Ads (728x90)



Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Luckiness Amlima akisikiliza kero kutoka kwa mmoja wa wananchi wa mji wa Namtumbo alipozungumza na wananchi mwishoni mwa wiki.


Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Luckiness Amlima akisisitiza jambo mbele ya wananchi wa mji wa Namtumbo


Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Luckiness Amlima akizungumza na wakazi wa mji wa Namtumbo
MKUU wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma Luckiness Amlima amewaonya wanaume wa wilayani humo kuacha kuoa wake wengi ambao huwageuza kama  matrekta kwa ajili ya shughuli za kilimo mashambani.

Kadhalika Mkuu huyo amewataka wanawake kwa upande wao kutumia mbinu mbadala kwa ajili ya kulinda ndoa zao ili wanaume wasishawishike kuwaolea wanawake wengine.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliozihusisha kata mbili za Namtumbo na Rwinga na vijiji vyake saba Amlima alisema ipo desturi kwa wanaume wa wilaya hiyo kuwatumia wanawake kama nyenzo ya kuwatumikia wanaume katika shughuli za uzalishaji mali.

‘’Nyie wanaume wa Namtumbo punguzeni kuoa oa na kuwafanya wanawake kama matrekta ya kulimia, hali hiyo inachangia kupunguza uzalishaji wa chakula, maana nguvu ya wanawake pekee haitoshi kutumika kuzalisha chakula mashambani,na nyie akina mama wenzangu mjirekebishe,mnashindwa kuzitunza ndoa zenu ndio maana wanaume hawatosheki wanawaolea wanawake wengine,’’alisema Amlima.

Alisema mbali na wanawake pekee kutumika katika uzalishaji wa chakula mashambani, wakati wa mavuno chakula hicho hicho kinachozalishwa na mwanamke kinauzwa na mwanaume ambaye kutwa hushinda kucheza bao na kuongeza mke mwingine hali ambayo inachangia kuwepo kwa unyanyasaji na dhidi ya mwanamke na hata kukosekana kwa chakula cha akiba katika kaya.

‘’Nyie ni watani zangu nitawaeleza ukweli kama nawakosea naomba mnisamehe lakini napaswa kusema ukweli juu ya vitendo vya unyanyasaji wanavyofanyiwa wanawake wenzangu, mimi kama mwanamke mwenzenu najisikia uchungu,’’alisisitiza huku kauli yake ikisindikizwa kwa vigelegele kutoka kwa akina mama waliohudhuria mkutano huo.

Aidha alisema kuwa kipindi cha mavuno wananchi wanamaliza  chakula chote ghalani kwa ajili ya  ngoma, vigodoro na unyago kiasi cha kukosa chakula cha akiba na mbegu  hali ambayo inaweza kusababisha kuibuka kwa baa la njaa.

‘’Tukipunguza mambo ya vigodoro na unyago wakati wa kiangazi, hatutafikwa na njaa wakati wa masika, tujitahidi kuhifadhi chakula na kupunguza ngoma na unyago,’’alifafanua Mkuu huyo wa wilaya ambaye huo umekuwa mkutano wake wa kwanza hadharani tangu ateuliwe na Rais kushika wadhifa huo Julai mwaka huu.

Katika hatua nyingine Amlima amesema kuwa wakazi wa mji huo ambao asilimia kubwa ni waislamu wanapaswa kuwahimiza watoto wao kujifunza imani za kiroho kwa kuwapeleka Madrasa na katika shule za kidunia ili wamjue Mungu na wajue mambo ya dunia na hatimaye waweze kuishi katika maadili mema yanayompendeza Mungu hapa duniani na baada ya kuondoka duniani.

Post a Comment