KIKAO cha
dharura cha Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya Mbeya kimependekeza jina la mkoa
mpya wa Mbeya liwe ni Mkoa wa Mbozi badala ya mkoa wa Rungwe kama
ilivyopendekezwa na wataalamu,wenye makao yake makuu wilayani Mbozi katika mji
wa Vwawa.
Wakizungumza
katika kikao hicho Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Mbeya walisema kuwa azma
ya kupendekeza kuwepo kwa mkoa mpya katika wilaya ya Mbozi umezingatia
jiografia ya mkoa na fursa za kiuchumi zilizopo badala ya hamasa za siasa.
‘’Sisi ni
madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Mbeya, hatuna maslahi yoyote ya kisiasa na
wilaya ya Mbozi, tumezingatia fursa za kiuchumi na jiografia ya mkoa ambayo
italeta tija na maslahi kwa Taifa,’’alisema Bw.Mashauri Mbembela Diwani wa kata
ya Nsalaga.
Awali katika
mapendekezo hayo ambayo yaliwasilishwa na Ofisa Uchaguzi wa wilaya kwa niaba ya
Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mbeya Bi. Marietha Mlozi,Bw.Edward
Mwaigombe alisoma taarifa ya mapendekezo ya jina la mkoa mpya kuwa ni Rungwe
kama lilivyopendekezwa na wataalamu.
Bw.
Mwaigombe alisema kuwa, taarifa ya wataalamu imezingatia vigezo vya idadi ya
watu, ukubwa wa eneo, huduma zilizopo na mawasiliano ambayo ni mapendekezo
kutoka katika kamati za maendeleo za kata 14 za Ulenje,Lwanjilo,
Ikukwa,Swaya,Mshewe,Igale, Iyunga Mapinduzi,Tembela,Bonde la Songwe, Utengule
Usongwe, Ilungu, Ilembo na Inyala.
Alisema kuwa
kamati zilipendekeza mkoa wa Mbeya ugawanywe katika mikoa miwili ya Mbeya na
Rungwe ambapo mkoa wa Mbeya wenye takwimu ya idadi ya watu 1,721,795 na ukubwa
wa eneo la kilomita za mraba 41,544 umependekezwa kuundwa kwa wilaya za
Chunya,Mbozi,Momba, ambapo makao yake makuu yanatarajiwa kuwa jiji la Mbeya.
Bw. Mwaigombe
alisema kuwa mkoa wa pili ambao una takwimu ya watu 985,915 na ukubwa wa eneo
wa kilomita za mraba 22,073 unatarajiwa kuundwa na wilaya za Mbarali,
Rungwe,Kyela na Ileje na makao yake makuu yanatarajia kuwa katika wilaya ya
Rungwe.
Aidha katika
taarifa hiyo kwa madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, ilipendekezwa
kuanzishwa kwa wilaya mpya kutokana na jiografia na kuzingatia mgawanyo mpya wa
mkoa kati ya wilaya ya Mbeya na Halmashauri ya Jiji la Mbeya na kupendekezwa
wilaya hizo zigawanywe katika wilaya tatu.
Hata hivyo
katika mapendekezo ya madiwani wa halmashauri hiyo walisema kuwa mji wa Mbalizi
ujigawe kutoka katika halmashauri ya wilaya ya Mbeya na ujitegemee kuwa wilaya
kamili.
Katika mapendekezo
ya awali madiwani walipendekeza majina mawili ya mkoa wa Mbozi na Mkoa wa
Songwe ambapo jina la mkoa wa Mbozi lilipitishwa na madiwani kwa kura 24 dhidi
ya kura 3 ambapo baadaye majina mawili ya mkoa wa Rungwe na mkoa wa Mbozi nayo
yalipigiwa kura na jina la mkoa wa Mbozi lilipita kwa kura 24 dhidi ya kura
tatu za jina la mkoa wa Rungwe.
Akizungumza
katika kikao hicho Makamu Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mbeya Bw.
Mwalingo Kisemba alisema kuwa mchakato huo umekuja baada ya ushauri na mapendekezo
ya kuugawa mkoa wa Mbeya ambao kwa sasa una jumla ya watu milioni 2.7 na ukubwa
wa kilomita za mraba 63,617.
Post a Comment