Ads (728x90)

MOJA YA KABURI LA MTU ALIYEUAWA KWA USHIRIKINA
MWANAMKE ALIYEDAIWA KUPIGWA NA KUVULIWA NGUO NA ASKARI POLISI
MKAZI WA MYUNGA AKISISITIZA KUTOHESABIWA SIKU YA SENSA
MWANAMAMA ALIYEDAI KUVULIWA NGUO NA ASKARI POLISI
DIWANI WA KATA YA TUNDUMA NA DIWANI WA KATA YA MYUNGA WAKISIKILIZA KERO ZA WANANCHI
MWANANCHI AKISISITIZA JAMBO KATIKA MKUTANO WA WANANCHI MYUNGA
MKAZI WA MYUNGA AKIELEZEA MATUKIO YA MAUAJI YANAYODAIWA KUFANYWA NA MFANYABIASHARA ANAYEDAIWA KUKUMBATIWA NA SERIKALI

Na, Rashid Mkwinda, Momba


WAKATI zoezi la sensa ya watu na makazi likiendelea nchini kote wakazi wa kijiji cha Myunga kata ya Myunga wilayani Momba mkoani Mbeya wamesisitiza azma yao ya kutohesabiwa hadi pale serikali itakapotoa tamko juu ya kulindwa kwa mtuhumiwa wa mauaji ya njia za ushirikina yaliyodaiwa kufanywa na mfanyabiashara mmoja kijijini hapo.

Wananchi hao walizungumza katika kikao maalumu cha kutathmini mauaji yaliyotokea kijijini hapo na kusababisha  uvunjifu wa amani uliotokana na kuuawa kwa wakazi wa kijiji hicho na kunyofolewa sehemu za siri ambapo hata hivyo mtuhumiwa wa mauaji hayo alitimuliwa kijijini hapo baada ya wananchi wenye hasira kubomoa na kuchoma nyumba yake.

Madai ya kuwepo kwa mauaji ya kishirikina yaliibuliwa mwezi Machi mwaka huu ambapo jumla ya watu saba waliuawa na miili yao kukutwa pembezoni mwa mto Momba ambapo mara baada ya wananchi hao kupiga kura walimbaini mfanyabiashara huyo (jina tunalo) kuwa anahusika na mauaji hayo.

Wakielezea ushahidi wa kuthibitisha kuhusishwa kwa mfanyabiashara huyo wakazi wa kijiji hicho walisema kuwa baadhi ya nguo za watu waliouawa zilikutwa nyumbani kwa mfanyabiashara huyo zikiwa zimetapakaa damu huku kukiwa na baadhi ya silaha kama vile visu na mapanga ambayo yanadaiwa kutumika kufanya mauaji.

Jofrey Simwanza mkazi wa kijiji cha Lwasho katika kata ya Myunga  alisema kuwa mmoja wa vijana waliouawa aliyefahamika kwa jina la Shati Sichula mwili wake ulikutwa chini ya daraja la mto Momba huku mwili wake ukiwa umeondolewa baadhi ya viungo kama vile sehemu za siri, macho na ulimi.

Alisema kuwa matukio ya mauaji hayo yaliendelea ambapo mwezi Juni mwili wa msichana mmoja ulikutwa ukielea katika mto Momba huku ukiwa  umekatwa matiti na kunyofolewa ulimi,macho na sehemu za siri ambapo matukio hayo yalisababisha wananchi kuhoji sababu za mfanyabiashara huyo kutochukuliwa hatua za kisheria.

Akizungumzia matukio hayo kijijini hapo Ofisa mtendaji wa kata hiyo Salum Jonas alisema kuwa kata hiyo yenye wakazi wanaokadiriwa kufikia 1,200 na kaya 200 wanaishi katika hofu kutokana na mauaji yaliyotokea ambayo yanahusishwa na imani za ushirikina hali ambayo inawafanya wakimbie nyumba zao na kuishi porini.

Alisema kuwa mara baada ya kutokea kwa mauaji hayo wananchi walivamia nyumba tatu za watu wanaohisiwa kuwa ni  wauaji na kuzichoma moto na kisha kubomoa na kusababisha upotevu wa mali zilizokuwemo katika nyumba hizo.

Alisema kuwa hatua hiyo ilisababisha jeshi la polisi kuwakamata wananchi wapatao 45 wakiwemo wafanyakazi wanaojenga barabara ya Tunduma- Sumbawanga ambao wanaishi kijijini hapo na kwamba hata hivyo baadhi yao waliachiwa huru na kubakizwa watuhumiwa 13 ambao wanahusishwa na kosa la jinai la kuvunja na kuiba.

Kwa upande wao wananchi wa kijiji hicho walidai kuwa utaratibu uliotumika kuwakamata watuhumiwa hao haukuwa wa kibinadamu kwa kuwa askari waliotumwa kuwakamata walivamia nyumba na kubomoa milango na kuwakamata baadhi ya akina mama wakiwa uchi na kuwapakiza katika gari la polisi nyakati za usiku.

Walisema kuwa kitendo hicho kinashindwa kuwabaini watu wema na wahalifu ambapo hata watu watakaokuja kuhesabu sense wanadaiwa kuja nyakati za usiku hali ambayo bado itajenga hofu kwa wao kutoa ushirikiano kwa makarani wa sensa.

Mmoja wa akina mama hao aliyejitambulisha kwa jina la Anna Nakamanga alisema kuwa askari walivamia nyumbani nyakati za usiku na kuwatoa nje wakiwa uchi kisha kuwatandika viboko na kusema kuwa kitendo hicho ni udhalilishaji mkubwa uliofanywa na askari polisi kwa raia wasio na hatia.

Naye kiongozi  wa Kanisa la Pentekostal la kijijini hapo aliyejitambulisha kwa jina la Mchungaji Nsokolo alisema kuwa matatizo yaliyopo kijijini hapo yamesababishwa na mauaji ya kinyama yaliyofanywa na mfanyabiashara huyo ambaye pamoja na kupatikana kwa vidhibiti juu ya mauaji aliyoyafanya jeshi la polisi limemuachia huru bila kumchukulia hatua za kisheria.

Akizungumzia tukio hilo kwa njia ya simu kamanda wa polisi mkoani Mbeya Diwani Athuman alisema kuwa alifikishiwa taarifa za wizi na uharibifu wa mali na mmoja wa wafanyabiashara wa eneo hilo ambapo alichokifanya ni kuamuru wahusika wakamatwe kwa kuwa walifanya kosa na kwamba hakuna taarifa zilizofika kwake zinazohusu mauaji dhidi ya wananchi kwa imani za ushirikina.

Aidha taarifa za awali zilidai kuwa mara baada ya mfanyabiashara huyo kukutwa na vidhibiti vya nguo zenye damu na silaha zinazodaiwa kutumika katika kutekeleza mauaji hayo aliachiliwa huru kwa kile kilichoelezwa kuwa aliwahonga  fedha baadhi ya viongozi wa polisi wa wilaya ili kuficha ukweli wa tukio hilo.





Post a Comment