Marehemu Adam Msyaliha aliyekuwa Mwenyekiti wa Programu ya Chadema Ni Msingi Mbeya mjini |
Marehemu Adam Msyaliha enzi za uhai wake |
MWENEYEKITI
wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo Programu ya ‘Chadema Ni Msingi’ Mbeya
mjini Adam Msyalika(26) amefariki ghafla baada ya kuanguka bafuni nyumbani kwa
baba yake mzazi Mzee Msalika eneo la Mabatini Jijini Mbeya.
Kwa mujibu
wa taarifa za Mwenyekiti wa Chadema Mbeya mjini John Mwambigija alisema kuwa
marehemu ambaye pia alikuwa Katibu wa vijana wa jimbo la Mbeya mjini alianguka
bafuni nyumbani kwa baba yake majira ya saa 5:00 asubuhi na baadaye alikimbizwa
katika Hospitali ya Rufaa Mbeya.
Alisema kuwa
alipofikishwa katika hospitali hiyo alilazwa katika wodi namba 11 ambako alipatiwa
matibabu lakini hali yake iliendelea kuwa mbaya hadi kifo chake majira ya saa
5:20 siku iliyofuata.
Mwambigija
alisema kuwa marehemu ambaye alikuwa ni mhitimu wa Chuo Kikuu cha Mwalimu
Nyerere Jijini Dar es salaam ambako alipata Diploma ya Ofisa Uhusiano aliingia
katika harakati za CHADEMA akiwa shule ya sekondari mwaka 2006 na kushika
nyadhifa mbalimbali kwa ngazi ya Kata hadi mkoa.
Alisema ndani
ya chama alikuwa ni kijana mchapakazi aliyeamini katika msimamo wake bila
kuyumbishwa ikiwa ni pamoja na kuchangia mawazo yenye kukijenga chama hicho
katika harakati mbalimbali za uongozi na chaguzi mbalimbali za ndani na nje ya mkoa.
Naye
Mwenyekiti wa Rasilimali na Fedha wa kanda ya Nyanda za Juu Kusini wa chama
hicho Lazaro Ngonyani alisema kuwa Marehemu ambaye alimaliza kidato cha sita
katika sekondari ya Mlima Mbeya alishika nyadhifa mbalimbali za uongozi wa
chama hicho kuanzia mwaka 2006.
Ngonyani
alisema kuwa marehemu kabla ya kuanguka alipata mshituko na kuanguka kisha
akakimbizwa katika hospitali ya Rufaa Mbeya ambako ghafla alipooza upande wa
kushoto na baadaye kufariki dunia akiwa katika harakati za matibabu.
Alisema
marehemu anatarajiwa kuzikwa katika makaburi ya Kijijini kwao Iyula huko wilaya
Mbozi mkoa wa Mbeya.
Post a Comment
Post a Comment