Vurugu za wafanyabiashara wadogo maarufu kama wamachinga zilizotawala kwa takribani siku mbili ambao walikuwa wakipambana na vikosi vya askari polisi kutoka mikoa mitatu ya Nyanda za Juu kusini wakishirilkiana na askari wa Jeshi la Kujenga Taifa JKT zilizimwa na Mbunge wa Mbeya mjini Joseph Mbilinyi maarufu kwa jina la Sugu.
Sugu ambaye alikuwa akihudhuria Bunge mjini Dodoma alisafiri usiku kucha na kufika Jijini Mbeya ambako moja kwa moja alipitiliza ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Bw. Abbas Kandoro ambako walizungumzia ghasia hizo ambazo zilionekana zina dalili ya kuwa na mkono wa kisiasa.
Katika ghasia hizo ambazo zilianza jana asubuhi kulikuwa na mabango yaliyokuwa yakisomeka kuwa MBEYA NI NCHI...SUGU NI RAIS, HATUMTAKI KANDORO!!!
Akizungumza katika mkutano wa hadhara eneo la Kabwe Jijini Mbeya Sugu alisema kuwa kuna amakubaliano yamefikiwa baina yake na viongozi wa Mkoa na wale wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya kuwa wamachinga hao wataendelea na biashara zao hadi hapo watakapotafutiwa eneo maalumu la kufanyia biashara.
Sugu ambaye hotuba yake ilikuwa ikikatishwa mara kadhaa na mayowe ya wananchi waliokuwa wakimshangilia alisema kuwa Halmashauri ya Jiji inajiandaa kuja na mikakati mipya itakayokubaliwa na pande zote juu ya uboreshaji wa maeneo ya biashara ya wamachinga jijini humo.
Aidha alisema kuwa wamekubaliana kuwaachia watu wote waliokamatwa kufuatia ghasia hizo tangu jana na leo ikiwa ni pamoja na kuwaondoa askari wote wanaozagaa mitaani ili kuepusha hofu miongoni mwa wananchi na kuwaacha waendelee na shughuli za uzalishaji mali.
Pia alikanusha vikali kuwa yeye ni Rais wa Mbeya na kusema kuwa Tanzania ina rais mmoja tu ambaye ni Jakaya Kikwete na kuongeza kuwa anaamini kuwa matatizo yaliyotokea dhidi ya wamachinga hayatajirudia tena na iwapo yatajirudia yeye ataungana nao kuingia mitaani.
Hata hivyo aliwasihi wamachinga kutoendeleza vurugu bali waendelee na shughuli zao kama kawaida kutokana na kumalizika kwa mgogoro huo ulioutikisa mkoa wa Mbeya na Taifa kwa ujumla.
Sugu aliwashukuru wamachinga hao kwa kuendesha harakati zao bila kufanya uporaji wa mali za watu na kuonesha kuwa harakati hizo zililenga kutoa ujumbe bali si kupora mali za watu.
Katika Mkutano huo, Sugu aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Bw.Evance Balama ambaye alishindwa kuhutubia mkutano huo baada ya wananchi kumzomea kwa madai kuwa alishindwa lkuwasaidia wakato tatizo hilo likiwa bichi.
Wananchi hao walipaaza sauti ya kumtaka aondoke jukwaani na kusema kuwa hawamtaki na kumwachia SUGU aendelee kuzungumza na wapiga kura wake.
Jitihada za Jeshi la Polisi, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Jeshi la Wananchi (JWTZ) kupambana na wamachinga ili kuzuia vurugu hizo ziligonga mwamba kwa siku mbili mfululizo, na wakati wamachinga wakipambana, muda wote walikuwa wakiimba nyimbo za kumkataa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro.
Kufuatia vurugu hizo watu zaidi ya 235 wanashikiliwa na jeshi la Polisi huku 17 wakiwa wamejeruhiwa kutokana na kurupushani hizo na wengine 7 kujeruhiwa kwa risasi huku mmoja kati yao akiwa amepoteza maisha.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Mbeya Bw. Abbas Kandoro ambaye wakati ghasia hizo zinaanza alikuwa katika ziara wilayani Mbozi na kulazimika kukatisha ziara alisema vurugu hizo zina dalili ya kuwa na shinikizo la watu fulani na kuwa na maandalizi ya muda mrefu kutokana na kuwepo kwa mawe makubwa yaliyowekwa katikati ya barabara ambayo hajawahi kuyaona.
Aliongeza kuwa katika vurugu hizo vijana walikuwa wakimtaja kuwa sugu ni rais jambo ambalo ni uhaini na kumuharibia Mbunge Sugu kwani hata yeye hawezi kujiita rais kwani rais ni Jakaya Mrisho ambaye amewekwa kwa kura ya wananchi.
STORI KWA HISANI YA MDAU DOTTO MWAIBALE
Poleni sana wakazi wote wa Mbeya kwa sintofahamu iliyoukumba mkoa wetu. Pia natoa Pole kwa Mkuu wa mkoa Mh. Kandolo, Mh Joseph Mbilinyi (Mb), RPC, Mkurugenzi, DC na Meya Mzee wangu na Mlezi wangu kichama Mzee Kapunga na wadau wote.
ReplyDeleteKwa ujumla wenu nawapongeza kwa juhudi zote mlizofanya mpaka hapo mlipofikia hatimae kurejesha mji katika hali yake ya kawaida ya amani na utulivu.
Pia natumia nafasi hii kumtoa wasiwasi Mkuu wetu wa mkoa Mh. Kandoro kwamba kilichotokea ni upepo mbaya tu, na maadamu tumefunika kombe ninaamini mwana haramu amepita. Si tabia ya wana mbeya na wala hatupo hivyo, kama nilivyosema hapo awali ni upepo mbaya tu. Karibu sana mkoani kwetu tusukume gurudumu la maendeleo.
Mtazamo wangu juu ya swala hili unanipeleka mbali na kunifanya nifike mahali ambapo
najaribu kufanya rejea ya walimu wangu walionifundisha shule ya msingi, sekondari na chuo hasa wa somo la fizikia.
Kuna mada moja iitwayo NISHATI au Energy kwa lugha ya Waliochanganyikiwa (Waingereza). Kanuni ya nishati(law of conservation of energy) inatamka hivi; energy can neither be created (produced) nor destroyed by itself. lakini hawakuishia hapo pia inatamka hivi: It can only be transformed.
Nachotaka kusema ni kwamba kila action huwa ina reaction. Najua bado sijaelweka lakini nitaeleweka tu. Nikiwa bado katika somo la fizikia, nadiriki kusema kama isingelikuwa kiburi na ubishi wa maji kukataa kukandamizwa Katu meli isingelielea. wale wenzangu na mimi huwa kuna kitu tunaita "Upthrust" inatajwa na Bwana Archimedes(Mwanasayansi aliyefanya utafi juu ya kitu kuelea juu ya maji) kwamba Upthrust ni nguvu inayopingana mkandamizo wa kitu kinachoelea juu ya majia.
Kwa hapa nilipofikia napenda kuwafananisha raia na Maji ya bahari halafu Dola niifananishe sawa na Meli kubwa lililosheheni kila kitu likiwa linaelea juu ya maji kuangalia usalama wa bahari.
Kama nilivyoandika mwanzoni kabisa kuhusu NISHATI, maji pia ni NISHATI ambayo tumesema “energy can neither be created (produced) nor destroyed by itself”. Hivyo basi pamoja na Dola (Meli) kuelea juu ya Maji (Raia) na kuchanja mbuga kwenda huku na huko, haitoshi.
Dola inahitaji, ujuzi, utaalam na ufundi wa kuelea na hatimae kupata muelekeo sahihi ktk randaranda zake za kuangalia usalama wa bahari. Kabla ya kuanza kurandaranda juu ya maji Dola (Meli) wanatakiwa kufanya yafuatayo.
Kwa kutumia utaalam wao lazima wawe na taarifa sahihi juu ya hali ya bahari, kwa ujuzi wao ni lazima wajue namna ya kuikabili hali ya bahari na kwa ufundi mkubwa lazima wahakikishe safari yao inakuwa salama juu ya Maji. Kwani nijuavyo mimi Daima Maji Huzamisha Meli bila kujali ukubwa wake na ilichosheheni.
Meli ikizama si tu ni hasara kwa mwenye meli, bali hata maji huchafuliwa, pia hulaumiwa kwa kusababisha hasara. Pia tukumbuke kuwa polisi, mkuu wa wa mkoa na viongozi wengine wote ni Watanzania wenzetu na ndugu zetu tuwasaidie kwa kuwashauri ili watuongoze vema
Mbeya ni mkoa wetu, Viongozi waliopo ni wetu bila kujali itikadi za dini na vyama vyao. Hivyo basi ni vyema tushauriane, tukosoane lakini kamwe tusigombane, tusiruhusu kumwaga damu ni laana ndugu zangu. tusikaribishe laana katika mkoa wetu.
Yaliyopita si ndwele tusameheane tufungue ukurasa mpya tujenge Mkoa wetu na nchi kwa ujumla.
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Mbeya
Shadrack Mwamaso