UWANJA wa
kisasa wa michezo utakaogharimu jumla ya sh. Bilioni 8, umeanza kujengwa
wilayani Chunya Mkoani Mbeya.
Uwanja huo
wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 50,000 pia unatarajiwa kuwa kitega uchumi
cha aina yake kuwepo katika wilaya ya Chunya na mkoa wa Mbeya na katika wilaya
za mikoa mingine nchini mbali na Jiji la Dar es salaam.
Akizungumzia
ujenzi wa uwanja huo Mkuu wa wilaya ya Chunya Deodatus Kinawiro alisema kuwa
uwanja huo unajengwa na wananchi wenyewe kwa kushirikiana na Halmashauri ya
wilaya hiyo ambapo pendekezo la ujenzi wa uwanja huo aliliwasilisha kwenye
vikao vya halmashauri na kuridhiwa na baraza la Madiwani.
Alisema
katika vikao vyake, ambapo Halmashauri ya wilaya hiyo ilipendekeza kutenga Sh. Milioni
70 katika bajeti yake ya kila mwaka huku kila mwananchi akiwajibika kuchangia
ujenzi wa uwanja huo kuanzia sh.2000 kwa kila mwaka ambapo matazamio uwanja huo
unatarajia kukamilika 2016.
Katika mkakati
wa ujenzi huo Kinawiro alisema kuwa wadau mbalimbali wamejitokeza kuchangia
ujenzi wa Uwanja huo ambao upo katika hatua za awali wakiwemo Kampuni ya Lafarge
inayozalisha saruji aina ya Tembo waliochangia saruji mifuko 1000.
Akizungumza
wakati wa kuchangia ujenzi wa uwanja huo Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Lafarge
Catherine Langreney alisema kuwa kampuni yake imepokea maombi hayo kutoka kwa
Mkuu wa wilaya ya Chunya na kukubali kuchangia saruji mifuko 1000.
Langreney
alisema kuwa mbali na kufanya biashara kampuni yake inachangia huduma mbalimbali
za kijamii kwa wananchi waliopo maeneo ya karibu na kiwanda chao hivyo msaada
huo ni sehemu ya huduma zao za kawaida kwa wananchi.
‘’Huduma
zetu zinazingatia mahitaji ya jamii inayotuzunguka bila kujali faida,’’alisema
Langreney.
Alibainisha
kuwa kuwepo kwa uwanja huo kutatoa fursa ya ajira kwa wananchi wa maeneo hayo
na kuinua uchumi wao.
Kwa upande
wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya
Wilaya ya Chunya Sophia Kumbuli alisema kuwa uwanja huo utakuwa ni sehemu
ya Mapato ya Halmashauri hiyo na kuwa wadau mbalimbali wamejitokeza kuchangia
uwanja huo kwa nguvu zao na mali zao.
Alisema kuwa
fursa ya kuwepo kwa uwanja huo wa kisasa itainua michezo ndani ya wilaya hiyo
na mkoa wa Mbeya kwa ujumla hivyo wadau wanapaswa kujitokeza kuchangia
maendeleo ya uwanja huo.
Naye Katibu wa Kamati ya Ujenzi wa uwanja huo Solo Tuyagaje alisema kuwa hadi
sasa jumla ya sh. Milioni 107 zilichangwa na wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja
na makampuni yanayochimba madini wilayani humo na wachimbaji wadogo.
Alisema
wadau wengine waliochangia ni pamoja na Mbunge wa Lupa Victor Mwambalaswa
aliyechangia jumla ya Milioni 11 ambapo Halmashauri ya wilaya imechangia jumla y
ash. Milioni 30 kwa mwaka wa fedha wa 2013/14.
|
Post a Comment
Post a Comment