Kikosi cha Mbeya City kikishangiliabaada ya ushindi katika moja ya mechi zake za ligi kuu
USIA WANGU
KWA VIJANA WA MBEYA CITY
LIGI kuu ya
Vodacom imemalizika, Mbeya City timu ambayo imejizolea umaarufu wa aina yake
katika ligi hii imemalizika ikiwa imeshika nafasi ya tatu nyuma ya Azam FC na
Yanga zote za Dar es salaam.
Ni wazi kuwa
ligi hii imekuwa na changamoto za kipekee kwa timu ngeni hususani Mbeya City
ambayo mbali na kuwa ngeni katika ligi hii bali imeibua hisia mpya za hamasa
kutoka kwa mashabiki ambao awali kabla ya kupanda kwa timu hiyo, wengi wao
walikuwa wamejikita katika hamasa na ushabiki wa mambo ya kisiasa.
Historia ya
soka mkoani Mbeya haiwezi kukamilika bila kuzitaja timu ambazo zimewahi kufanya
vizuri katika ligi hiyo nchini kama vile, Tukuyu Stars,Mecco,Tiger na Prison
ambazo zote kwa nyakati tofauti zilikuwemo katika ligi hiyo na kutoa hamasa ya mchezo wa soka mkoani
Mbeya.
Kwa msimu
huu wa ligi chini ya kocha Juma Mwambusi Mbeya City imeweza kugangamala na
kuzitoa jasho timu kongwe katika ligi hiyo na kuonesha njia ya matumaini ya
kufanya vyema katika ligi hii kama ilivyokuwa kwa kaka zao Tukuyu Stars ambayo kwa
mara ya kwanza ilipanda daraja mwaka 1986 na mwaka huo huo kuchukua kombe.
Ilikuwa ni historia
ya kutumainiwa kwa kizazi kipya cha soka nchini kwa mwaka ule wa 1986 ambapo chini
ya ufadhili Ramnik Patel (Kaka)timu ya Tukuyu Stars ambayo ilikuwa ni maarufu
kwa jina la utani la ‘’Banyambala’’ iliweza kupanda daraja na kutwaa ubingwa na
kuonesha maajabu ya timu za mikoani kuzichachafya timu za Dar es salaam.
Ili kuweka vyema historia ya soka mkoani Mbeya
ni vyema nikakitaja kikosi cha Tukuyu Stars ambacho kilivunja mwiko na kuiweka
Mbeya katika ramani ya soka nchini baada ya kutwaa kombe na kufanikiwa
kushiriki klabu bingwa bara la Afrika na klabu bingwa Afrika Mashariki mwaka
1987 na kuweza kutoka sare ya bao 1-1 na timu ngumu ya AFC ya kampala ambayo
awali ilikuwa ikifahamika kwa jina la Abaluya.
Wachezaji
waliounda kikosi cha Tukuyu Stars chini ya kocha Athuman Juma, walikuwa ni
mlinda mlango Mbwana Makata,walinzi wa kati Ali Chimwaga na Daniel Chundu,
Walinzi wa pembeni Godwin Aswile,Suleiman Mathew na Aston Pardon(marehemu).
Viungo wa
ulinzi Yusuf Kamba na Peter Mwakibibi, viungo wa ushambuliaji, Richard
Lumumba(marehemu) na Kevin Haule,Viungo wa pembeni,Karabi Mrisho na Suleiman
Mwankenja.
Baada ya
kuonekana kufanya vizuri katika ligi hiyo timu hiyo iliimarisha zaidi usajili
wake kwa mwaka uliofuata na kuongeza wachezaji mahiri kama vile akina Asanga
Aswile,Ali Mrisho, Salum Kabunda, Justin Mtekele(marehemu),Golikipa Joshua
Kilale,Salum Kussi,Michael Kidilu, Jimmy Mored na Steven Mussa(Marehemu).
Pamoja na
mafanikio hayo Tukuyu Stars ilikumbana na changamoto nyingi za wachezaji wake
kuhamia katika timu kubwa za Yanga na Simba ambapo timu hiyo ilishuhudia
wachezaji wake mahiri kama vile akina Godwin Aswile, Suleiman Mathew,Salum
Kabunda,Steven Mussa na wengineo wakihama timu hiyo.
Ikumbukwe
kuwa Tukuyu Stars ilikuwa ni mwiba mchungu kwa timu ya Yanga ambayo wakati ule
ilipofanikiwa kupanda ligi kuu na kuchukua
ubingwa timu ya Yanga ilishindwa kuwatambia wageni hao ambapo kwa
michezo yote miwili ilifungwa na timu hiyo kwa bao 1-0 mechi iliyochdezwa mjini
Mbeya na 2-1 katika mechi ya marudiano Jijini Dar es salaam.
Kutokana na
historia hiyo ya Tukuyu Stars ambayo ilishuka daraja mwaka 2008 ikiwa chini ya
kocha wa sasa wa Mbeya City Juma Mwambusi, kuna mambo ya msingi ambayo inapaswa
kuzingatia ili kujihakikishia kuwa inadumu katika medani ya ligi kuu kwa miaka
mingi ijayo na hata kutwaa ubingwa.
Pamoja na mafanikio
iliyoonesha Mbeya City kwa msimu wa ligi iliyomalizika jana yapo mapungufu
mengi ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi na kuiweka timu hiyo katika mafanikio ya
ligi kwa msimu ujao.
Katika jumla
mechi 26 ilizocheza timu ya Mbeya City imeshinda mechi 13 imetoka sare mechi 10
imepoteza michezo 3, imefungwa jumla ya magoli 32 na kufunga magoli 21 na
kujikusanyia jumla ya pointi 49 ikishikilia nafasi ya 3 katika msimamo wa ligi
hiyo.
Hadi
inamaliza mzunguko wa kwanza timu hiyo kama ilivyokuwa kwa timu mabingwa wa
msimu huu wa ligi Azam ilikuwa haijawahi kupoteza mchezo hata mmoja.
Katika
mzunguko wa pili wa ligi timu hiyo kama vile iliyoanza kulewa sifa ikajikuta
ikipoteza mechi tatu, ilifungwa na Yanga ambayo katika mzunguko wa kwanza
iliweza kugangamala na kutoka nayo suluhu,ikafungwa na Coastal Union Jijini
Tanga na baadaye kupoteza mechi muhimu ya kutumainiwa iliyowapa ubingwa Azam
katika uwanja wa nyumbani wa Sokoine.
Yapo mengi
yaliyoibuka katika mechi hiyo ikiwemo minong’ono iliyoibuka hata kabla ya mechi
hiyo kwamba Mbeya City imeiuza mechi hiyo na kwamba kwa hali ilivyo ni lazima
timu ya Azam itashinda mechi hiyo na kujihakikishia ubingwa kabla ya kumalizika
kwa ligi hiyo.
Kama
zilivyokuwa fununu za mwanzo Mbeya City iliingia uwanjani na kuonekana ikicheza
chini ya kiwango huku washambuliaji wake wakishindwa kulisogelea lango la Azam
na kusababisha katika kipindi chote cha kwanza mpira ukichezwa nusu uwanja.
Ni mara
chache wachezaji wa Mbeya City walionekana kulikaribia lango la Azam hali
ambayo baadhi ya mashabiki walianza kuingiwa na hofu kuwa huenda timu hiyo
inaweza kufungwa na Azam ambapo dakika moja kabla ya kwenda mapumziko mchezaji
Gaudence Mwaikimba wa Azam alifanikiwa kuandika bao la kuongoza kwa timu yake.
Kipindi cha
pili kilianza kwa kuonekana uhai kwa timu ya Mbeya City, maelekezo ya mwalimu
yalianza kuonesha matumaini ya timu hiyo kurejesha matumaini kwa mashabiki na
hatimaye dakika 70 mchezaji wa Mbeya City Mwagane Yeya alifanikiwa kusawazisha
bao hilo kwa tiktaka.
Matarajio ya
kufanya vizuri kwa kikosi hicho yalianza kuingia na dosari ya mwamuzi wa mechi
hiyo Nathan Lazaro wa Kilimanjaro aliyedaiwa kuibeba timu ya Azam akisaidiwa na
washika vibendera wake Abdallah Uhako na
Godfrey Kihwili wote kutoka Jijini Arusha.
Matokeo ya
mchezo huo yalisababisha vurugu kwa mashabiki hata baadhi ya wachezaji walionekana
kumzonga mwamuzi, hata hivyo kuna mambo mengi ya kujifunza kwa timu hiyo
kutokana na mtiririko mzima wa ligi hiyo na jinsi ilivyomalizika.
Zipo lawama
za moja kwa moja ambazo Mbeya City haipaswi kuzikwepa, kujisahau baada ya kuona
imeanza kupata umaarufu,kucheza chini ya kiwango na kuipa Azam ushindi na kutwaa
kombe kabla ya kumalizika kwa ligi.
Mbeya City
bado haijavunja rekodi iliyowekwa na kaka zao wa Tukuyu Stars, inapaswa
kujiwekea mikakati mbadala ya kuimarisha kikosi kwa kuenzi jitihada za wadau wa
soka wa mkoa wa Mbeya na kwingineko ambao kwa namna moja ama nyingine walikuwa
wakiitakia mafanikio timu hiyo kwa hali na mali.
Kama mdau wa
soka na mwandishi wa habari za michezo sitaacha kuyasema haya ili iwe chachu ya
maendeleo ya klabu hii ambayo mbali na kurejesha hamasa za soka Jijini Mbeya
imesaidia kuongeza fursa za kiuchumi kwa wakazi wa Jiji hilo ambapo mbali na
viingilio vinavyopatikana milangoni, wageni wengi kutoka mikoa ya jirani huja
kuishangilia timu hiyo.
Mbeya City
inatakiwa ijifunze kwa watangulizi wake ambao hadi sasa wanaonekana kusuasua
katika ligi hii, ikumbukwe pia timu ya Prison iliyodumu katika ligi hii muda
mrefu ilishuka daraja mwaka 2011 ikiwa chini ya kocha ambaye kwa sasa ndiye
kocha wa Mbeya City Juma Mwambusi.
Hadi sasa
bado inaendelea kupumulia mashine kwa kila msimu kunusurika kushuka daraja
ambapo kwa msimu huu almanusura ishuke daraja ambapo imemaliza ligi hiyo ikiwa
na jumla ya pointi 28 ikiwa na jumla ya michezo 26 na kufungwa jumla ya magoli
25 huku ikiwa imeshinda mechi 6 na kutoa sare mechi 10 na kupoteza mechi 10.
Timu ya
Mbeya City inamilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya ambapo imepanda daraja
msimu huu wa ligi.
Kikosi cha
Mbeya City kiliongozwa na kocha Juma Mwambusi na wachezaji David Burhani/Geofrey Julius,Hassan
Mwasapili/Mohamed Kijuso,Hamad Kibobile,Yusuf Abdallah,Yohana Morris,Christian
Sembuli,Hamid Mohamed,Kenny Ally,Saad Kipanga,Mwagane Yeya,Deus Kaseke,Aziz
Sibo,Antony Matogolo,Yusuf Wilson,Francis Castor na Jeremiah John.
Post a Comment
Post a Comment