DOSARI UANDIKISHWAJI VISIWANI NINI KIPO NYUMA YA PAZIA.
Na, Rashid Mkwinda.
ALFAJIRI ya Jumamosi Septemba 16 nilikuwa ni miongoni mwa abiria lukuki waliosafiri kwa boti ya Sea Express kuelekea visiwa vya karafuu vya Zanzibar , pamoja nami kulikuwa na raia wengi wa kigeni ambao walionekana kama ni mara yao ya kwanza kuelekea visiwani.
Niliwafahamu raia hao baadaye wakati abiria wote tulipoingia katika Boti hiyo na safari kuanza rasmi kuelekea visiwani. Sikupata taabu sana kujua kuwa ilikuwa ni mara yao ya kwanza kufika visiwani humo baada ya kuona namna ambavyo wanaingia na kutoka nje ya boti kwa nia ya kupiga picha meli na baadhi ya visiwa vilivyopo katika bahari ya Hindi.
Walikuwa ni watalii miongoni mwa watalii kutoka nchini Uingereza,Japan na Ufaransa niliwajua kutokana na aina ya mazungumzo yao na wajihi wao.Kama ilivyo desturi ya boti iendayo kwa kasi ndani ya saa moja na nusu tukawa tumeingia katika bandari ya Zanzibar .
Mandhari ya visiwa hivi hususani katika bandari ya Zanzibar imetofautiana kidogo na ile ya Dar es salaam na kwingineko bali inaonekana kama ni bandari yenye meli nyingi zaidi zinazoingia na kutoka nje ya nchi, nilishuhudia zaidi ya meli 25 zikiwemo boti zikiwa zimeegeshwa mbali na bandari hiyo zingine zikisubiri kushusha mizigo huku zingine zikisubiri ratiba yake ya safari kwa siku inayofuata.
Nilishuka katika boti hiyo moja kwa moja nikaingia mitaani na kuelekea katika mtaa mmoja maarufun unaojulikana kwa jina la Darajani. Huko nilikuta pilikapilika nyingi zinazoshabihiana kabisa na maeneo ya aina hiyo upande wa bara ambapo bidhaa mbalimbali zilionekana kuuzwa na watu mbalimbali kutoka mikoa ya bara walionekana wakinunua bidhaa na kurejea nazo bandarini.
Jua la asubuhi lilizidi kuvuta mandhari ya rangi ya samawi na ile ya bluu bahari na kuleta faraja kwa kila aliyepo visiwani humo huku upepo mwanana ukiwa ni moja ya burudani inayokidhi na kushawishi kila aingiaye katika visiwa hivi vya karafuu atamani kuweka makazi ya kudumu katika visiwa hivi.
Ni visiwa ambavyo awali wakati wa Mapinduzi havikuzidi watu 150,000 na baadaye wakati wa Muungano idadi ya wakazi wake waliongezeka hadi kufikia wakazi 300,000 na kuzidi kuongezeka kulingana ana ujio wa watu wengi kutoka maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya nchi hadi kufikia wakazi 700,000 ambapo kwa sasa wakazi wake wanakadiria kufikia zaidi ya milioni 1.5.
Tofauti ya siku zingine za kawaida hoteli nyingi zilikuwa zimefungwa kutokana na mwezi huo kuwa ni mwezi mtukufu wa Ramadhan ambapo baadhi ya watu nilioongozana nao walianza kuilaani hali hiyo na kufikiria namna ambavyo wanaweza kustaftahi ilhali wakazi wengi wa visiwa hivi walikuwa katika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Hali ya utulivu wa bahari na upepo mwanana wa visiwa hivi ulishabihiana kabisa na namna desturi za wenyeji wa visiwa hivi ilivyo na muonekano wao ulioshitadi kwa nyuso za ukarimu,upole na bashasha ambapo kwa muda wote walionekana ni wacheshi na mahiri wa kuzungumza kwa ufasaha na haraka lakini kwa kituo.
Desturi ya wakazi wa visiwa hivi ilipambwa na aina ya mavazi ambayo yalikuwa yanavaliwa na wanawake ambapo ilikuwa ni nadra kumuona mwanamke Kigori ama mtu mzima akiwa amevaa nguo iliyoonesha utupu au sehemu kubwa ya mwili wake kubaki wazi. Aghalabu ya wakazi wa visiwa hivi walikuwa katika mavazi ya Buibui.
Mara baada ya kupata mahala pa kujisitiri kwa malazi nikapata taarifa kuwa siku hiyo kulikuwa na zoezi la uandikishwaji wa daftari la kudumu ambalo ni mchakato wa serikali wa kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura kwa awamu ya pili, nilipata mshawasha wa kufuatilia kwa kina hatua kwa hatua juu ya namna ambavyo uendeshwaji wa daftari hilo unaendelea.
Nilitafuta usafiri wa kuelekea katika vituo vya uandishwaji wa daftari la kudumu na kupitia katika vituo kadhaa vilivyopo mkoa wa Unguja kaskazini jimbo la Nungwi na jimbo la Mkwajuni katika Shehia za Kilindi, Kigunda, Tazari, Nungwi, Kilimani, Kidoti, Fukuchani, Bwereu na Mwange.
Nilizidi kuvutiwa zaidi na mandhari ya visiwa hivi nilipokuwa nikielekea zaidi katika maeneo ya mashambani ambapo niliona namna ambavyo ardhi inayoonesha kila dalili za hapo awali kwamba ilikuwa ikitoa mazao bora kama vile migomba, michungwa, mifenesi,minazi, mihogo ambapo kwa wakati huo mazao hayo yalionekana kama vile ni mazao yaliyopo katika ardhi isiyo kuwa na rutuba.
Niliyafananisha mandhari ya maeneo hayo kama yale ya Kigamboni ambako sehemu kubwa ya mazao ya chakula, mboga mboga na matunda yanayopatikana jijini Dar es salaam hutokea huko.
Nilimuuliza mwenyeji wangu kulikoni hali hii…ilhali inaonekana dhahiri kuwa kuna kila dalili ya mazao hayo kuwa bora iwapo yatasimamiwa vizuri na wakulima kupata mbinu bora za kilimo cha kisasa, jibu nililokutana nalo lilionesha kiwango cha upeo wa hasira na kukata tamaa kwa maisha ya watu wa Zanzibar .
Majibu niliyopewa si tu yalinirudisha miaka ya tisini kabla ya mfumo wa vyama vingi havijaanza nchini ambapo pia nilipata bahati ya kutembelea visiwa hivi na kukaa kwa muda mrefu bali yalinipa upeo kuwa inawezekana kila mwananchi wa visiwa hivi ni mwanasiasa ama ni mkereketwa wa mambo ya kisiasa.
Katika miaka ile ya tisini kabla ya mfumowa vyama vingi kuanza wananchi walikuwa wakiishi kwa amani na utulivu huku desturi ya vurugu na mikikimikiki ni mambo ambayo yalikuwa ni sawa na msamiati mgumu kwa wakazi wa visiwani ambapo hata foleni kwa ajili ya watu kuingia katika daladala maarufu kwa jina la Chai Maharage haikuwa ya kugombewa kama ilivyo kwa sasa.
Miaka ile ya tisini gari la abiria likisimama watu huingia kwa utaratibu bila vurugu ambapo watu wakienea katika siti,gari huondoka na hakuna mtu aliyethubutu kuingia katika gari ambalo limejaa.
Jamaa alinijibu kuwa; ‘’Huu ndio ukuaji wa nchi na uharibifu wa maadili na kukithiri kwa tatizo la uongozi mbovu usiojali maisha ya watu… ‘’twaijua Zanzibar njema yenye neema atakaye na aje’’lakini kwa sasa Zanzibar si yenye neema tena viongozi waliopo wanajua kutawala wala si kuongoza, wangekuwa wanaweza kuongoza hali hii isingeweza kutokea.
Kauli ya jamaa huyu ilinipa maswali mengi kichwani ambapo hakuishia hapo tu bali aliendelea kwa kusema kuwa, hakuna kinachoweza kuendelea kwa sasa kwa kuwa kila kiongozi anayekaa madarakani anachofikiria ni namna ya kujiimarisha katika madaraka kwa kutumia fedha ambazo zingeweza kuwasaidia wakulima kuwapatia pembejeo za kilimo kwa kusababisha kuwepo na vurugu katika uchaguzi.
Wakati akiendelea kunisimulia habari hizi ghafla gari tulilokuwemo lilisimama tulipofika katika shehia ya Fukuchani ambako kulikuwa na zoezi la uandikishwaji daftari la kudumu la wapiga kura, hapo tulikutana na makundi ya vijana na wananchi waliokuwa wamesimama pembeni mwa kituo hicho umbali upatao mita 200.
Tulifika eneo hilo na kuwakuta vijana hao kila mmoja akizungumza kwa mtazamo wake namna ambavyo zoezi hilo la uandikishwaji linavyoendeshwa ambapo wengi wao walionesha kuchukizwa na kutoa maneno makali yaliyonisababisha nifikirie kufuta hisia zangu kwamba Wazanzibar ni watu wapole na wakarimu wasiozoea mikikimikiki na shuruba.
Nilitafakari mara mbili kumaizi hali hii hatimaye kundi la waandishi wa habari lilipowasogelea wananchi hao ndipo niliposikia kila aina ya bezo na kebehi dhidi ya serikali ya Mapinduzi Zanzibar na namna ambavyo wananchi hao wakilalamikia uongozi uliopo madarakani jinsi ambavyo hauwajali wakazi wake.
‘’Unaona sisi ni raia wa Zanzibar tumezaliwa hapa tumesoma hapa na kukulia hapa lakini leo hii tunanyimwa haki ya kupewa vipande(vitambulisho) vya ukaazi….kisa sababu za hisia kwamba sisi tupo kambi ya upinzani, ‘’alisema mmoja wa vijana aliyekuwepo katika kundi hilo aliyejitambulisha kwa jina la Bw.Husein Madai Ali mkazi wa Fukuchani.
Bw. Ali(26)alionesha kadi yake ya kuzaliwa yeye na ile ya ukaazi ya mama yake mzazi na kusema kuwa tatizo kubwa lililopo linatokana na kuhisiwa kuwa wao wako katika kambi ya upinzani hivyo wananyimwa fursa ya kujiandikisha wakijua kuwa hawatakipigia kura chama kinachotawala.
Bw. Ali alienda mbali zaidi kwa kusema kuwa kinachofanyika kwa serikali ni mbegu mbaya inayopandwa kwa wananchi kwa kuwa raia anastahili kujiandikisha na kupata haki yake ya msingi ya kupiga kura na kwamba jambo la ajabu baadhi ya watu wengine hufuatwa majumbani kwao na Masheha na kulazimishwa kwenda kujiandikisha na kupata vitambulisho hata kama hawana sifa.
‘’Sisi tumekuja wenyewe kujiandikisha tunazo sifa zote za kuandikishwa lakini tunakataliwa…wanafuatwa walioko majumbani hata kama hawajatimiza umri wa miaka 18 ili wajiandikishe…hili linatutia mashaka makubwa tuna hisi kama kuna njama za kutuzuia haki yetu ya kupiga kura mwaka 2010,’’alisem,a Bw. Ali.
Mkazi huyo alikuwa ni miongoni mwa wananchi wasiopungua 30 katika kituo hicho cha Fukuchani ambao wote kila mmoja alionesha namna ambavyo amekerwa na uendeshaji huo wa uandikishwaji wa daftari la kudumu ambao kwa mtazamo wao umelenga kuwabagua.
Hali ya aina hiyo ilionekana pia katikaa kituo kingine cha Bwereu, Tazari. Kigunda na Kidoti ambapo katika kituo kilichopo katika makao makuu ya jimbo cha Nungwi hali ilionekana tete zaidi baada ya kukuta vikosi vya askari wa kikosi cha kutuliza ghasia na wale wa KMKM wakiwa wamezagaa kila kona kwa kile kilichoelezwa kuwa walikuwa katika harakati za kulinda usalama zoezi la uandikishwaji wa daftari hilo la kudumu katikam maeneo hayo.
Jambo moja ambalo nilijiuliza kichwani kwangu inakuwaje katika zoezi la uandikishwaji hali inakuwa hivi huku ilhali zoezi hili linatakiwa kuendeshwa kwa njia ya amani na utulivu, kabla sijamaliza kujiuliza swali hili niliona kundi la watu wakizozana na mmoja wa watu ambaye anadaiwa kuwa ni mfuasi wa CCM na wengine wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa CUF.
Mzozo uliokuwepo pale ni vijana wa CUF walikuwa wakimhoji kijana yule ni wapi alipata barua ya kuidhinishwa kupata kitambulisho cha ukaazi ilhali vijana wengine walikuwa wakizungushwa kupata barua hizo.
Tafrani hiyo ilisababisha kundi hilo la vijana kumzuia kijana aliyekuwa akitaka kwenda kujiandikisha kwa madai kuandikishwa kwake kumegubikwa na utata kwani kuna kila dalili za hujuma dhidi ya vijana ambao ni wafuasi wa CUF ambao kwa maelezo ya vijana hao hawatakiwi kujiandikisha kutokana na nia yao ya kutaka kukiondosha madarakani chama cha Mapinduzi kwa njia ya kura mwaka 2010…..INAENDELEA
.....Kundi la vijana lilionekana kumzuia kijana aliyekuwa akitaka kwenda kujiandikisha kwa madai kuandikishwa kwake kumegubikwa na utata kwani kuna kila dalili za hujuma dhidi ya vijana ambao wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa CUF ambao kwa maelezo yao hawakutakiwa kujiandikisha kutokana na kile kilichoelezwa kutaka kukiondosha madarakani chama cha Mapinduzi kwa njia ya kura mwaka 2010.
Tafrani hiyo iliendelea kiasi cha kuwafanya vijana hao kupanda jazba ambapo mmoja wa viongozi katika Shehia hiyo alikwidwa na vijana hao na kuondoshwa katika eneo la kujiandikishia na kuonywa kutokuwa na kimbele mbele juu ya mambo ambayo yanagusa maslahi ya watu wengi katika visiwa hivyo.
Sakata hilo liliendelea kwa muda mfupi ambapo baadaye vikosi vya askari polisi na wale wa KMKM walisogea maeneo hayo na kuwataka vijana ambao hawana sifa ya kujiandikisha waondoke karibu na vituo vya kuandikisha wapiga kura hali ambayo ilitiiwa na vijana hao na kuamua kukaa umbali wa mita 200 kutoka katika vituo vya kuandikisha wapiga kura.
Nilishawishika kuwafuata vijana katika kundi hilo waliloketi chini ya mbuyu ili kujua nini kilichokuwa kikiendelea baina yao na sakata lililotokea muda mfupi, nikakutana na maneno ya bezo na kebehi za kila aina kutoka kwa kila mmoja aliyekuwepo pale;’’mwingine akisema kuwa sisi tumeambiwa kadi zimeisha, lakini wengine wanaendelea kupewa!!! na mwingine akisema watueleze ukweli kama sisi ni wakimbizi katika nchi yetu’’.
Tafsiri halisi ya maneno ya vijana hao ilionekana kuwa kama vile wamenyimwa haki yao ya msingi ya kujiandikisha ilhali ni wenyeji na wazawa wa visiwa hivyo lakini kuna taratibu ambazo zinakinzana juu ya wao kupata vitambulisho vya ukaazi ambapo pia vijana hao ambao wengi wao ni wapiga kura katika uchaguzi wa mwaka 2000 na 2005 wameonekana kuwa wamepoteza sifa ya kupiga kura kwa awamu hii hadi wapate vitambulisho vya ukaazi.
Vijana hao walionekana wakihoji uhalali wa mkaazi kuwa na haki ya kujiandikisha na uharamu wa raia kukosa sifa ya kuwa mpiga kura na kuibua hisia tata ndani ya sheria baina ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ZEC ambayo tafsiri halisi ya uhalali na uharamu ya uandikishwaji katika daftari ka kudumu ndio hasa kinachoonekana kugombewa na wanasiasa.
Mtazamo wa watu wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa CUF ni hoja ipi inayopaswa kufuatwa na kutekelezwa katika mchakato wa uandikishwaji ilhali fikra zilizopo baina yao ikiwa ni dhuluma na hujuma za uandikishwaji kwa kile kilichosemwa kuwa ni kupunguza idadi ya wapiga kura wanaoshabikia upande wa upinzani visiwani humo.
Mgongano unaoshabihi kauli hizi unakuja kwa tafsiri yakinifu inayohusu aina hii ya uandikishwaji huku kukiwa na pande mbili za Muungano ile ya Tanzania Visiwani na ile ya bara, huku upande mmoja ukilazimika kupigia kura nne za rais wa Muungano, rais wa Serikali ya Mapinduzi, Wabunge na wawakilishi ilhali upande mmoja ukiwa na nafasi ya kuwapigia rais wa Muungano na wabunge pekee.
Sifa ya kuwa mkaazi inatajwa kuwa anatakiwa kuishi bila kuhama sehemu moja kwa kipindi kisichopungua miaka mitano na ndipo anapokuwa na sifa ya kuwa mpiga kura, sheria ambayo iko upande mmoja tu wa Muungano huku kukiwa na tafsiri kwamba Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano...napata kigugumizi hapa nini kinajificha nyuma yake.
Zipo nchi za Ughaibuni ambazo zinakaribisha wageni kutoka nchi nyingine ambazo baadaye wageni hao hupata sifa ya kuwa wakaazi lakini si raia ambapo sifa hiyo ya ukaazi hukoma mara anapoamua kurejea nchini kwake ama kukiuka taratibu za kuishi katika nchi husika na hivyo kukosa sifa kuendelea kuwa mkazi wa nchi hiyo.
Pia tumeshuhudia raia wa nchi kadhaa waliopo nchini mwetu ambao hupewa haki ya kuwapigia kura viongozi wao walioko nchini mwao huku wakiwa hawako nchini mwao kwa miaka zaidi ya 20 jambo ambalo kwa visiwa vya Unguja na Pemba halina nafasi kwa Mpemba anayefanyabiashara zake Dar es salaam au yule aliyepo nje ya nchi.
‘’Kwa nini tunanyimwa haki yetu ya uraia tunawekewa vikwazo na mifano mingi ya kutukwamisha, mimi nimezaliwa hapa, nimekulia hapa, baba na babu yangu wote nimewazika hapa naambiwa sina haki ya kujiandikisha na sasa nina umri wa miaka 40 nini kimejificha nyuma ya pazia,’’anasema Bw.Hamis Ali Hamis mkazi wa Fukuchani.
Anasema jambo ambalo ni la ajabu na kushangaza ni kitendo cha Masheha kupita nyumba kwa nyumba kuulizia wanachama wa chama cha Mapinduzi CCM na kwamba wanapowakuta wanachama wao huwapa fomu za kujaza kwa nia ya kujiandikisha na kupata vitambulisho vya ukaazi ambapo kwa upande wa watu ambao si wanachama wa CCM wanakosa fursa hiyo.
Nilikuwa na maswali mengi ya kujiuliza pasipo majibu na kutafakari kilicho nyuma ya pazia juu ya zoezi hili la uhakiki na uandikishwaji wapiga kura kuwa na kasoro katika visiwa vya Zanzibar pekee huku katika mikoa ya bara ambako pia kulikuwa na zoezi la aina hii hakukuwa na matatizo kama haya.
Nilizidi kuumiza kichwa changu na kuzidi kutafakari namna ambavyo nguvu kubwa ya dola ilivyoelekezwa katika zoezi la uandikishaji visiwani humo kiasi cha kuathiri mali, uchumi na hata kuleta madhara kwa wananchi ambao ndio walengwa wakuu wa upigaji kura mara unapowadia muda muafaka wa kufanya hivyo wakati wa uchaguzi mkuu.
Aidha nilikuna kichwa changu juu ya hatima ya visiwa hivi katika mfumo wa vyama vingi huku kila unapowadia wakati wa uchaguzi wananchi huanza kujiandaa kwa lolote ikiwemo kuwa na hofu na hatimaye kufikiria kukimbia makazi yao ambapo pia wageni kutoka nje nao hujihadhari na kuanza kuondoka visiwani humo kwa hofu ya uchaguzi unaofanyika visiwani.
Kadhalika niliinamisha kichwa changu chini kwa nia tu ya kuvuta fikra kwamba aina hii ya mfumo wa utawala kama ina nia ya kuwasaidia Watanzania kwa njia za kisiasa wenye nia ya kuleta maendeleo kwa wananchi huku wananchi hao wakizidi kujengewa hofu ya maisha kila kukicha tena kwa maslahi ya watu wachache tu wenye nia ya kujiimarisha madarakani.
Nilitafakari zaidi kuona namna ambavyo akina mama na watoto wa vizazi hivi wanavyopandikiziwa fikra za uadui baina yao na viongozi wanaoongoza nchi huku nikirejesha kumbukumbu za mauaji yaliyotokeza visiwani humo Januari 27 2001 ambapo dola ilitumia nguvu za ziada kutawanya maandamano ya wafuasi wa chama cha wananchi CUF.
Serikali inapaswa kujiuliza kwa makini hatima ya haya yanayofanyika na maslahi yake kwa jamii na nini matunda ya hiki kinachopandikizwa katika jamii ambayo ndiyo tegemeo na nguvu kazi ya Taifa ambalo ni miongoni mwa mataifa masikini zaidi kuliko mengine duniani.
Hatimaye fikra zangu zilinifikisha mbali zaidi na kudhani kuwa hakuna tena haja ya kuwepo kwa mfumo wa vyama vingi nchini ikiwa uwepo wake hauna maslahi kwa wananchi bali ni hofu na mashaka na zaidi ya yote kukithiri kwa umaskini kutokana na kukosekana kwa huduma za kijamii kwa maeneo ambayo hayaungi mkono chama kinachotawala.
Nikaendelea kuumiza zaidi kichwa changu na kujiuliza nini hasa sababu ya hofu hii kwa watawala kutumia nguvu kubwa ya dola katika maeneo ambayo chama tawala hakikubaliki?kwamba ni hofu ya kuondoka madarakani na hisia za watawala wapya kulipiza kisasi kwa maovu yao?au ni kuzoea tu kuwepo madarakani na hakuna kazi nyingine ya kuifanya zaidi ya siasa? Maswali mengi niliyokuwa nayo hayakuwa na majibu ya mara moja kichwani mwangu.
Niliamua kuachana na fikra hizo na kuendelea na safari yangu ya kutembelea vituo vya kuandikishwa wapiga kura hadi Shehia ya Bwereu ambacho ni kituo kilichopo katika skuli ya Fukuchani, huko nilikutana na malalamiko ya wakazi wa Shehia hiyo yanayolingana na yale niliyoyasikia katika kituo cha Fukuchani.
Lakini hapa kulikuwa na tatizo la watu kukamatwa ambapo mtu na mwanaye waliofahamika kwa majina ya Bw. Makame Mcha na Ali Makame Mcha ambao wote walikamatwa na askari polisi kwa kile kilichoelezwa kuhoji kwa jazba sababu za wafuasi wa CCM kupewa vitambulisho na wao kunyimwa haki hiyo.
Katika kituo cha Shehia ya Nungwi iliyopo Wilaya ya Kaskazini 'A' nilipata jambo jingine ambapo hapa liliongezeka jambo moja mbali na malalamiko ya wakazi hao, kwamba wakati zoezi hili linaanza asubuhi kulikuwa na mzozo wa kuuliza sababu za wengine kunyimwa haki ya kujiandikisha ilhali wanazo sifa na hivyo kufikia hatua ya baadhi yao kukamatwa na askari polisi.
Waliokamatwa katika kituo hicho walikuwa ni watu wanne ambao ni Bw. Ame Mtwana Juma na mwanaye Bi Suluma Ame Mtwana,Bw. Ali Jafar Haji na Bi. Hadiya Neema Hamid ambao wote walionekana kuwa ni wafuasi wa chama cha wananchi CUF kutoka katika Shehia ya Nungwi.
Katika jumla ya malalamiko yaliyotolewa na wakazi hao ni hoja za kuhitaji ufafanuzi wa wengine kupewa vitambulisho na wengine kunyimwa kama ilivyoelezwa na Katibu wa wilaya wa chama cha wananchi CUF wilaya ya Kaskazini A Bw.Khamis Abbas ambaye alisema kuwa wao waliomba vitambulisho walinyimwa ilhali wenzao wa CCM walipewa bila vikwazo.
Nilipata fursa ya kuzungumza na mmoja wa wananchi wa maeneo hayo aliyejitambulisha kwa jina la Makame Adibu Pesa ambaye yeye kwa upande wake anasema kuwa alipata kupiga kura mwaka 2005 na ana kitambulisho alichopigia kura wakati huo na kuhoji sababu za msingi za kunyimwa haki hiyo mwaka huu huku akiwa ni miongoni mwa wananchi waliopiga kura katika uchaguzi mkuu uliopita.
Jambo moja ambalo lilinishangaza ni kutolewa kwa malalamiko kwa wananchi ambao kila mmoja akionekana kuwa ni mfuasi wa chama cha wananchi CUF huku kukiwa hakuna dalili za malalamiko kwa wafuasi wa chama cha Mapinduzi CCM hali ambayo ilinifanya nizidi kubaki njia panda na kuhisi kwamba huenda kinachozungumzwa na wananchi hawa kina ukweli ndani yake.
Nilipata hisia hizo kutokana na ukweli kuwa inawezekana wafuasi wa CCM huandikishwa kupitia kwa Masheha kama ilivyoelezwa na wafuasi wa CUF ambapo pia wananchi hao walidai kuwa utaratibu unaotumika kuwajua kuwa huyu ni mfuasi wa CCM na huyu ni mfuasi wa CUF ni aina ya mihuri inayogongwa katika barua zinazotolewa kuidhinisha kupatiwa vitambulisho vya ukaazi.
Hisia hizo zilijikita zaidi baada ya kuona hakuna mfuasi hata mmoja wa chama cha Mapinduzi anayejitokeza kutoa malalamiko ya kunyimwa kuandikishwa bali kila mmoja anayelalamika hujitaja kuwa yeye ni mfuasi wa chama cha Wananchi CUF.
Bw. Mwevula Kheri Haji na wenzake katika Shehia ya Fukuchani wanasema kuwa wanapokwenda kwa Sheha kupata fomu ya kuidhinishwa kupata vitambulisho vya ukaazi, hugongwa muhuri wa kuwatambulisha ambapo mfuasi wa CCM hugongewa muhuri mara moja na yule mfuasi wa CUF hugongewa muhuri mara mbili.
Wanasema kuwa hali hiyo huwatambulisha watu wa vitambulisho kuwa mwenye mihuri iliyogongwa mara mbili si mtu anayepaswa kupewa kitambulisho kwa kuwa si mfuasi wa CCM na yule ambaye muhuri wake umegongwa mara moja ndiye mtu anayepaswa kupewa kitambulisho kwa kuwa ni mtu wao.
Jambo hili lilizidi kunipa utata katika fikra zangu ambapo pamoja na waandishi wa vyombo vingine tulilazimika kuwauliza wahusika wakuu wa uandikishwaji wa daftari hilo kama kuna aina hii ya hujuma kwa kukutana na Sheha wa Shehia ya Nungwi Bw.Kombo Ali Mkuni ambaye anasema kuwa hakuna aina hiyo ya hujuma kwa fomu za kuwatambulisha watu wanaoandikishwa katika daftari la kudumu.
''Si kweli kwamba kuna mihuri miwili inagongwa katika fomu...inawezekana kuwa makosa yaliyofanyika lakini si kwa ajili ya kuhujumu wafuasi wa chama kingine, anasema Bw. Mkuni.
Hata hivyo aina hiyo ya fomu ambazo zimegongwa mihuri miwili zilionekana kwa wananchi wengi wa maeneo hayo kiasi cha kuhisi kwamba huenda kuna ukweli wa madai yao na kulazimika kumtafuta Mkuu wa kituo cha uandikishwaji Bw.Jabir Haj ili aelezee hali hiyo ambapo naye kama Bw. Mkuni anaelezea kuwa hakuna hali kama hiyo katika zoezi ka uandikshwaji wa daftari la kudumu.....(0713310096)...INAENDELEA..
WANANCHI na wakazi wa maeneo haya walikuwa na malalamiko yao juu ya fomu ya uandikishwaji ambapo fomu hizo zilizogongwa mihuri miwili zilionekana kwa wananchi wengi katika maeneo haya kiasi cha kuhisi kwamba huenda upo ukweli juu ya utata huu ambao wananchi wanaonesha kulalamikia kwa nguvu kubwa.
Ili kuupata ukweli na kujiridhisha juu ya madai haya nililazimika kumtafuta Mkuu wa kituo cha uandikishwaji cha Nungwi Bw.Jabir Haji ambaye alielezea hali hiyo kama vile ilivyoelezwa na Sheha wa Nungwi Bw.Kombo Mkuni Ali kuwa hakuna hali kama hiyo katika uandikishwaji wa daftari la kudumu na hivyo kuzidi kuibua utata juu ya dosari zilizopo kwa uandikishwaji visiwani Zanzibar.
Siku ya pili ya uandikishwaji wa daftari hilo ilianza kwa kugubikwa na matukio ya kutatanisha huku upande wa visiwa vya Pemba hali ikiwa tete zaidi ambapo jimbo la Ole lililopo mkoa wa kaskazini Pemba kundi la watu wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa chama cha Wananchi CUF lilionekana likizidi kuyatahadharisha makundi ya wafuasi wachache waliokuwa na nia ya kutaka kujiandikisha.
Jimbo la Ole kwa mujibu wa maelezo ya Mbunge wake kwa tiketi ya CUF Bw.Bakari Shamisi Faki ni kwamba kuna jumla ya wazee pamoja na vijana wapatao 3000 ambao hawana vitambulisho na kwamba wamekuwa wakivifuatilia vitambulisho hivyo kwa muda mrefu bila mafanikio na hivyo kuleta dhana kwamba kuna hujuma ya kuwazuia wasipate fursa ya kujiandikisha.
Hali hiyo ilisababisha kundi la watu wanaodaiwa kuwa ni wanachama wa CUF kuzuia wengine wanaotaka kwenda kujiandikisha hadi hapo raia wote wa Zanzibar watakapopewa haki ya kujiandikisha katika daftari la kudumu pasipokuwa na masharti na hivyo kupata ridhaa ya kuwa wapiga kura kama walivyopata ridhaa hiyo mwaka 2000 na 2005.
Takribani wakazi wote ambao kwa kipindi hiki wamedaiwa kukosa sifa za kuwemo katika daftari la kudumu ni wale waliojiandikisha na kupiga kura mwaka 2000 na wengine mwaka 2005.Nilipata fursa ya kulijua hili baada ya kuona kadi za kupigia kura za baadhi ya wananchi ambapo mmoja niliyezungumza naye alinionesha kadi aliyoitumia kupigia kura mwaka 2005.
‘’Unaona tunanyimwa vipande vya ukaazi ilhali tumepiga kura tangu uchaguzi uliopita katika mfumo wa vyama vingi uanzishwe,’’anasema Bw. Salum Mohamed Salum(30) mkazi wa Shehia ya Nungwi.
Anasema wapo wengi wanaozidi miaka 18 wananyimwa kuandikishwa katika daftari la kudumu ilimradi ajulikane kuwa ni mfuasi wa chama cha upinzani na kudai kuwa wale wafuasi wanaoonekana wana dalili za kuwa ni wafuasi wa CCM hata kama wana kila dalili za kuwa chini ya miaka 18 walilazimishwa chini ya usimamizi wa Masheha kwenda kujiandikisha kwenye daftari la kudumu.
Siku ya pili ya uandikishaji kituo kilichopo katika skuli ya Kilindi katika Shehia ya Kilindi ni mtu mmoja tu aliyekuwa amejiandikisha kama anavyoeleza mkuu wa kituo hicho Bw.Shahar Mussa Makame ambaye anasema kuwa makundi ya watu wote waliojitokeza hawakuwa na sifa ya kukidhi masharti ya kuwa na kitambulisho cha ukaazi.
‘’Kila aliyekuja kituoni hakuwa na sifa ya kuandikishwa, tumewaeleza waende katika Shehia zao ili wapewe fomu za kuthibitishwa kuwa ni wakazi wa maeneo hayo,’’anasema Bw. Makame.
Kwa upande wake msimamizi wa tume ya uchaguzi Zanzibar ZEC katika kituo cha skuli ya Kilindi Maalim Khamis Mussa anasema kuwa makundi ya watu ambao wamejitokeza katika uandikishaji wa daftari la kudumu ni wa muda mrefu na kwamba tume imeanza kutangaza kwa kutoa taarifa juu ya watu kujitokeza, ambapo ulitolewa muda wa kutosha lakini hakuna aliyejitokeza hadi dakika za mwisho.
Aidha Bw. Mussa anakanusha tume ya uchaguzi Zanzibar kuhusika na suala la vitambulisho vya ukaazi na kudai kuwa suala hilo linasimamiwa na ofisi ya vitambulisho iliyopo eneo la Gamba kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya ya Kaskazini A.
‘’Tulitoa muda wa kutosha kwa uandikishaji na kutoa semina kwa wananchi wote kujitokeza kuandikisha….vijana wengi walipuuzia hivi sasa ndio wanaona umuhimu wa kujitokeza mapema kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura,’’anasema Bw.Mussa.
Naye Sheha wa Kilindi Bw.Omar Ali Kheri anakanusha Shehia yake kuhusika katika utoaji wa fomu kwa kubagua itikadi za vyama na kudai kuwa iwapo yeye binafsi atathibitika kuhusika kwa namna moja ama nyingine kuhujumu uandikishwaji wa daftari la kudumu atawajibika.
Takribani kila kituo cha uandikishaji kulikuwa na mawakala wawili au watatu wa vyama vya siasa ambapo asilimia kubwa walikuwa ni mawakala wa vyama viwili vya CCM na CUF na vituo vichache vilikuwa na mawakala wa vyama vingine tofauti na CCM na CUF ambavyo ni UPDP na Sauti ya Umma (SAU).
Uandikishaji wa daftari la kudumu uliendelea kusuasua huku kukiwa na matukio ya hapa na pale ikiwemo kuongezeka kwa askari katika vituo vya uandikishwaji na baadhi ya vijana na wananchi wengine wakijenga hofu kusogelea katika vituo vya uandikishaji kutokana na wingi wa askari waliop[o vituoni humo.
Akizungumzia hali hiyo Kamanda wa polisi wa mkoa wa Kaskazini Unguja Bw.Mselemu Masuod Mtulya ambaye naye alikuwa miongoni mwa watu waliotembelea vituoni kuhakikisha hali ya usalama inadumishwa anasema kuwa jeshi la polisi limelazimika kutuma askari wengi katika vituo vya uandikishaji kwa makusudi ili kudhibiti uhalifu unaoweza kutokea na kwamba limeamua kujipanga kwa hali yoyote kwa nia ya kukabiliana na uvunjifu wowote wa amani unaoweza kujitokeza.
Mwandishi: Kamanda wa polisi wa mkoa wa Kaskazini Unguja unaweza kutueleza sababu za kuwepo kwa idadi kubwa ya askari polisi katika eneo la uandikishaji upigaji Kura?
Kamanda Mtulya:Naam! tumelazimika kufanya hivyo kudhibiti aina yoyote ya uhalifu inayoweza kutokea wakati wa uandikishaji wa daftari la kudumu la wapigaji kura.
Mwandishi:Huoni kama hali hii inawajengea hofu baadhi ya watu wanaostahili kujiandikisha kusogea katika eneo hili,…kwani ni jambo gani lililowapa hofu hadi mkalazimika kutuma kundi kubwa la askari wa kutuliza ghasia katika vituo vya kuandikishia wapiga kura?
Kamanda Mtulya:Mtu yoyote mwenye haki ya kujiandikisha hapaswi kujenga hofu sisi tupo kwa ajili ya kulinda amani na utulivu na usalama waweze kujiandikisha kwa amani na utulivu, yapo makundi ya vijana wasio na sifa ya kujiandikisha wamejitokeza kwa nia ya kufanya vurugu na kuzuia wengine kujiandikisha…kama jeshi la polisi lazima tujihadhari mapema.
‘’Tunayo nguvu kubwa ya kudhibiti hali hii…ikilazimika kutumia silaha za moto tutafanya hivyo…tunao uwezo wa kufanya hivyo inapobidi,tunawaonya wote waliolenga kuvuruga uandikishaji….tutapambana nao kwa nguvu zote,’’anaongeza kusema Bw.Mtulya.
Mwandishi:Kwa nini hasa muamue kutumia silaha za moto katika uandikishaji, mnadhani hiyo ndiyo suluhu ya matatizo au ni kuzidi kujenga chuki baina ya dola na wanasiasa?...na wale ni vijana wamejikusanya wanalalamika kunyimwa hakii yao ya kujiandikisha katika daftari la ukaazi?
Kamanda Mtulya:Lile ndio kundi la vijana wanaofanya vurugu kuwazuia wengine wasijiandikishe na hiyo ndiyo hali ambayo tumekuja kuikabili katika vituo vyote vya uandikishaji wa daftari la wapiga kura...tutahakikisha tunakomesha hali hii kwa nguvu zote na hata ikiwezekana kutumia nguvu ya akiba na silaha za moto tutafanya hivyo.
Kulingana na mazungumzo na Kamanda wa polisi wa mkoa Kaskazini Unguja Bw.Mtulya inaonesha dhahiri kuwa jeshi la polisi limejipanga kukabiliana na hali yoyote ya vurugu ambayo inaweza kutokea katika vituo vya kujiandikisha, lakini hali hii iko tofauti kwa upande mmoja wa shilingi ambapo wale waliokosa fursa ya kujiandikisha wanadai kuwa kuna hujuma za kisiasa zinafanya dhidi yao.
Hisia za chuki dhidi ya viongozi wa uandikishaji na Tume ya uchaguzi zilianza kuonekana dhahiri katika nyuso za vijana ambao walionekana wakiwa wamekaa katika vikundi vikundi kwenye maeneo mbalimbali ya vituo vya uandikishaji.
Kisiwani Pemba katika jimbo la Ole hali ilikuwa tete zaidi baada ya nyumba ya Sheha kudaiwa kuchomwa moto na watu wasiojulikana usiku wa siku moja wa mwanzo wa uandikishaji na kuwa mwanzo wa mtafaruku baina ya wafuasi wa CUF ambao kwa yakini walikuwa wakiwashinikiza wenzao wa CCM kutojiandikisha hadi hapo raia wote watakapokubaliwa kujiandikisha.
Mtafaruku huo ulizidi kupamba moto zaidi Septemba 14 asubuhi ambapo vikosi vya askari polisi wa kutuliza ghasia na wale wa KMKM walionekana wakivinjari katika mitaa ya kisiwani Pemba katika jimbo la Ole wakipita nyumba hadi nyumba kuwataka wananchi wajitokeze kujiandikisha katika daftari la kudumu.
Zoezi hilo la askari polisi na wale kikosi cha KMKM lilipokelewa kwa mtazamo hasi na wananchi wengfi visiwani humo ambapo walionesha dhahiri kugoma kujitokeza kuandikisha na kufanya vituo vya uandikishaji viendelee kubaki vitupu hatua iliyofanya askari hao huku wakiwa na kipaza sauti wakipita nyumba hadci nyumba kuwataka wananchi wajitokeze.
Hali hiyo ya askari kuvinjari mitaani wakiwa na silaha za moto na mabomu ya machozi ilikuwa kama imerejesha kumbukumbu za shari kisiwani humo kutokana na matukio yaliyopata kutokea wakati wa maandamano ya wafuasi wa CUF mwaka 2001 iliyosababisha baadhi ya wafuasi wa chama hicho kuuawa na wengine kukimbilia Shimoni ,Mombasa nchini Kenya.
Dalili hizo zilianza kuonekana kwa vijana hao ambapo wakati askari polisi wakirusha mabomu ya machozi na maji ya kuwasha mwilini wakiwataka wananchi hao kutoka katika majumba yao ,vijana hao walisikika wakisema….tuueni kama mlivyowaua wenzetu mwaka 2001…hatuogopi kufa kwa kudai haki!!!Sawa kwa wote!!!
Ilikuwa kama mchezo wa kuigiza vile ghafla mabomu yalianza kuvurumishwa hewani na silaha za moto na gari la maji ya kuwasha yakawa yanarushwa kwa watu na kuzusha tafrani kubwa miongoni mwa wakazi wa visiwa hivi hususani kwa akina mama wajawazito,wazee vikongwe na watoto wadogo ambao walianza kukimbia makazi yao na kuelekea vichakani.
Mtafaruku huo ulisababibisha watu watano wakazi wa Shehia ya Sizini,Mjini Kiuyu na Shumbu ya Vyamboni wakiwemo akina mama na watoto kulazwa katika hospitali ya wilaya yaWete baada ya kudhuriwa na mabomu ya machozi na maji ya kuwasha ambayo yalikuwa yakirushwa na magari ya askari mitaani bila kujali aina ya watu waliopo.
Wakiwa chini ya usimamizi wa Mkuu wa mkoa wa Kaskazini Pemba Bw. Dadi Faki Dadi na Kamanda wa polisi mkoa wa Kaskazini Pemba Bw. Yahya Buki askari hao walizama katika mitaa kadhaa ya mjini Pemba wakiwa na silaha zao na kujenga hofu kwa wananchi kutoka nyuma ya nyumba zao na kukimbilia ufukweni mwa bahari na wengine kukimbilia katika mji wa Shumbu ya Mjini wilaya ya Micheweni kunusuru maisha yao.
Uendeshaji wa zoezi hilo la kulazimisha wananchi wa maeneo ya Sizini kwenda kujiandikisha katika daftari la kudumu ilisababisha madhara baada nyumba mbili za wakazi wa maeneo hayo kuangukiwa na bomu na kuteketea kwa moto hali iliyozidi kuleta hofu kwa wakazi wa visiwa hivyo.
Uhakiki huo wa daftari la kudumu kisiwani Pemba ulisababisha watu waliochomewa nyumba kwa mabomu ya polisi kushikiliwa kwa kile kilichoelezwa kuwa walikuwa ni miongoni mwa watu waliohamasisha kufanyika vurugu na kuzuia watu kujitokeza kujiandikisha.
Akizungumza katika eneo la tukio Mbunge wa jimbo la Micheweni Bw. Shoka Hamis Shoka anasema kuwa vurugu hizo zimetokana na askari polisi kupita nyumba hadi nyumba kulazimisha wakazi hao kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapoiga kura kutokana na wakazi wengi wa visiwa kususia uandikishaji baada ya baadhi yao kudaiwa kukosa sifa ya kuandikishwa.
Katika hali ambayo kama ilionesha kuwa jambo hili lilikuwa linafahamika matokeo yake kabla serikali ya Marekani kupitia ubalozi wake ilitoa tamko la kuwataka wamarekani waliopo visiwani kuanza kurejea makwao kwa kile kilichosemwa kuwa kuna hali ya hatari iko visiwani humo.
Hali hiyo ilionesha kutiiwa na baadhi ya watalii kutoka nchini ,Marekani ambapo tofauti ya jiografia na desturi ya wakati ambao ni kipindi cha “High Season“ watalii walionekana wakifungasha virago na kutafuta mwelekeo kwa ajili ya kuondoka kurejea makwao hususani kutoka katika maeneo mbalimbali ya vivutio vya kitalii visiwani humo.
Maeneo mbalimbali ya vivutio vya utalii yaliyoathirika kwa kupungukiwa na wageni ni kutoka katika Shehia za Nungwi,Mkwajuni,Matemwe,Tumbatu,Donge na Mkokotoni vilivyopo wilaya ya Kaskazini A, maeneo ya Mchangani,Uroa na Chwaka yaliyopo wilaya ya Kati na maeneo mengine ya vivutio vya kitalii kama vile Bwejuu,Paje,Jambiani,Muyuni,Kizimkazi na Makunduchi yaliyopo wilaya ya Kusini.
Hali hiyo pia ilidhihirika katika jumba maarufu la historia na makumbusho ambalo historia yake imeenea duniani kote la Beit El Ajab ambako idadi ya watalii waliokuwa wakifika hapo ilipungua kwa kiasi kikubwa kutoka watalii 50 hadi watano kwa siku na hivyo kuchangia kuathiri kwa uchumi visiwani humo.
Aidha Septemba 14 mbali na askari wa FFU na wale wa JKU kurusha mabomu na kuchoma nyumba katika Shehia za Sizini,Shumba ya Vyamboni na Mjini Kiuyu,wilaya ya Kaskazini A mkoa wa Kaskazini Unguja katika shehia ya Mwange watu wasiofahamika walipakaza vinyesi milango na madirisha na upupu ambapo pia meza na viti na ukumbi mzima ulipakazwa upupu.
Hali hiyo ilidhihirika wakati wa alfajiri wakati mawakala wa vyama vya siasa alipofika kituoni hapo kwa nia ya kuanza maandalizi ya kuandikisha na hivyo kujikuta wakishindwa kufanikisha vyema kazi hiyo kwa kujikuna mwilini ambapo kwa mujibu wa Sheha wa Shehia ya Mwange Bw.Makame Khamis Ali alisema hali hiyo ilijitokeza baada ya baadhi ya vijana kuzuiwa kujiandikisha katika daftari la kudumu.
TAMATI........inaendelea.....
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment