SERIKALI
imewataka wafanyabiashara wa mazao ya wanyama na Uvuvi waliopo mipakani kuboresha
mazingira ya biashara zao ili yawe kivutio kwa wanunuzi wa ndani na nchi jirani.
Akizungumza
na wafanyabiashara wa biashara ya dagaa waliopo mpakani mwa Tanzania na Zambia
katika mji mdogo wa Tunduma Waziri wa Mifugo na Uvuvi Dkt. Titus Kamani alisema
ili wafanyabiashara hao wanufaike zaidi wanapaswa kuboresha mazingira ya biashara
hizo.
Alisema,
wanunuzi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi jirani wanaangalia zaidi ubora wa
mazingira yanayoendeshewa biashara hizo na kuwa mazao ya samaki yanahitaji usafi
kutokana na mazingira ya aina ya biashara yenyewe.
‘’Mnajua
samaki na dagaa wanahitaji utunzaji na mazingira safi,watu wengine wakikutana
na mazingira yasiyo masafi, wanapata kinyaa wanashindwa kununua bidhaa zenu,’’alisema
Dkt. Kamani.
Kwa upande
wake Mkuu wa wilaya ya Momba Abihudi Saideya alisema kuwa wakazi wa wilaya ya
Momba wanapata samaki kupitia Ziwa Rukwa ambalo liko upande wa bondeni mwa
wilaya hiyo.
Alisema kuwa
hata hivyo kwa kipindi cha miezi sita ziwa hilo lilifungwa kutokana na
uharibifu wa mazingira uliofanywa na wananchi na hivyo kusababisha ziwa hilo
kukauka na uzalishaji wa samaki kuwa duni.
‘’Tulilifunga
ziwa Rukwa kwa ushirikiano na Wilaya washirika watumiaji wa Ziwa hili,
tukalifungua baada ya miezi 6 hata hivyo bado uzalishaji uko chini,’’alisema Saideya.
Naye Ofisa Uvuvi
wa wilaya ya Momba Ali Libenanga alisema kuwa kwa kipindi cha miezi 6 baada ya
kufunguliwa ziwa hilo jumla ya milioni 108 zimekusanywa kutokana na kodi za
uvuvi na kuwa hata hivyo samaki wanaovunwa ziwani humo wamedumaa hawakui katika
kiwango kinachostahili.
Dkt Kamani
alifanya ziara ya kutembelea wafanyabiashara wa dagaa waliopo mpakani Tunduma
ili kuangalia mazingira ya biashara hizo katika maeneo ya mipakani ambapo pia
alikutana na watendaji wa Halmashari ya Mji wa Tunduma.
Post a Comment