodi chini ya sheria ya
chai Na. 3 ya mwaka 1997 sura ya 275 ya sheria ya Tanzania iliyofanyiwa
marekebisho mwaka 2009 pamoja na kanuni zake za mwaka 2010 kwa muji wa tangazo
la serikali Na.42 la mwaka 2010.
Sheria hizo na kanuni zinaweka
masharti ya msingi kwa ajili ya kuzingatiwa na mkulima, mnunuzi na msindikaji
wa chai ili kuhakikisha kuwa chai inayozalishwa na kusindikwa inakidhi ubora
unaokubalika Kimataifa ili kuiwezesha kupata soko la uhakika.
Aidha sheria hii inalenga kumlinda
mlaji au mtumiaji wa bidhaa za chai ili aweze kupata chai yenye ubora wa
uhakika na hivyo kumuongezea kipato.
Wakulima wadogo wapatao 15,000
waliopo wilayani Rungwe mkoani Mbeya huzalisha wastani wa jumla ya kilo milioni
20 kwa mwaka ambayo ni sawa na tani 20 ambayo ni nusu ya wakulima wadogo
wote nchini.
Idadi hii ya wakulima wa Chai
waliojiunga pamoja wanaojulikana kwa kifupi RSTGA (Rungwe Small Holder
Tea Growers Association) huuza majani ya chai mabichi katika kiwanda cha
Wakulima Tea Company(WTC) ambao kimantiki wanahitaji kupata mfumo mpya wa
maisha yanayowezeshwa na kilimo cha chai.
Manufaa ya wakulima katika kiwanda
hicho yanajionesha kulingana na maelezo yao kwamba umekuwepo umiliki wa pamoja
wa kiwanda ambapo kila mkulima mwanachama ana hisa ya asilimia 30 ya kiwanda
hicho kutokana na mauzo ya majani mabichi ya chai na ongezeko la thamani ya
umiliki wa pamoja.
Kwa kuthamini thamani ya ardhi yao
yenye rutuba wananchi wa wilaya ya Rungwe waliamua kujiunga pamoja na kuunda Umoja
wa Wakulima Wadogo wa Chai(RSTGA) mwaka 1998 ukiwa na lengo la jumla la
kuboresha maisha ya wakulima hao kwa
kuongeza mapato yatokanayo na majani mabichi ya chai na ongezeko la thamani ya
umiliki wa pamoja.
Bw. Steven Mwaikuka mkulima na mkazi
wa kijiji cha Katumba mmoja wa wanachama
wa (RSTGA)anasema kuwa kuwepo kwake katika umoja kumemuwezesha kujenga nyumba
ya kisasa yenye umeme na maji ambapo pia anapata gawio la hisa kutoka kiwanda
cha chai cha WTC.
Anasema mbali na hisa anazopata kila mwaka kutoka
kiwandani hapo ananufaika na malipo ya
pili kila baada ya miezi mitatu ikiwa ni pamoja na kukopeshwa pembejeo za kilimo wanazorejesha kwa kukatwa baada ya kuuza majani mabichi kila
mwezi sh.75/.
Bi. Josephine Kindole Njunwensi(56)
ni mkulima wa kijiji cha Bujesi ni mmoja kati ya wakulima wa chai mahiri
wa zao hili ambaye mwaka huu ametunukiwa cheti na zawadi kwa kuwa na
shamba bora la chai kuliko mashamba yote nchini.
Mkulima huyu ambaye ni mjane anasema
kuwa anathamini zao la chai kwa kuwa linamuendeshea maisha yake na kuwa yeye ni
miongoni mwa wanahisa wa Kiwanda cha Chai cha WTC ambapo ananufaika kwa kupata
pembejeo za kilimo na gawio la hisa kulingana na hisa zake zilizopo kiwandani.
Anasema kutokana na kilimo cha chai
ameweza kumudu maisha bila kuwepo mumewe
ambaye kwa sasa ni marehemu aliyemtaja kwa jina la Zephrine Njunwensi na kwamba anashukuru
jitihada za mumewe kumuwekea msingi bora wa maisha ya kilimo cha chai ambacho
kwa sasa ndicho kinachomuendeshea maisha pamoja na watoto wake watano
aliomuachia.
‘’Kutokana na chai nimefungua mradi
wa maduka mawili, duka la vinywaji vya jumla na rejareja na shamba kubwa la
chai, kutokana na ubora wa shamba letu nimefanikiwa kuwa mkulima mwenye shamba
bora la chai nchini’’ anasema Bi. Njuwensi.
Mtendaji mkuu wa Umoja huo Bw.Lebby
Gabriel anasema kuwa tangu kuanzishwa
kwake, umoja huo umekuwa ukitekeleza mikakati mbalimbali kuendeleza maslahi na
ustawi wa wakulima wadogo wa chai wilayani Rungwe ikiwa ni pamoja na kuboresha
uwingi wa majani yanayozalishwa na wanachama, kuwakilisha umiliki wa mwanachama
na maslahi yake.
Anasema kuwa hisa za mwanachama
huwakilishwa katika kampuni yoyote ya kibiashara inayoongeza thamani ya mapato
kwa nia ya kuinua hali ya biashara na kusimamia fedha na miradi ya pamoja na
kufanya mawasiliano baina ya wanachama na wadau wa ndani na nje ya nchi.
Bw. Gabriel anasema kuwa katika
mikakati hiyo ya umoja umeweza kupata mafanikio kutokana na wanaumoja
kuboreshewa maisha yao ambapo hadi sasa uzalishaji wa masjani mabichi ya chai
umeongezeka kutoka tani 3,000 mwaka 2001 hadi tani 20,500 mwaka 2012.
Anasema kuwa sanjari na ongezeko
hilo wakulima wameanza kunufaika na bei ya majani mabichi ya chai kutoka sh.
71.25 mwaka 2001 hadi sh.231.00 mwaka 2013 ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa malipo
ya pili kwa majani mabichi ya chai yaliyofikia wastani wa sh.25/= kwa kilo
mwaka 2012.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa
Wakulima wadogo Bw. Johnson Mwakasege kupitia umoja wao wa (RSTGA) wameweza
kunufaika na ujenzi wa miradi ya maendeleo yenye thamani ya sh. bilioni 1.7
tangu mwaka 2002 ambayo ni ujenzi wa madarasa, zahanati, Nyumba za
walimu,ujenzi wa madaraja, maji safi na kuwezeshwa kuanzishwa kwa chama cha
Akiba na Mikopo SACCOS.
Bw. Mwakasege anasema kuwa mwaka 2012 kampuni ya WTC ilikusanya sh.
milioni 200 kutokana na ununuzi wa hisa kwa wanachama wake ambazo
zinawanufaisha wanachama kwa kupata gawio kila mwaka kulingana na hisa za
mwanachama.
Anasema kuwa thamani ya zao hilo
inatokana na kilimo bora cha chai kutoka kwa wataalamu wa kilimo,uhifadhi wa
mazingira ya kilimo cha zao hilo sanjari na uanzishwaji wa vitalu vya miti
ambapo pia kamati za Chai hupatiwa
mafunzo ya mara kwa mara ya uhifadhi wa vyanzo vya maji.
Mkuu wa wilaya ya Rungwe Crispin
Meela anasema kuwa zao la Chai ni kati ya mazao ya mazao makubwa ya biashara
yanayopatikana wilayani humo na kwamba wakulima hawapaswi kukatishwa tamaa juu
ya kilimo hicho ambacho kinawapa tija na kuinua uchumi wao na uchumi wa wilaya
ya Rungwe.
Post a Comment
Post a Comment