Sheikh Ponda Issa Ponda |
Waumini wa dini ya Kiislamu wakifurahia kuachiwa kwa Sheikh Ponda hii ilikuwa mwaka 2014(Picha Maktaba) |
Na Bloga Wetu, Morogoro.
MACHOZI ya furaha na sauti za kumtukuza
Mwenyezi Mungu za Takbir!!! Allahu Akbar!! Zilihanikiza viwanja vya Mahakama ya
Hakimu Mkazi mkoa wa Morogoro baada ya mahakama hiyo kumwachia huru Kiongozi wa
Taasisi na Jumuiya za Kiislamu Sheikh Ponda Issa Ponda.
Kuachiwa huru kwa Sheikh Ponda aliyekaa
mahabusu takribani miaka miwili kumefuatia upande wa mashtaka kushindwa
kuthibitisha mashtaka yaliyokuwa yakimkabili ambayo yalifunguliwa dhidi yake.
Hakimu mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo Mary
Moyo alitoa uamuzi huo huku Sheikh Ponda akitokea rumande alikokuwa amekaa kwa
zaidi ya miaka miwili kutokana na dhamana yake kuzuiwa na mkurugenzi wa
mashtaka DPP kwa kile kilichoelezwa kuwa maslahi ya Taifa.
Mara baada ya kuachiwa huru Sheikh Ponda
aliishukuru Mahakama kwa kutenda haki ingawa pia aliilaumu kwa kuchelewa
kutenda haki hiyo mapema kutokana na dhamana yake kuzuiwa.
Sheikh Ponda alikuwa akikabiliwa na
mashtaka mawili ambayo ni kudaiwa kutoa maneno yenye kuumiza imani za dini
ikiwa ni pamoja na kutoa ushawishi wa watu kutenda kosa, makosa ambayo alidaiwa
kuyatenda Agosti 10, 2013 kwenye viwanja vya shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege
Manispaa ya Morogoro.
Kwa upande wa mashtaka kesi hiyo
iliwakilishwa na wakili wa serikali Mwandamizi Bernard Kongola,George Mbalassa
na Sunday Hyera ambapo upande wa utetezi uliwakilishwa na wakili Juma
Nassoro,Bathoromeo Tarimo na Abubakar Salim.
Post a Comment