Wanahabari nchini wametakiwa kutumia fursa ya kuwepo kwa Mfuko wa kuwawezesha wanahabari wa TMF kutafiti na kuandika habari zitakazoibua uchunguzi utakaosaidia jamii.
Wakizungumza wakati wa semina ya siku moja iliyoandaliwa na Mfuko wa Vyombo vya Habari TMF kwa baadhi ya wanahabari wa mkoa wa Mbeya, waandishi nguli wa tasnina hiyo Edda Sanga na Ndimara Tegambwage waliwataka wanahabari kutumia vyema taaluma yao kuibua,kuandika na kufanyia utafiti habari za uchuguzi ambazo zitaongeza chachu ya maendeleo katika jamii.
Kwa upande wake Tegambwage alisema kuwa wanahabari wengi wamekuwa wakiripoti habari za mijini ambazo hazigusi uhalisi wa maisha ya wananchi wenye matatizo hivyo wanayo fursa ya kuandika habari kwa undani wakilenga kuibua na hatimaye kufanyia uchunguzi mambo yanayosababisha kero miongoni mwa jamii.
Alisema kuwa mwandishi anayejikita katika habari za uchunguzi anapaswa kufanya utafiti wa awali utakaolenga kuinufaisha jamii na kuangalia maslahi itokanayo na uchunguzi atakaoufanya.
''Unachotaka kuchunguza kiangalie kimelenga nini, kina uzito gani katika habari na pia uangalie upya wake katika habari,''alisema Tegambwage.
Aidha alisema kuwa katika jamii kumekuwa na matukio mengi yanayoibuka na kuelezwa kuwa yanatokana na imani zinazoitwa kuwa ni za Ushirikina na kuwa mwanahabari anapaswa kuandika hali halisi inayosababisha jambo linaloelezewa kuwa linahusishwa na imani za ushirikina bila kuutaja ushirikina wenyewe.
''Ni ngumu tafsiri yake neno Ushirikina, elezea uhalisia wa tukio lenyewe kulingana na stori ilivyo,'' alifafanua.
Naye Edda Sanga aliwakumbusha wanahabari kuandika habari kufanya bidii ya kujisomea badala ya kudhani kuwa taaluma hiyo inaweza kufanywa bila kufuata maadili yake.
Alisema lipo kundi la watu waliojiingiza katika taaluma ya habari na kufanya mambo ya habari bila kufuata maadili na kusababisha upotofu wa maadili ya taaluma hiyo hivyo ni vyema kila mwandishi akajitahidi kusoma na kujua miiko ya habari ili kutopotosha umma.
''Kwa sisi tuliokuwa tukitangaza zamani, tunaposikiliza matangazo ya kwenye Redio nyingi za sasa, kwa kweli Wana ' boa' hawataki kwenda na changamoto zilizopo,''alisema.
Kadhalika aliwataka wanahabari kufuatilia kwa kina uozo unaotendeka kwa baadhi ya viongozi wa umma ambao kimsingi walipaswa kuwa ni kioo kwa wananchi.
Wakati huo huo aliyekuwa Ofisa Ruzuku wa TMF Japhet Sanga ameaga rasmi kulitumikia shirika hilo alilodumu nalo tangu mwaka 2010 na nafasi yake inachukuliwa na Dastan Kamanzi.
Akizungumza juu ya kuachia nafasi hiyo Sanga alisema kuwa pamoja na kuwa amemaliza muda wake wa kulitumikia Shirika hilo ataendelea kuwa karibu na wanahabari kwa ushauri na mambo mbalimbali yahusuyo maendeleo ya taaluma hiyo na maendeleo kwa waandishi wa habari.
Alisema wanahabari wamekuwa wakipata changamoto nyingi katika utendaji wao na kuwa kuwepo kwa Mfuko wa TMF umesaidia kuizindua serikali katika mambo mengi ambayo ilikuwa imejisahau hivyo ni fursa kwa wanahabari kuutumia vyema mfuko huo kwa kuibua kero zitakazowakumbusha watendaji kuitumikia jamii.
| | |
|
Post a Comment
Post a Comment