Mwenyekiti wa CHADEMA Mbeya mjini John Mwambingija akionesha vifungu vya Katiba vinavyotoa baraka ya kumvua uongozi kiongozi anayekiuka taratibu
Mwambigija akisisitiza jambo katika kikao na waandishi wa habari ofisini kwake leo alasiri |
Baadhi ya wajumbe wa kamati ya utendaji ya CHADEMA Mbeya mjini |
Aliyekuwa Katibu Mwenezi wa CHADEMA Wilaya ya Mbeya Lucas Mwampiki |
Pichani wa pili kutoka kushoto ni Katibu Mwenezi wa CHADEMA aliyejiuzulu wadhifa wake Lucas Mwampiki |
Katibu CHADEMA wilaya ya Mbeya Christopher Mwamsiku akizungumza juu ya uamuzi wa chama kumvua madaraka Katibu Mwenezi aliyetangaza kujiuzulu |
Katibu Mwenezi Baraza la Wanawake CHADEMA Tabia Mwakikuti akizungumzia ukiukwaji ulifanywa na aliyekuwa Katibu Mwenezi wa chama hicho na uamuzi uliochukuliwa dhidi yake. |
SIKU mbili
baada ya aliyekuwa Katibu Mwenezi wa CHADEMA Jiji la Mbeya Lucas Mwampiki
kutangaza kujiuzulu wadhifa wake, chama hicho kimedai kuwa kilishamvua nafasi
hiyo kabla hajatangaza kujiuzulu kutokana na kuvujisha siri za chama kwa
upinzani.
Mwampiki
ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mwakibete alitangaza kujiuzulu nafasi ya Katibu
Mwenezi kwa madai kuwa amekuwa akitengwa na baadhi ya viongozi wa chama katika
shughuli mbalimbali za chama kwa nafasi yake kama mjumbe.
Akitangaza
uamuzi wa chama hicho dhidi ya Mwampiki, Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Mbeya
mjini John Mwambigija alisema kuwa kikao cha kumvua uongozi Katibu Mwenezi huyo
kiliketi April 14 baada ya kujiridhisha mwenendo wa utendaji wake na yeye alitangaza kujiuzulu nafasi hiyo April 16.
Alisema kuwa
kufuatia hali hiyo uongozi wa chama wilaya kwa kuhusisha vikao halali vya chama
umeridhia kumuengua katika nafasi yake ikiwa ni pamoja na kumzuia kutojihusisha
na shughuli zozote za chama.
Mwambigija
alisema kuwa kiongozi huyo wa juu wa chama
alikiuka vifungu vya katiba ya chama kwa kusambaza taarifa za majungu na
kutokuwa mkweli na muwazi ikiwa ni pamoja na kujihusisha na upotoshaji juu ya
maamuzi halali ya chama.
‘’Tumeamua
kwa kauli moja kumsimamisha shughuli zote za chama kwa mwaka mmoja,ataendelea
na Udiwani wake, hatakiwi kufanya chochote kinachohusiana na chama
chetu,akiendelea tutachukua uamuzi wa kumnyang’anya kadi na kumvua uanachama,’’alisema
Mwambigija.
Alifafanua
kuwa miongoni mwa sababu zilizosababisha avuliwe wadhifa wake ni pamoja na kuvujisha
siri za chama kwa wapinzani ikiwa ni pamoja na kutotoa ushirikiano katika
harakati za chama za sasa za ‘Chadema ni Msingi’ na kwamba uamuzi waliouchukua
uko katika sheria zinazolindwa na Katiba ya chama.
Alisema kuwa
kabla ya kuchukua uamuzi huo chama kilimuita kiongozi huyo katika vikao mara
nne ambapo alishindwa kuhudhuria hivyo uamuzi waliouchukua una baraka za vikao
halali vya chama na kuwa hata hivyo anayo nafasi ya kukata rufaa kwa ngazi za
juu iwapo ataona kuwa hajatendewa haki dhidi ya uamuzi huo.
Kwa upande
wake Katibu Mwenezi aliyejiuzulu Mwampiki alisema kuwa aliamua kujiuzulu baada
ya kuona hapewi ushirikiano na viongozi wenzake na kuwa mara nyingi alipokuwa
akihoji mambo ya msingi ya kukiendeleza chama amekuwa akinyooshewa kidole kama
msaliti.
‘’Nimeamua
kujiuzulu mwenyewe bila kushinikizwa na mtu, kutokana na afya ya chama, kwa
mujibu wa Katiba ya chama ya mwaka 2006 kifungu 6.3.4(a) hiki kinaainisha ukomo
wa uongozi, nimetumikia chama kwa kila hali hadi rasilimali fedha, nitaendelea
kuwa mwanachama mwaminifu,’’alisema Mwampiki.
Aidha
alisema kuwa hajawahi kuitwa na viongozi wala kuandikiwa barua yoyote inayomtaka kufika
ofisini ambayo kulingana na taratibu ilipaswa kumfikia ndani ya siku 14 na yeye
kuweka saini yake hivyo uamuzi wowote uliochukuliwa dhidi yake ulipaswa
kuzingatia taratibu hizo.
‘’Siwezi kuchukuliwa
hatua bila maandishi ambayo yanapaswa kunifikia ndani ya siku 14, vinginevyo
uamuzi wowote dhidi yangu mbali na kutamka kujiuzulu kwangu, haujafuata
taratibu za kisheria,’’alisema Mwampiki.
Post a Comment
Post a Comment