Ads (728x90)

Assalaam Alaykum!! Ni matarajio yangu nyote mko salama usalimini,nachukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunifikisha siku ya leo,bila kuwasahau ndugu jamaa na marafiki ambao kwa namna moja ama nyingine wamefanikisha uwepo wangu hadi leo.
Nitakuwa mja nisiye na shukurani iwapo  nitaacha kuwaombea dua wazazi wangu waliotangulia mbele ya haki ambao kwa kila hali uwepo wangu ulitokana na wao kuwepo duniani kwa kunizaa na kunilea kisha kunisomesha kwa  tabu na mashaka wakijidunduliza vijisenti vyao kidogo walivyopata kwa ujasiriamali mdogo.
Walifanya hivyo kwa nia moja tu ya kunipa mwanga wa kutambua mema na mabaya kwa kunisaidia nipate elimu ya dini na dunia.
Nilipata utambuzi wa kujua mema na mabaya kupitia elimu ya dini waliyonipatia kadhalika nilipata ujuzi wa mambo ya kidunia na kujiendeshea maisha kwa kadri Mungu alivyonijaalia, na sasa nami nimekuwa mtu mzima, nimekuwa baba, mwenye jumla ya watoto 7, wake kwa waume, Alhamdulillah.
Jambo moja adimu na adhimu kwangu ni masikitiko yangu makubwa yaliyonikumba,ambayo ni matarajio ya wengi kutamani sana kuishi duniani bali inapofikia muda wa kupungua umri wa  kuishi huufurahia na kusherehekea kwa nderemo na vifijo.
Ningekuwa na furaha na faraja iwapo ningelikuwa nimejihakikishia mizani ya mema kuliko maovu niliyoyatenda hapa duniani, nikijipima sijioni kama ni mtukufu wa kuufurahia umri wa nusu karne nilionao, Mwenyezi Mungu aendelee kuninusuru.
Aghalabu tulio wengi hufurahia tabia hii ya kimaumbile ya kuongezeka miaka na baadhi yetu tumekuwa tukiandaa  sherehe kubwa tukiadhimisha na kufurahia tukio kubwa la kihistoria katika uhai wetu, bali kinyume na walio wengi kwangu ni masikitiko makubwa.
Yapo mambo ambayo yananifanya nisikitike, jambo moja ni kuwa kadri ninapoongeza miaka ndivyo ambavyo umri wangu wa kuishi unapungua,natafakari muda wote wa miaka 50 niliyoishi jambo gani nimelifanya ambalo litaniweka katika mikono salama mbele ya Mwenyezi Mungu.
Natafakari, ndugu na jamaa nitakaowaacha duniani watarithi mwenendo gani kutoka kwangu, nitakuwa kiigizo chema ama nitakuwa mfano mbaya usiopaswa kuigwa na wengine, yote haya ni maswali yaliyojaa kichwani mwangu hata najikuta sijivunii kufikia umri huu.
 Natafakari maisha haya ambayo nimeruzukiwa hapa duniani kama yatakuwa na manufaa kwa kizazi changu ama wale wanaonizunguka,ni wangapi wamenikosea nikashindwa kuwasamehe, na wangapi niliwakosea wakashindwa kunisamehe, wangapi wananidai sijawalipa madeni yao na wangapi ninao wadai hawajanilipa?
Natafakari  mengi zaidi ya haya kwamba mimi ni msafi kwa kiwango gani hata nikaufurahia umri huu, je! chakula nilacho kina Baraka ama ni laana kwa tumbo langu? Je! kinatokana na vyanzo halali vya mapato yangu ama kuna mahala nilikula ama kuchukua cha mtu bila ridhaa yake?
Nainua mikono juu namuomba Mwenyezi Mungu anijaalie niwe na maisha mepesi na kipato ambacho kitatokana na riziki halali katika maisha niishiyo ambayo kiukweli ni magumu na sijui hatima ya maisha haya, kama yanastahili kufurahia na kuadhimishwa kama wengi wafanyavyo, natafakari nabaini ni majuto na majonzi tu kila uchao!!   
Wakati mwingine hupata riziki ambayo aidha imetoka kwa wenye mikono inayochuma chumo halali na mara nyingine hupata riziki kutoka kwa watu ambao nina mashaka nao, hata hivyo wapo wengine kwa macho yangu ya yakini naona kabisa nimefanya kazi zao halali lakini malipo yao sijui yanatokana na vyanzo vipi.
Bado natafakari  aina hii ya maisha,wapo wanaonilaumu kwa utendaji wangu wa kazi pia wapo wanaonipongeza kwa kazi nzuri, kioo changu ni jamii inayonizunguka, sijijui ila wananijua, wanayaona makosa yangu?, nikosoeni ningali hai, ili nijijue nilipokosea niwaombe radhi, msisubiri nikifa ndipo mnisimange na kuniteta kwa makosa ambayo ningeweza kujirekebisha kwayo.
Leo March 12, 2015 nimetimiza miaka 50, ni nusu karne, sikutuma maombi kwa Mwenyezi Mungu anifikishe umri huu ambao kiukweli sijivunii sana kwa kuwa sijui kiwango changu cha mema kama kinaweza kuyafuta maovu niliyowahi kutenda ikiwa nimetenda kwa bahati mbaya ama nimetenda kwa kukusudia.
Natimiza umri huu ilhali wapo kundi la watu na ndugu wanaonihusu  niliokuwa nikiwategemea wakiwa wametangulia mbele ya haki, baadhi yao hawakufikisha umri huu walitangulia, wangependa waishi na wafikie umri kama huu nilionao, Mwenyezi Mungu awarehemu, niliwapenda lakini Mungu aliwapenda zaidi.
Nililia sana hadi machozi yalikauka nilipowapoteza ndugu zangu kwa matukio mbalimbali ya kutisha na wengine wakidhulumiwa haki yao ya kuishi kwa kuuawa na wengine kwa ajali na wengine kwa maradhi mbalimbali, mimi sijui aina ya kifo changu kitakavyokuwa ni Mungu pekee ajuaye hatima yangu.
Najiuliza nitakufaje? Nimejiandaaje na kifo hicho, nitakufa usingizini ama nitakufa barabarani, ama nitakufa kwa maradhi? Yote ni maswali ambayo katu siwezi kupata majibu yake sasa.
Wapo watakaoumizwa na kifo changu wakitafakari mengi, kwamba walipenda niwe nao siku zote duniani ama walipenda ucheshi wangu na wengine walikuwa tu na mapenzi ya kibinadamu, bali watalia kwa uchungu kwa kuondokewa na kipenzi chao.
Wapo pia watakaofurahia kifo changu ijapo hawatajionesha hadharani kuwa wamefurahia, watajitokeza wakijifanya wana uchungu,wakipaza sauti za kilio huku wakigaragara chini kumbe moyoni wana lao jambo, haya ndiyo maisha ya binadamu na namna ambavyo tulivyo roho zetu.
Natimiza miaka 50 nikiwa na historia ndefu ya maisha na magumu mengi niliyopitia, ila jambo moja nililojifunza sipaswi kumpenda sana rafiki yangu kwani kuna siku anaweza kuwa adui kadhalika pia nimejifunza kuwa sipaswi kumchukia sana adui yangu kwani iko siku anaweza kuwa rafiki yangu.
Nitaendelea kuwapenda na kuwathamini enyi ndugu na marafiki zangu, sina lolote ninaloweza kuwalipa kwa wema mliowahi kunitendea bali ni Mwenyezi Mungu pekee ndiye mwenye uwezo wa kuwakirimu kutokana na wema mlionifanyia, ninawaombea kwa Mungu awajaalie mpate riziki halali na yenye manufaa
 ‘’Metimiza Hamsini, Mola amenijaalia,
Japo sioni thamani, umuri kufurahia,
Namshukuru manani,na wangu wazazi pia,
Mola amenijaalia, sasa myaka hamsini.
Sasa myaka hamsini, Mola amenijaalia,
Nimefikwa mitihani,mingi ilonipitia,
Bado ninajithamini,ngawa sijafurahia,
Mola amenijalia, sasa myaka hamsini.
Mwisho nimeufikia, shukurani naitoa,
Leo nimetimizia, myaka hamsini si mia,
Umuri umeshapea, Uzee nakimbilia

Mola amenijalia, Sasa myaka hamsini.

Post a Comment