Ads (728x90)



Mche wa mahindi ulionyauka kwa kukosa mvua eneo la Likonde Namtumbo



Mkulima Ayubu Makuti wa eneo la Migelegele Namtumbo akiangalia shamba lake la mahindi lililoathiriwa na jua baada ya kukosa mvua kwa wiki tatu

 Mkulima wa Likonde Namtumbo Omari Mangoto akiwa katika shamba lake lililoathiriwa na jua kwa kukosa mvua kwa wiki tatu.



Wakulima wakipalilia shamba lililoathiriwa na jua katika kijiji cha Migelegele Namtumbo

-Mazao yaliyopandwa yaanza kukauka
-Jua kali launguza mazao, mvua yasimama
Na Rashid Mkwinda, Namtumbo
HOFU ya kufikwa na Baa la njaa katika msimu wa mavuno wa 2017  wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma imetanda miongoni mwa wakulima baada ya jua kali linalowaka kukausha mazao yaliyopandwa ambayo yalitegemea mvua iliyotarajiwa kuanza kunyesha mwezi Novemba na Disemba msimu wa kilimo wa 2016-17.
‘’Kipindi hiki ndicho ambacho mvua hunyesha na kurutubisha mazao yaliyopo mashambani, mwaka huu mvua imegoma kabisa mazao yanakauka shambani, kuna dalili kubwa ya njaa msimu huu,’’alisema mkulima mmoja mkazi wa Namtumbo anayelima eneo yalipokuwa mashamba ya NAFCO aliyejitambulisha kwa jina la Kassim Said.
Alisema kuwa kwa kipindi cha miaka mingine wakati huu mahindi yangekuwa yamefikia urefu wa kima cha futi 4’ hadi futi 5’ na baadhi ya maeneo yangekuwa yameanza kuchanua lakini kutokana na tatizo la mvua hadi sasa mahindi yaliyoanza kuota yamekauka.
Alisema kuwa kwa mbegu za mahindi za muda  mfupi zinatumia muda wa siku 60 ambapo kwa mvua inayonyesha kuanzia mwezi Novemba sasa hivi mahindi yangekuwa yameanza kuchanua bali kwa mbegu ya kawaida inayotumia siku 90 sawa na miezi mitatu kwa sasa ingekuwa imefikia urefu wa futi 5’.
Kwa upande wake mkulima Ayubu Makuti(50) mkulima wa kijiji cha Migelegele wilaya ya Namtumbo alisema kuwa kuna dalili ya njaa mwaka huu kwa kukosa mvua kwa kuwa yeye alianza kupanda mvua za kwanza zilipoanza kunyesha lakini hadi sasa mahindi hayajafika hata urefu wa futi 1’ hali ambayo inaashiria madhara katika msimu huu wa kilimo.
‘’Tuliambiwa kuwa mvua za kwanza ni za kupandia, watu wamepanda mazao yao mapema, mvua imegoma kunyesha kinachofuatia baada ya hapa ni njaa, ukifika shambani wakati wa jua kali mahindi unayaona yakiwa yamenyauka kwa jua,’’alisema Makuti.
Naye mzee Abedi Parahane(80) mkulima wa kijiji cha Migelegele alisema kuchelewa kwa mvua kuna madhara makubwa kwa wakulima wa mazao ya mahindi, mpunga na tumbaku na iwapo haitanyesha hadi ifikapo Januari 10 mwakani wakulima wa Namtumbo watakumbwa na njaa.
‘’Tulijitahidi kuwahi kulima kama desturi yetu, tofauti na mwaka jana watu waliwahi kulima na mvua ilinyesha kwa wakati, unyeshaji wa mvua wa aina hii ni dalili ya njaa’’ alisema Mzee Ali Kilosa(78) mkazi wa kijiji cha Rwinga.
Akizungumza hivi karibuni katika mkutano wa hadhara ulioitishwa na Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dkt.Binilith Mahenge, Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Luckiness Amlima aliwataka wananchi kutouza chakula chote walichovuna msimu uliopita kutokana na kukosekana kwa mvua ya kutosha msimu huu.
Alisema kukosekana kwa mvua ya kutosha kunaweza kusababisha kuibuka kwa njaa hivyo ili kuepuka fedheha hii ya baa la njaa wananchi wanapaswa kutokuwa na tamaa ya kuuza chakula chote ili kiwasaidie iwapo mvua itaendelea kunyesha kwa kusuasua.
Baadhi ya maeneo ambayo wananchi wamekuwa wakitoa malalalamiko ya mazao yao kukauka na jua ni pamoja na Masuguru, Mtonya, Luegu, Litola, Lusewa,Rwinga, Mandepwende,Likuyu,Mputa na Namtumbo ambako ndiko kunakotegemewa kwa ajili ya mazao ya chakula na biashara kama vile Mahindi, Mpunga,Tumbaku, Mbaazi na Ufuta.

Post a Comment