Ads (728x90)

Ofisa wa Jeshi la Magereza akiwa na picha ya enzi za Uhai ya Marehemu Hassan Mlwilo aliyewahi kuwa kocha wa timu ya Prison na baadaye kuwa Ofisa Michezo wa Jeshi la Magereza.

Baadhi ya Maofisa Magereza wakiungiza mwili wa marehemu Hassan Mlwilo kwenye gari kwa ajili ya kuelekea kwenye makaburi ya Mabanda Rujewa wilayani Mbarali jana asubuhi

Jeneza lenye mwili wa marehemu Hassan Mlwilo kabla ya mazishi Rujewa wilayani Mbarali jana



Maofisa wa Magereza wakiliweka jeneza lenye mwili wa aliyewahi kuwa kocha wa timu ya Prison kwa ajili ya ibada ya kuswalia kabla ya mazishi huko Rujewa wilayani Mbarali jana.

Maofisa wa Jeshi la Magereza wakiwa wamesimama kuashiria heshima za mwisho kabla ya mazishi ya marehemu Hassan Mlwilo kwenye makaburi ya Mabanda, Rujewa wilayani Mbarali jana asubuhi

(PICHA KWA HISANI  YA  VETERANI WA TIMU YA PRISON  ALPHONCE MWAKILEMBE MAARUFU KWA JINA LA KEI'  ALIZOTUMA KWA MTANDAO KWA WHATSAPP  KWENYE BLOGU HII)
‘’BABA!!! Umetuacha wakiwa!!  hatutakuona tena!!! ni sauti ya maombolezo iliyojaa simanzi ya  mtoto mdogo wa marehemu Hassan Yassin Mlwilo(58), sauti iliyohanikiza hewani na kugonga nyoyoni mwa kundi kubwa la waombolezaji waliohudhuria maziko ya marehemu Mlwilo nao wakajikuta wakifuta machozi kwa leso zao wakikumbuka maisha ya marehemu.
Ni vigumu kuamini kwa wakati huo, bali ni wajibu kukubali na kuamini mipango ya Mwenyezi Mungu anapoamua kuvichukua viumbe vyake na kuviweka katika makao ya milele,tunalazimika kukubali na kuamini kuwa ndugu yetu kipenzi tuliyemzoea kwa wema wake Hassan Mlwilo hatunaye tena duniani.
Mlwilo ambaye ameacha mke na watoto wanne amezikwa jana kwenye makaburi ya Mabanda mjini Rujewa wilayani Mbarali kwa heshima zote za kijeshi kutokana na utumishi wake akiwa Ofisa wa Jeshi la Magereza akijihusisha zaidi na michezo.
‘’Kijana huyu alikuwa mchamungu,alikuwa mcheshi ni vigumu kubaini wakati gani amechukia kwa kuwa muda wote alikuwa ni mkarimu na mcheshi,tumempoteza kijana mwema, Mungu amhifadhi katika makao yake ya kudumu,’’alisikika akisema mmoja wa wazee wa mjini Rujewa ambaye alikuwa akimfahamu vyema marehemu Mlwilo.
Mlwilo alifariki juzi katika hospitali ya Muhimbili Jijini Dar es salaam alikokuwa amelazwa kufuatia maradhi ya ini ambayo yalikuwa yanamsumbua kwa takribani miezi miwili iliyopita.
Meneja wa timu ya soka ya Tanzania Prison inayocheza daraja la kwanza Athanas Kilindo alisema kuwa marehemu Mlwilo kabla ya kuhamishiwa hospitali ya Muhimbili alilazwa katika hospitali ya Rufaa Mbeya hadi Januari 16.
‘’Alihamishiwa Muhimbili kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi zaidim bahati mbaya Januari 21 majira ya saa 5:30 ametutoka,’’alisema Kilindo.
Kilindo alisema kuwa enzi za uhai wake Mlwilo alipata kufundisha timu mbalimbali za mkoa wa Mbeya ikiwa ni pamoja na timu ya Tiger ya Tunduma na baadaye kuifundisha timu ya Prison kabla ya kuwa mwalimu wa michezo wa Jeshi la Magereza.
‘’Tumempoteza mdau muhimu wa michezo ndani ya Jeshi la Magereza alikuwa na uwezo mkubwa na alijitikiza katika michezo yote, hadi anafariki alikuwa ni Ofisa michezo wa Jeshi la Magereza,’’alisema Kilindo.
Mbali na maofisa wa Jeshi la Magereza mkoani Mbeya kushiriki kwa hali na mali katika mazishi hayo baadhi ya wanamichezo hasa wachezaji wa timu ya Prison walionekana kugubikwa na majonzi huku baadhi yao muda wote wakionekana kujifuta machozi.

Marehemu Mlwilo amezikwa jana saa nne kwenye makaburi ya Mabanda mjini Rujewa wilayani Mbarali na ameacha mjane na watoto wanne kati yao wawili ni watoto wa  kiume, Mwenyezi Mungu aiweke roho ya marehemu mahala pema, Amiin!!!
Siku ya Ijumaa mara baada ya swala ya Ijumaa Imamu wa Msikiti wa Isanga Jijini Mbeya Shekhe Ibrahimu Bombo alitoa taarifa za msiba wa Mlwilo huku akiashiria mahala ambapo marehemu Mlwilo alikuwa akipenda kukaa wakati wa ibada ndani ya msikiti huo na kuelezea kuwa hiyo ni dalili njema kwa Mchamungu ambaye alijali na kukumbuka wajibu wake wa kufanya ibada katika maisha yake.
''Shekhe Hassan ametutoka, tutamkumbuka kwa uchamungu wake, mara kwa mara alikuwa akipenda kukaa kwenye kona ile kila wakati wa ibada, Mwenyezi Mungu amsamehe makosa yake,''alisema Sheikh Bombo.

Post a Comment

Post a Comment