Ads (728x90)

SMZ yadaiwa kupanga kuhujumu ushindi wa CUF
-Yadaiwa safari hii mbinu imeelekezwa kuzuia uandikishaji daftari la kudumu

Na,Rashid Mkwinda,Zanzibar.

UKIWA umesalia takribani mwaka mmoja kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 na mvutano juu ya uundwaji wa serikali ya mseto visiwani Zanzibar kumeibuka madai ya hujuma na mkakati wa ushindi wa kishindo kwa chama cha Mapinduzi CCM dhidi ya chama cha Wananchi CUF.

Mkakati huo unadaiwa umelenga kupunguza kasi ya kile kinachozungumzwa na viongozi wa siasa kilichojadiliwa katika mazungumzo ya muafaka baina ya vyama vya CCM na CUF ambao hata hivyo utekelezaji wake umeonekana kusuasua na hivyo kuleta hisia tata na tete za kuibuka upya kwa mgogoro wa kisiasa katika uchaguzi ujao.

Miongoni mwa mambo yanayodaiwa kujadiliwa katika mazungumzo ya muafaka kwa vyama hivyo ni uundwaji wa serikali ya mseto ambapo hivi karibuni viongozi wa juu wa chama tawala akiwemo Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Bw. Samwel Sitta na Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara ambaye pia ni Spika Mstaafu Bw.Pius Msekwa kuzungumzia kuwepo kwa serikali ya mseto visiwani.

Madai ya kuwepo kwa mkakati huo yanadaiwa kuwa ni mahsusi yaliyoandaliwa na Chama Cha Mapinduzi CCM kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za kiserikali ikiwemo Tume za Uchaguzi NEC na Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC kwa kuhusisha vyombo vya dola kuhakikisha CCM kinashinda uchaguzi hata kama kitashindwa Visiwani Zanzibar.

Aidha mkakati huo umelanga pia kushinda viti sita vya uwakilishi na Ubunge Kisiwani Pemba ili kuvunja kabisa uwepo wa nguvu za CUF visiwani humo unaosababisha kuibuka kwa serikali ya mseto visiwani humo ambapo pia mchakato huo unadaiwa pia ulianza kwa kupunguza majimbo ya uchaguzi yaliyo ngome ya CUF kwa kuvunja majimbo ya Mlandege na Malindi na kuwekwa jimbo moja la Mjimkongwe.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari vimedai kuwa mkakati huo ambao awali ulikuwa ni wa siri ndani ya chama cha Mapinduzi CCM umevuja na kudhihirika katika kauli ya Waziri wa Habari michezo na Utamaduni Bw. George Huruma Mkuchika aliyeibuka hivi karibuni na kuelezea kuwa CUF isitegemee kuwepo kwa serikali ya mseto Zanzibar.

Bw. Msekwa alinukuliwa na vyombo vya habari nchini kikiwemo Televisheni ya Taifa TBC 1 akionesha umuhimu wa kuwepo kwa serikali ya mseto visiwani akihofia kuwepo kwa mgogoro wa kisiasa kama uliowahi kutokea katika nchi za Kenya na Zimbabwe katika uchaguzi mkuu wan chi hizo.

Hata hivyo kauli ya Bw. Mkuchika ya kupinga kuwepo kwa serikali ya mseto inaelezwa kuwa ndio mkakati halisi wa chama cha Mapinduzi kuelekea katika uchaguzi mkuu ujao ambapo kauli ya akina Mzee Msekwa na Spika Sitta imedaiwa kuwa ni kiini macho cha kuwalaghai Wazanzibari waamini kuwa mazungumzo ya muafaka yatatekelezwa kabla ya uchaguzi mkuu wa 2010.

Mazungumzo ya wakazi wengi visiwani humo yaliyonaswa na gazeti hili katika maeneo mbalimbali ya mikoa ya Mjini Magharibi,Kaskazini Unguja na mkoa Kusini Unguja na takribani maeneo yote ya mikoa ya Kisiwani Pemba kutoka kwa watu mbalimbali hususani kwa wafuasi wa chama cha Wananchi CUF kwamba huo ni muendelezo wa hujuma za ushindi kwa CCM.

CUF ilidaiwa kupata ushindi katika uchaguzi wa mwaka 1995 hata hivyo ushindi huo ulidaiwa kubatilishwa baadaye na kumpa ushindi mgombea wa CCM Dkt.Salmin Amour Jumaa(Komandoo) aliyepata asilimia 50.02 dhidi ya mgombea wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad aliyepata asilimia 49.08 ya kura zote zilizopigwa visiwani humo.

Katika uchaguzi huo kama ilivyotangazwa awali Dkt.Salmin alipata kura halisi 165,706 sawa na asilimia 49.05 ilhali Maalim Seif alipata kura halisi 163,706 sawa asilimia 49.03 ambapo hata hivyo hesabu hiyo ya kura haikuhusishwa kura zilizoharibika na zile zilizokosewa ambazo ni 4,922 sawa na asilimia 1.47.

Inadaiwa hakukuwa na uainishaji wa kura zilizoharibika ambazo kama ingeweza kuainishwa vyema uchaguzi huo ungerejewa kutokana na kufungana kwa wagombea wa urais kwa CCM na CUF mwaka 1995 ilhali hata watafiti kutoka umoja wa Kimataifa wa UNDP walipohesabu kura katika jimbo la Mlandege na Kitope walibaini hujuma za uchaguzi dhidi ya chama kimoja.

Taarifa zaidi zinadai kuwa muendelezo wa hujuma hizi pia uliibukia katika uchaguzi wa mwaka 2000 ambapo inadaiwa visanduku vya kupigia kura viliibiwa na wasimamizi wa uchaguzi na kukaa kwa siku sita na hatimaye kutangazwa kwa mshindi ambaye ni mgombea wa Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt.Salmin aliyetangazwa kupata asilimia 63 dhidi ya asilimia 37 za mgombea wa CUF.

Ushindi huo ndio unaodaiwa kuzusha mtafaruku na mgogoro mkubwa visiwani na kusababisha kutokea kwa mauaji na baadhi ya wananchi kukimbia makazi yao na kuishi uhamishoni nchini Kenya na baadaye kukimbilia Mogadishu Somalia hadi sasa hawajulikani hatima yao na familia zao.

Taarifa za kiuchunguzi kutoka katika vyanzo mbalimbali visiwani zimedai kuwa mkakati huo umeibuliwa kutokana na madai ya asilimia kubwa ya wapiga kura wa mwaka 2010 kubadilika na kutaka kukipa ushindi chama cha Wananchi CUF hususani kutokana na mauaji yaliyofanywa na vyombo vya dola wakati wa maandamano yaliyofanywa na wafuasi wa CUF visiwani humo.

Uwiano wa idadi ya wapiga kura kwa mwaka 1995 ulikuwa ni asilimia 90 kwa asilimia kumi za CCM kisiwani Pemba ilhali katika Kisiwa cha Unguja ilikuwa ni kati ya asilimia 58 za CCM na asilimia 42 za CUF idadi ambayo inaongezeka na kupungua kulingana na matukio ya kisiasa yanayojiri kwa nyakati tofauti visiwani humo.

Inadaiwa kuwa mabadiliko hayo ndiyo yanayosababisha kuwepo kwa mkakati wa ushindi kwa CCM kutafuta ushindi kwa namna yoyote ambapo hadi sasa idadi ya wananchi wanaostahili kupiga kura ambao awali walikuwa hawana fursa hiyo kutokana na kutotimiza umri ndilo hilo kundi la vijana ambao wengi wao wanakumbuka madhila na maafa yaliyotokana na uchaguzi wa mwaka 1995.
Katika kisiwa cha Unguja inaonesha asilimia za wapiga kura kwa upande wa CCM zinaendelea kupungua kwa matukio yanayoibuka mara kwa mara ambapo kwa sasa inaonesha kuna uwiano unaokaribiana baina ya wafuasi wa CCM na wale wa CUF huku kukiwa na dalili za kuzidiwa idadi kwa upande wa CCM kwa asilimia 55 kwa asilimia 45.

Taarifa zaidi zimedai kuwa asilimia kubwa ya waliotarajiwa kupiga kura mwaka 2010 ni vijana wadogo waliokuwa chini ya miaka 18 mwaka 2001 wakati wa vurugu zilizosababisha mauaji Januari 27 2001 na maandamano yaliyofanywa na wafuasi wa CUF ambao kwa sasa wamefikisha miaka 25 hadi 27 na kwamba kukiunga kwao mkono chama hicho kimetokana na hisia za chuki kutokana na nguvu kubwa ya dola iliyotumika kudhibiti upinzani.

‘’Kumbuka vijana wanaonyimwa mara hii kuandikishwa katika daftari la kudumu,mwaka 1995 walikuwa hawajatimiza miaka 18…wengi wao walikuwa bado watoto…wanakumbuka namna kaka zao walivyouliwa na wengine kukimbia makazi yao na hata dada zao kubakwa…si rahisi kwa hawa kukipigia kura CCM,’’alisema mmoja wananchi mkazi wa Wete Pemba.

Hata hivyo kumekuwepo na takwimu zinazopishana juu ya idadi ya watu waliouawa katika maandamano hayo huku upande wa serikali ukidai waliouawa walikuwa ni 23 ilhali upande wa CUF ukidai kupoteza watu 47 na kufikia zaidi ya 100 wakiwemo wale walikokimbilia uhamishoni na kwenda kuishi Shimoni Mombasa nchini Kenya na baadaye kaskazini mwa Kenya na hatimaye Mogasdishu nchini Somalia.

‘’Hawa vijana walipania kupiga kura za chuki…baadhi yao wala si wafuasi wa chama chochote, wamelazimishwa kuonekana ni wafuasi wa vyama vya siasa kutokana na chuki waliyonayo dhidi ya dola baada ya kuona na kusikia namna ndugu zao walivyouliwa na wanawake kubakwa,’’alisema mwananchi mmoja mkazi wa Wete mkoa wa Kaskazini Pemba.

Alidai mkazi huyo wa Wete ambaye hakupenda kutajwa jina lake kutokana na madai ya kulinda nafasi yake kisiasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 kuwa asilimia kubwa ya wakazi wa visiwa vya Pemba na Unguja ni wanandugu waliooleana na hivyo kujenga hisia za chuki dhidi yao kutokana na mambo ya kisiasa.

Matukio ya hujuma yanayodaiwa na CUF ni kwamba hujuma hizo zilisababisha pia kutokea kwa vurugu mwaka 2005 ambapo kwa mujibu wa Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar Bw. Juma Duni Haji ni kwamba matokeo yaliyotangazwa na Tume ya uchaguzi ZEC ni kwamba Rais Aman Karume alipata kura halisi 239,832 sawa na asilimia 53.02 ilhali Maalim Seif alipata kura halisi 207,733 sawa na asilimia 46.01.

Bw. Duni alisema kuwa hitilafu katika uchaguzi huo ulitokana na wizi wa fomu za uchaguzi ambapo baada ya malalamiko ya CUF,tume ya uchaguzi Zanzibar (ZEC)ilitoa matokeo ya pili baada ya mwezi mmoja ambayo yalionesha kuwa Rais Karume alipata kura halisi 241,899 sawa na asilimia 53.06 ilihali Maalim Seif alipata kura halisi 205,872 sawa na asilimia 45.06 na hivyo kuthibitisha kuwa kulikuwa na wizi wa kura zaidi 184 kutokana na kutangazwa mara mbili kwa matokeo ya uchaguzi.

Kwa mujibu wa Bw.Duni ni kwamba dosari zinazoendelea kujitokeza katika uandikishwaji wa daftari la kudumu visiwani ni muendelezo wa hujuma na ushindi dhidi ya CCM kwa kuzuia watu halali wanaostahili kuandikishwa na kupandikiza watu kutoka maeneo mbalimbali.

Alitolea mfano jimbo la Nungwi, Tumbatu visiwani Unguja na jimbo Konde kisiwani Pemba na kusema kuwa idadi ya waliopewa vitambulisho katika Shehia ya Uvuvini 84 lakini walioandikishwa ni 1109 ambapo katika jimbo la Konde katika shehia ya Msuka Magharibi kisiwani Pemba idadi ya waliopewa vitambulisho ni 81 ilhali walioandikishwa ni 1056.

Akizungumzia madai hayo ya CUF Mkurugenzi wa Vitambulisho wa Zanzibar Bw.Mohamed Juma Ame alisema kuwa idadi ya wakazi huongezeka na kupungua kulingana na uanzishwaji wa Shehia mpya kwa mujibu wa mamlaka ya Mkuu wa mkoa ambaye anaamua kuanzisha Shehia moja ama kuivunja Shehia nyingine.

Alisema wapo watu walioandikishwa kabla ya kuanzishwa kwa Shehia husika hivyo kuonekana kama hawana sifa ya kujiandikisha bali kinachoangaliwa kama ni mkazi wa jimbo hilo anakubaliwa kujiandikisha katika Shehia yoyote iliyopo jimboni humo tofauti na madai ya CUF kwamba kuna watu wanapandikizwa katika uandikishaji.

Bw.Ame alitolea mfano jimbo la Tumbatu ambako alisema kuwa jumla ya watu 9501 wamesajiliwa lakini wenye vitambulisho vya ukaazi ni 5538 ilhali idadi hiyo imepungua kutoka watu 10,881 waliosajiliwa mwaka 2005 ambapo katika jimbo la Konde waliosajiliwa ni 6,445 lakini waliopata vitambulisho ni 2,500.

Aliyataja majimbo mengine kuwa ni jimbo la Mgogoni ambapo mwaka 2005 watu waliosajiliwa ni 8,529 ilhali mwaka 2009 walisajiliwa ni 6284 na hivyo kuwa na tofauti ya watu 2,245 ambapo katika jimbo la Micheweni waliosajiliwa walikuwa ni 9814 mwaka 2005 na kupungua idadi hiyo hadi kufikia watu 7,513 kwa mwaka 2009 na hivyo kuwa na tofauti ya watu 2311.

Alisema madai yanayotolewa na CUF hayana msingi kutokana na kuzidiwa na teknolojia kutokana na kupandikiza watu wasiotimiza umri na wengine kutoka nje ya Zanzibar kama vile Pangani na Mombasa.

‘’Waanasiasa wanaona idadi inazidi kupungua hivyo ‘wamepanic’teknolojia ya mara hii imewazidi nguvu hawana ujanja wa kupandikiza watu…wanachokifanya kwa sasa ni propaganda zisizokuwa na msingi,’’alisema Bw.Ame.

TAMATI.

Post a Comment