Rais Jakaya Kikwete akiongoza umati wa waombolezaji kwenye mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Mbinga Magharibi Kapteni John Komba jana nyumbani kwa marehemu kijijini Lituhi wilayani Nyasa. |
Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa akiwa na mpambe wake mashuhuri Mwenyekiti wa CCM mkoa Shinyanga Hamis Mngeja alipowasili kwenye mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Mbinga Magharibi Kepteni Komba |
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Prof. Mark Mwandosya alipowasili kwenye mazishi ya Kapten John Komba kijijini Lituhi wilayani Nyasa jana. |
Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika Steven Wasira akiwasili msibani wakati wa mazishi ya Kapten John Komba |
Mbunge wa Songea Mjini Dkt. Emmanuel Nchimbi akiwa na Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera na Uratibu Jenister Muhagama wakati wa mazishi ya Kapten John Komba. |
Rais Jakaya Kikwete akisisitiza jambo na Spika wa Bunge Anna Makinda wakati wa mazishi ya Kapten Komba. |
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Prof Mwandosya akiweka udongo kwenye kaburi la Kapteni Komba. |
Vijana waliovalia tisheti zenye maneno Friends Of Lowasa wakivinjari huku na kule kwenye msiba wa Kapten John Komba |
Naibu Waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba akiongozwa kuketi kwenye jukwaa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera na Uratibu Jenister Muhagama wakati wa mazishi ya Kapten John Komba |
Jenister Muhagama akimpa mkono wa rambirambi mke wa marehemu Kapten Komba, Salome Komba wakati wa mazishi yake kijijini kwake Lituhi jana. |
Jeneza lililobeba mwili wa marehemu Kapten Komba likipelekwa makaburini kwa ajili ya mazishi |
Nyumba ya kudumu ya Kapteni John Komba |
Yalikuwa ni majonzi na simanzi kwa baadhi ya waombolezaji huku baadhi yao wakitumia fursa hiyo kujiwekea mazingira kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015.
Ni kama vile walijiandaa kujipatia umashuhuri wa kisiasa kupitia msiba huo, bali hisia na dhana zilizoibuka wakati wa maziko ya Kapteni John Komba(61) yalitafsiri mustakabali wao wa kisiasa katika uchaguzi mkuu ujao kwa nafasi za Ubunge na Urais.
Kapteni Komba aliyetambulika kwa msimamo wake na kutoyumba kwa maamuzi yake na kusimamia vitendo kuliko maneno amekumbukwa kwa hotuba mbalimbali zilizotolewa kwenye mazishi hayo huku viongozi wa kisiasa wakipata mwanya kuweka sawa mambo yao.
Rais Jakaya
Kikwete aliyeongozana na mkewe Mama
Salma waliongoza umati wa waombolezaji kutoka kona mbalimbali za nchi huku
wanasiasa wanaotajwa kuwania urais kwa tiketi ya CCM wakionekana kutumia fursa
hiyo kujidhihirisha kwa wananchi kwa
mbwembwe tofauti tofauti.
Kundi la Vijana
wanaosadikiwa kumuunga mkono Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa ambao
walivalia sare rasmi zenye maandishi yaliyosomeka
‘’Friends Of Lowassa’’ waliacha taharuki katika msiba huo huku wakiranda huku na kule ilhali wakidaiwa kuwasili msibani hapo na magari 6 ya kifahari yenye rangi nyeusi.
Kundi hilo
la vijana wa kike na kiume lilizagaa kila kona ya kijiji hicho kidogo kilichopo takribani
kilomita 140 kutoka Songea mjini wakati wa mazishi hayo na kuibua taharuki
miongoni mwa wakazi wa kijiji hicho.
‘’Hawa ndio
akina nani? Aliuliza mzee mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Sebastian Mapunda
mkazi wa kijijini hapo.
Mbali na
tukio hilo ujio wa Lowassa aliyewasili uwanjani hapo majira ya saa 7:30
uliwafanya vijana hao wawe makini zaidi
na kurandaranda huku na kule mithili ya walinzi wa usalama na hivyo kuongeza
mbwembwe za aina yake katika msiba huo uliohudhuriwa pia na baadhi ya wabunge
walioongozwa na Spika Anna Makinda.
Baadhi ya
wabunge waliohudhuria ni pamoja na Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Profesa Mark
Mwandosya ambaye alifika katika eneo la uwanja mapema kabla ya viongozi
wengine, huku Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu sera na Uratibu Jenister
Muhagama akionekana kinara kwa kuwakaribisha wageni mahali hapo.
Wengine
waliohudhuria ni pamoja na Naibu Waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba,Waziri wa Habari,Vijana utamaduni na Michezo Dkt. Fenella Mukangara,Waziri wa Kilimo Chakula na
Ushirika Steven Wasira,pamoja na wabunge wote kutoka mkoa wa Ruvuma.
Akizungumza
mara baada ya wakazi wa kijiji hicho kuuaga mwili wa marehemu Spika wa Bunge
Anna Makinda alisema kuwa ataendelea kumkumbuka Kapteni Komba kutokana na
umahiri wake wa kuenzi na kuhamasisha amani na utulivu wa nchi yetu ambapo
nyimbo zake zilitoa ujumbe kwa umma.
Awali akisoma
wasifu na historia ya marehemu Kaimu Katibu wa Bunge John Joel alisema kuwa
marehemu alitumikia maisha yake katika kazi za kutoa elimu kuanzia alipokuwa
Mwalimu 1977 hadi alipojiunga na Jeshi la Wananchi na kulitumikia kwa miaka 14
hatimaye kujiunga katika siasa 1992.
Alisema
marehemu ambaye ameacha mjane na watoto 11 kabla ya kifo chake
kilichosababishwa na shinikizo la damu na kisukari alikuwa ni mbunge wa jimbo
la Mbinga Magharibi tangu mwaka 2005 na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha
Mapinduzi kwa miaka 28 kuanzia mwaka 1987.
Kwa upande
wake mwakilishi wa kambi ya upinzani, Mbunge wa Lindi mjini Salum Baruani
ambaye ni mlemavu wa ngozi mbali na kuwakilisha salamu za rambirambi kutoka kwa
kambi ya upinzani alisema kuwa Kepteni Komba alikuwa ni sehemu ya mhimili wa
ulinzi dhidi ya mauaji ya Albino.
Alisema mara
zote walipokuwa kwenye matukio mbalimbali alimweleza wazi kuwa ataendelea
kusimama kidete kuwalilia Alibino na kuhakikisha jamii inatambua utu kwa
kutowafanyia unyama wenye ulemavu wa ngozi.
Mshereheshaji
wa mazishi hayo aliwaacha waombolezaji midomo wazi pale aliposoma ujumbe wa
rambirambi uliotumwa kwa barua pepe kutoka kwa Rais Mstaafu wa Malawi Bakili
Muluzi ambaye ilidaiwa ujumbe huo katumiwa Mbunge wa Songea Dkt Emmanuel
Nchimbi.
Kwa mujibu
wa mshereheshaji huyo ni kwamba Rais huyo mstaafu katuma ujumbe huo wa barua
pepe kupitia Nchimbi na kumpa pole juu ya msiba huo hali ambayo iliwafanya watu
wajiulize iweje ujumbe huo utumwe kwa mtu ambaye hana wadhifa wowote wa
kiserikali na rais Mstaafu huku ukiachwa kutumwa kwa Rais aliyepo au Mkuu wa
mkoa husika.
Tukio
jingine ambalo lilionesha kuwashangaza watu ni pale Waziri wa Kilimo Chakula na
Ushirika, Wasira ambaye alikosa kiti kutokana na kuchelewa kufika makaburini na
kuanza kuhaha huku na kule akiwasukuma watu ili aketi hadi pale Mbunge wa
Chalinze Ridhiwani Kikwete alipompisha aketi katika kiti alichokuwa amekalia
yeye.
Wasira
ambaye pia hakutajwa kuwa miongoni mwa watu watakaoweka udongo ikiwa ni ishara
ya kumuaga Kepteni Komba alijipenyeza na kujichomeka kwenye mstari na hatimaye
kufika kaburini na kuchukua udongo na kuuweka kaburini.
Waziri mkuu
mstaafu Lowassa alikuwa akitajwa mara kwa mara na mshereheshaji wa mazishi hayo
alikuwa ni kati ya watu waliofuatia kutoka kwa Rais Kikwete na Mama Salma ambapo baada ya
kurejea kwenye kiti Rais alimuinua Waziri Mwandosya na kumtaka aende kutia
udongo katika kaburi la marehemu.
Ratiba ya
mazishi hayo ambayo ilianza majira ya saa nne asubuhi ilikamilika saa 11 jioni
ambapo marehemu alizikwa kwenye makaburi yaliyopo kijijini kwake Lituhi wilayani
Nyasa mkoani Ruvuma.
Post a Comment