Baadhi ya wakazi wa Jiji la Mbeya wakimsikiliza Prof. Mark Mwandosya |
`Mmoja wa wazee maarufu kutoka Kata ya Lufilyo wilayani Rungwe akitoa nasaha zake kwa Prof. Mwandosya |
Ifuatayo ni hotuba ya Profesa Mark Mwandosya
alipotangaza nia yake ya kuwania Urais kwa tiketi ya CCM kwenye viwanja vya
ukumbi wa Mikutano wa Mkapa jijini Mbeya jana.
Nianze kuwa kumshukuru Mwenyezi Mungu,muweza wa yote
kwa rehema nyingi alizotushushia kutuwezesha kuifikia siku hii ya leo. Kwani
hatukustahili zaidi ya wengi waliotutangulia mbele za haki.Nawashukuru ninyi
nyote mliofika kuungana nami katika siku hii muhimu katika kukuza,kuimarisha na
kuendeleza demokrasia ndani ya Chama chetu,Chama Cha Mapinduzi. Wazee
wangu, Waheshimiwa Maaskofu, Viongozi wa Dini na madhehebu
mbalimbali,Waheshimiwa viongozi wa kimila,Waheshimiwa Machifu,akina
mama,vijana,WanaCCM wenzangu,Viongozi wa vyama vya siasa,Wananchi,Wana
Mbeya,Nawashukuru,Asanteni sana kwa uwepo wenu.
Ndugu zangu,
Kwa muda mrefu na kwa njia mbalimbali za mawasiliano
mmekuwa mkinidadisi Mbona kimya kuhusu mwaka 2015? Pamoja nna kwambamliutaja
mwaka tu, lakini niliwaelewa.Wengi mliushangaa ukimya wangu.Pamoja na na kwamba
ukimya ni sehemu ya haiba yangu na daima nimeupokea kama ni karama
aliyonitunuku Mwenyezi Mungu,Muweza wa yote,baadhi yenu niliwajibu "
Ukimya una Kishindo"! Kuhusu Sultan Qabus wa Oman,mwandishi mmoja maarufu
aitwae Robert Kaplan amemwelezea ifuatavyo: Ni mtu mkimya, mpole, hapendi
kuzungumza na waandishi wa habari mara kwa mara, hapendi habari zake ziandikwe
kwenye magazeti mara kwa mara,lakini ameibadilisha nchi ya Oman kutoka makundi hasimu
ya makabila na kuwa taifa linaloheshimika na linaloendelea kwa kasi sana na
kuwa mfano wa kuigwa...." Sijifananishi na Sultan Qabus, la
hasha.Isipokuwa najaribu kusisitiza kwamba mara nyingi ni bora katika maisha
kuwa mjenga hoja na mtendaji makini kuliko kuwa mpayukaji na maamuzi ya
papo kwa papo yenye matokeo hasi na yenye hasara kwa taifa. Nimeenda nje kidogo
ya mada yangu!
Kwa staili ya siku hizi wagombea watarajiwa huwa
tunajitokeza na kusema : tutatangaza nia siku hii au ile! Nadhani tunawashangaza
na mtuwie radhi.Kwani kwa kusema hivyo tunakua tayari tumetangaza
nia!Basi nami kwa staili hiyo hiyo naomba kutangaza rasmi mbele ya kadamnasi
hii kama mashahidi,kwamba kwa unyenyekevu mkubwa, nitaomba ridhaa ya
kuchaguliwa kuwa mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Natarajia kuendeleza rasmi safari niliyoianza leo kwa kuchukua fomu za maombi
hayo pale Dodoma,Makao Makuu ya CCM, jumatano, tarehe 3 Juni,2015, saa 4
kamili,barabara.
Kipindi cha mpito kutoka awamu moja ya uongozi kwenda
awamu nyingine kingekuwa kigumu sana kwa nchi nyingi hasa nchi zetu za
kiafrika. Mifano iko wazi.Majirani zetu wamepata shida.Lakini waasisi wetu
Hayati Mwalimu Nyerere na Hayati Abeid Amani Karume wametujengea misingi imara.
Tuna kila sababu ya kuwashukuru na tuna kila sababu ya kujivunia misingi hiyo.
CCM haijayumba na CCM haitayumba.Baadhi ya wanachama inawezekana wameyumba.
Hebu tuzirudie Ahadi za mwana CCM: binadamu wote ni ndugu zangu na AFrika ni
moja, nitaitumikia nchi yangu na watu wake wote, nitajitolea nafsi yangu
kuondosha umaskini, ujinga, magonjwa na dhuluma, rushwa ni adui wa haki
sitapokea wala kutoa rushwa, cheo ni dhamana sitatumia cheo changu wala cha mtu
mwingine kwa faida yangu binafsi, nitajielimisha kadri ya uwezo wangu na kuitumia
elimu yangu kwa faida ya wote, nitashirikiana na wenzangu wote kujenga nchi
yetu, nitakuwa mwanachama mwaminifu wa ccm na raia mwema wa Tanzania na Afrika
nzima. Nitasema kweli daima fitna kwangu ni mwiko. Hii ndiyo CCM na atoaye
ahadi mbele za Mwenyezi Mungu ndiye Mwana CCM,na si vinginevyo.
Ahadi ya mwanaCCM ya kuondoa umaskini inanipa nafasi
ya kuelezea na kusisitiza kipaumbele muhimu sana cha serikali iliyodhamiria
kuwaondoa wananchi wake kutoka lindi la umasikini ni kukuza uchumi,uchumi wa
kisasa,uliojikita katika misingi ya sayansi na teknolojia na kutumia teknolojia
ya habari na mawasiliano kama kichocheo cha maendeleo hayo. Kama sayansi na
teknolojia ndio msingi wa uchumi wa kisasa basi naweza kusema,tena kwa
unyenyekevu mkubwa kwamba aliye mbele yenu ndiye pekee mwenye ujuzi,uelewa,na
uzoefu wa masuala haya. Ninalotaka kusisitiza hapa ni kwamba kukuza na
kusimamia uchumi ndio utakuwa kipaumbele namba moja.Jenga kwanza uchumi imara
na mengine yatafuata.
Uchumi imara unajengwa hasa pale panapokuwa na lengo
la kitaifa.Lengo katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ni Tanzania kufikia nchi
yenye kipato cha kati ifikapo mwaka 2025. Lengo hilo liliwekwa mwaka 2000.
Tudhamiria sasa kwamba ifikapo mwaka 2030 Tanzania iwe nchi za juu zenye
kipato cha kati(High Middle Income),na kwamba ifikapo 2050 Tanzania iwe nchi
iliyoendelea.
Tunawezaje kuyafikia malengo hayo? Tunawezaje kukuza
uchumi na ukuaji huo uwe endelevu?Hili ndilo swali.
1.Kilimo cha kisasa na cha kisayansi kupitia matumizi
zaidi na bora ya mbolea; kuendeleza utafiti kwa kuboresha miundombinu,vifaa,na
kuendekeza rasilimali watu;kuboresha mifumo na aina ya mikopo kwa wakulima
wadogo;kuboresha barabara za vijijini; kuendeleza ujenzi wa maghala kwa ajili
ya kutunza nafaka;kuwa na migumo ya uhakika ya masoko ya mazao;na kuhakikisha
kiwanda cha kimkakati cha mbolea itokanayo na gesi asilia kinajengwa haraka
iwezekanavyo.
2.Kuanzisha na kuendeleza viwanda,kwa kuanzia viwanda
vinavyoongeza thamani ya mazao na rasilimali asili
3.Kuendeleza kilimo cha umwagiliaji ili kuwa na
uhakika wa upatikanaji wa chakula.
4.Kuendelea kusimamia kutengemaa kwa uchumi mpana
5.Kuondoa vikwazo vinavyozuia uwekezaji wa ndani na
kutoka nje
6.Kuhakikisha sekta ya utalii inakuwa ipasavyo kwa
kufungua fursa nyingi za utalii wa ndani na utalii katika sekta ya kusini.
7.Kuongeza tija katika utendaji wa kazi kwa kuthamini
kazi(kufanya kazi kwa bidii,kwa uadilifu,na kwa kujituma), kusimamia
kanuni,maadili na miiko ya utumishi wa umma na kuufanya utumishi wa umma usiwe
wa mazoea tu bali wa ushindani unaopimika katika kutoa huduma kwa wananchi.Hii
itakwenda sambamba na kulinda haki na kuboresha msilahi ya wafanyakazi.
8.Kuchukia,kuzuia na kupambana na ufisadi na rushwa.
Kuondoa vikwazo vinavyoonekana kuwepo kwa matabaka mawili ya wananchi; wale
wanaoshughulikiwa na takukuru moja kwa moja,na wale ambao kibali kinahitajika
kuwashtaki,kwa kuipa Takukuru uwezo wa kisheria kufanya kazi bila kuingiliwa na
chombo chochote,wakati huohuo kuhakikisha haki za wananchi wema zinalindwa
kupitia chombo cha kusimamia malalamiko (ombudsman).
9.Kuendeleza na ikibidi kuimarisha uhuru wa Benki
Kuu na uhuru wa vyombo vya udhibiti wa huduma za kiuchumi,mifuko ya
jamii,bima.
10.Serikali kuwa injini ya ukuaji wa uchumi lakini
kuweka mazingira mazuri kwa sekta binafsi,mtu mmoja,vikundi vya
wajasiriamali,saccos,na kampuni binafsi kuchochea ukuaji wa uchumi.
Uchumi unapokua,basi serikali itakuwa katika nafasi
nzuri ya kutekeleza vipaumbele katika maendeleo ya jamii: Elimu,maji safi na
salama,afya, na miundombinu. Kuhusu elimu,lengo litakuwa ni kuboresha mitaala
ili iendane na matumizi ya sayansi na teknolojia katika ngazi zote;kuhakikisha
kila mtanzania ana nafasi sawa ya kujiendeleza kielimu kuanzia ngazi ya awali
mpaka elimu ya juu; kuendeleza elimu ya ufundi na kilimo; kuandaa na kutekeleza
mipango kwa hatua kuifanya elimu ya msingi ifikie kidato cha pili, cha nne na
hatimaye kidato cha sita;kuongeza wingi wa udahili wa wasichana katika
katika ngazi ya elimu ya juu;kuboresha hali na ari ya utendaji wa kazi
kwa walimu,ikiwa ni pamoja na ujenzi nyumba za kuishi na kuongeza ujira.
Katika maeneo mengine ya huduma za kijamii,lengo la
serikali litakuwa ni kutekeleza sera zilizopo na kuhakikisha malengo
yanatekelezwa na yanapimika.Katika kuleta afya bora kwa wananchi lengo litakuwa
ni kuweka mizania katika kuzuia na kupambana na magonjwa.
Uchumi hauwezi kukua pasipokuwa na amani na utulivu.
Amani usalama na utulivu ni tunu.Waasisi wetu wametujengea msingi wa tunu hii.
Viashiria vya kupotea kwa amani vinaanza kuonekana kutoka ndani na nje.Hali
inahitaji kuimarisha vyombo vyetu vya usalama katika maeneo yote hususan
mafunzo,vitendea kazi,vifaa, miundombinu na silaha za kisasa.Hatimaye ulinzi wa
nchi unaanzia mwananchi mwenyewe.
Nafasi ya Zanzibar katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania
ni kubwa. Hii inatokana na asili na haiba ya nchi zenye visiwa,Zanzibar ikiwa
mojawapo. Historia ya Zanzibar inatukumbusha hili.Kwani katika karne ya kumi na
tisa Zanzibar iliongoza eneo lote la Afrika ya Mashariki kiuchumi na
maendeleo,ukuondoa biashara ya utumwa. Ilisemekana Ikipigwa zumari Zanzibar
wanacheza ngoma maziwa makuu. Kila linalowezekana litafanywa kuondoa kabisa
hali inayoweza kuikwaza Zanzibar kufikia uwezo wake mkubwa kiuchumi.Muungano
utaimarika na uchumi wa Tanzania utakuwa kwa kasi zaidi.
Nahitimisha na suala muhimu la uzalendo.Kwa tafsiri
isiyo rasmi,Uzalendo ni upendo kwa nchi. Tumeanza kushuhudia kupungua kwa
uzalendo. Upungufu huo unajionesha katika kuenzi tamaduni za nje,kubeza juhudi
za maendeleo yaliyopatikana, viongozi kutoa matamshi yanayo kebehi nchi wakiwa
nje ya nchi,kutojivunia historia yetu iliyojikita katika michango ya mashujaa
wetu. Hawa ni pamoja na wale waliopambana na wakoloni,akina
Kinjeketile, Mkwawa ,Mirambo,Chaburuma na wengineo ambao walitoa uhai wao
kulinda na kutetea heshima ya mwafrika dhidi ya ukoloni.Aidha waasisi wa
TANU,Hayati Mwalimu Nyerere,Sykes,Mzee Kawawa, na wenzao;Waasisi wa Mapinduzi
matukufu ya Zanzibar,Hayati Abeid Amani Karume na wenzake akina Mzee Thabit
Kombo,Kanali Seif Bakari,Hais Darwesh,Edington Kisasi,Yusuf Himid,Said Washoto
na wengineo;ambao walionesha upendo na uzalendo wa hali ya juu.Vilevile tuna
mashujaa wa ukombozi wa Kusini mwa Afrika akina George Magombe na Hashim
Mbita.Tutaendelea kuenzi, kuthamini,na kuiendeleza michango mikubwa ya
Marais wetu wastaafu,Mzee Aboud Jumbe, Mzee Ali Hassan Mwinyi, Hayati Idris
Abdukwakil,Dr Salmin Amour,Dr Amani Abeid Karume,na Mzee Benjamin William
Mkapa. Kipekee napenda kuwashukuru Marais wetu wa sasa; Mheshimiwa Dr Jakaya
Mrisho Kikwete,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,na Mheshimiwa Dr Ali
Mohamed Shein.ambao wamefanya kazi kubwa ya kuimarisha uchumi na umoja wa nchi
yetu. Daima nitaenzi mchango wao. Tujivunie nvhi yetu na Kwa pamoja
tutaenga nchi tunayoitaka.
Post a Comment