Ads (728x90)

WAKILI maarufu nchini ambaye pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Mbeya Bw.Sambwee Shitambala amechukua na kurejesha fomu ya kuwania nafasi ya Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC)na kuendelea kuwabeza wapinzani kwa kutokuwa na mikakati endelevu ya maendeleo kwa wananchi.

Bw.Shitambala ambaye amekuwa ni miongoni mwa wanachama kadhaa wa CCM waliojitokeza kuwania nafasi hiyo ameendelea kuviponda vyama vya upinzani na kusema kuwa ni ndoto kwa vyama hivyo kushika dola kwa kuwa wanaendelea kupandikiza chuki kwa wananchi dhidi ya serikali na hivyo kusababisha kudorora kwa maendeleo.

Bw. Shitambala amekuwa ni miongoni mwa wanasiasa machachari wakati akiwa katika kambi ya upinzani ambaye pia amewahi kugombea Ubunge kwa tiketi ya CHADEMA katika jimbo la Mbeya vijijini akichuana na mgombea wa CCM na baadaye aliamua kujiunga na CCM April Mwaka jana mjini Dodoma mbele ya Rais Jakaya Kikwete.

Amesema kuwa ameamua kujichimbia zaidi ndani ya uongozi wa juu wa CCM ili kuweka mikakati na mizizi imara itakayofanya chama hicho kising’oke madarakani na kwamba ukongwe wa chama hicho unakisaidia kukifanya kiendelee kuongoza nchi kwa karne nyingi zijazo.

Amesema kuwa nia yake ya dhati ni kuona  CCM haing’oki madarakani,kwa kuwa  ina uwezo mkubwa ambapo ikitupwa itakuwa imetupwa hazina ambayo haiwezi kupatikana tena nchini.

Amefafanua kuwa ameingia katika uongozi kama mwakilishi mwaminifu na makini kwa ajili ya kuitumikia nchi na kwamba wale wanaodai kuwa CCM itakufa wanajidanganya nafsi zao kwa kuwa hawaijui vyema CCM.

Amezidi kubainisha kuwa chama chochote chenye viongozi makini kila kinapomaliza uchaguzi kinarejea kwenye utekelezaji wa ilani zake kwa maslahi na tija ya wananchi na si kuendeleza malumbano na maandamano ambayo yanaibua chuki na uhasama baina ya wananchi na serikali yao.

Wengine waliojitokeza kuwania nafasi hiyo hadi leo mchana ni pamoja na mkulima aliyewahi kuingia katika mchuano wa kura za maoni kugombea nafasi ya Urais ndani ya CCM mwaka 1995 Bw.Agrey Mwasanguti ambaye pia amerejesha fomu yake jana katika ofisi za CCM wilaya ya Mbeya mjini.

Post a Comment