Ads (728x90)


Mchungaji Antony Lusekelo( Mzee wa Upako) niliyemfahamu kwa jina la SEKELO enzi hizo

 Wacheza Karatee aina ya GoJu Ryu wakiwa katika stence kujiandaa na shambulizi
Baadhi ya wacheza Karate aina ya GoJu Ryu katika DOJO mbalimbali duniani( Picha kwa hisani ya Mtandao)
#SEKELO

Kundi la vijana wapatao 12 hadi 20 wenye umri kati ya miaka 12 hadi 18 walikuwa wanahudhuria mafunzo ya Karate mtindo wa Go Ju Ryu yenye asili yake katika Kisiwa cha Okinawa nchini Japan.

Mafunzo haya ya Karate yaliyokuwa chini ya Dojo la Sempai Haruna yalikuwa yakifanyika kila siku katika Ukumbi wa Olofea( Wallfare) mjini Iringa hii ilikuwa ni miaka 35 iliyopita.

Kila siku Sempai Haruna(Said Kassim Haruna) alikuwa akiwafundisha vijana wale upole na kutolipiza kisasi kutokana na aina ya  mafunzo hayo kuwa yalikuwa ni mafunzi ya hatari ambayo ni silaha pekee ya mauaji inayopaswa kutumiwa kwa uangalifu mkubwa.

Sempai Haruna ambaye kwa wakati huo alikuwa na Mkanda wa Brown akiutafuta mkanda mweusi baada ya kupitia mkanda wa Kijani na Mweupe alikuwa ni mahiri kwa mafunzo na alimudu vyema kuwa treat vijana wake ambao kwa wakati ule walikuwa wamejenga heshima kubwa ya mafunzo wakihudhuria kwa wingi katika Dojo ambalo lilipewa jina maarufu ‘Hekalu la Kujilinda’.

Katika siku za mwanzo kundi kubwa la vijana lilihudhuria mafunzo, nadhani hii ilitokana na hamasa ya miaka ile ya vijana kupenda kujifunza Sanaa ya Mapigano kutokana na ujio wa filamu za Kung Fu na Karate.

Baadhi walihamasika ili wajifananishe na Bruce Lee Mchina aliyetokea kuwa mahiri kwa  kucheza Kung Fu ama Sonn Chiba Mjapani kutokea Kisiwa cha Okinawa nchini Japan aliyekuwa mahiri katika mapigano hasa kwa mchezo wa Karate ya mtindo wa Go Ju Ryu( Ngumu Na Laini).

Kadri siku zilivyoyoma ndivyo ambavyo kundi lilianza kuwa na wanafunzi wachache, lilipungua wanafunzi aidha kutokana na aina ya mafunzo na mazoezi yalivyokuwa magumu ama ni kutokana na namna ya mapokeo ya wanafunzi hao waliodhani kwamba mafunzo hayo yatawatuma kuingia mitaani na kupiga watu na kujionesha umahiri wa kupiga mateke na KATA.

‘’Maegel, Ushiro Gel,Jodan Zuki, Gedan Zuki Chudan Zuki’’  ni aina ya mateke na aina ya ngumi zilizokuwa zikitumika wakati wa mafunzo ambayo kila siku ya DOJO hasa kwa wale vijana wa awali kuingia walilazimika kucheza ngumi hizo na kupiga mateke aina hiyo hadi mwisho wa mafunzo wakati wale waliotangulia wakiwa katika KATA zingine kama vile Sanden Uke Bara ink.

Nimetanguliza muhtasari wa maelezo hayo ili nieleweke vyema maudhui yangu nikijinasibisha mimi mwenyewe mwandishi wa stori hii na kijana mdogo mwembamba mwenye kamwili kadogo wakati ule ambaye tulizoea kumuita jina la SEKELO.

Sekelo alikuwa ni kati ya vijana waliojiunga na DOJO la SEMPAI Haruna kwa mhemko akitaka ajue mambo mengi kwa wakati mmoja, bahati mbaya Sempai Haruna alikuwa akitoa mafunzo ngazi kwa ngazi ili wanafunzi wake tuelewe vyema Sanaa ya Mapigano.

SEKELO alikuwa ni kati ya vijana wa mwanzo kuingia mitini kutoroka DOJO kati ya kundi la vijana wengi waliojiunga na kutaka siku ya kwanza tu aweze kurusha mateke ya Ushiro Gel kabla hata hajajua kupiga teke la MAEGEL, teke la Ushiro lilikuwa ni la kuzunguka na Maegel lilikuwa ni teke la kawaida la kupiga mbele.

Na ili uweze kupiga teke la USHIRO ulipaswa kuwa Flexible kutokana na mazoezi ya muda mrefu unayohudhuria ikiwemo mazoezi ya viungo na Push Up, mazoezi ambayo mara nyingi SEKELO alikuwa akiyakacha.

Kundi kubwa la vijana walikimbia, hadi tukabaki vijana wachache na hatimaye tukabaki wanafunzi wawili, mimi Rashid Mkwinda na mwenzangu Abbas Upete, tulivumilia na mafunzo yetu na kufikia hatua kubwa tukauacha mkanda mweupe, tukaingia mkanda wa KIJANI na baadaye tukaupata mkanda wa BROWN wakati huo Sempai wetu akiwa ameukwaa mkanda mweusi, tuliacha kumuita SEMPAI tukajikuta tukimuita SENSEI ingawa yeye mwenyewe hakupenda kuitwa SENSEI.

SEKELO ambaye kwa sasa asilimia kubwa ya Watanzania wanamuita MZEE WA UPAKO tulikuwa tukimuita hivyo kwa jina kifupi cha jina la LUSEKELO, wakati ule sikulijua jina la ANTONY tulizoea kumuita hivyo SEKELO.

Mimi na mwenzangu Abbas Upete tulipata kazi kubwa sana ya kumfundisha SEKELO kwa kuwa tuliwa ni kati ya vijana wakubwa katika DOJO lile na hawa akina SEKELO wakiwa ni vijana wadogo wadogo waliokuwa wakija kwenye HEKALU LA KUJILINDA mara moja moja na siku ambayo alitokeza SEMPAI Haruna hakuacha kumpa adhabu ya kupiga Push Up.

Wakati ule SEKELO nilikuwa namuona kama kijana mbishi na mwenye pupa aliyetaka kujua mengi kwa wakati mmoja bila kupitia ngazi zingine,pia nilimuona ni kijana mwenye hamaki ni kama alijiunga katika DOJO kwa ajili ya KULIPIZA KISASI kwa vijana wenzie waliokuwa wakimuonea shuleni kwao pale WILOLESI ambao mara kadhaa walimtwanga MAKONZI,nilimuona SEKELO kama mtu wa visasi.

Wakati huo DOJO likiwa limebaki na wanafunzi watatu pamoja na mwenzetu mmoja mwanafunzi aliyekuwa akisoma Highland Secondary( mwenzangu Abbas Upete atakuwa anamkumbuka vyema), SEKELO alikuwa akija mara moja moja kuchungulia kuona hatua tuliyofikia hata baada ya kuhama kufanyia mazoezi OLOFEA hadi shule ya Msingi AZIMIO vijana wengi walikuwa wakija kusimama na kuchungulia dirishani akiwemo SEKELO.

Nilipotezana na SEKELO miaka ile ya mwanzoni mwa themanini hadi miaka ya hivi karibuni ANTONY LUSEKELO(MZEE WA UPAKO) alipoanza mahubiri, nilijiuliza maswali mengi, bali niliamini kwamba ni kitambo kirefu tumeachana inawezekana SEKELO amebadilika tabia na kwa vile anamtumikia Mungu huenda kwa sasa ameongoka na amekuwa mtumishi wa kweli wa wanaKONDOO waliopotea wanaohitaji uongofu.

Leo Napata picha halisi ya ANTONY LUSEKELO niliyemjua tangu miaka ya themanini akiwa kijana mdogo tukimfundisha kupiga ngumi na mateke na baadaye kuamua kuingia mitini huenda ni baada ya kuona makusudio yake ya kujifunza KARATE ili akalipize kisasi kwa waliomtandika KONZI shuleni hayakutimia.


Post a Comment