Ads (728x90)

Bw. Makene hii ni sehemu ya kazi ambayo imenifanya niwe mvivu kupannndisha kazi za kishairi katika Blogu

RASI YA DHULUMIKA-1.

Na, Rashid Mkwinda.

CHOMBO kilikuwa kikikata mawimbi katikati ya bahari kuu usiku wa manane huku mawimbi ya bahari yakikilazimisha chombo hicho kufuata muelekeo sanjari na mawimbi hayo yaliyosababishwa na bamvua ambapo samaki wakubwa aina ya Papa na Nyangumi nao walijificha katika Matumbawe ya bahari wakiipa nafasi bahari kukamilisha mchafuko wake.

Giza lile totoro liliongeza hofu kwa mabaharia waliokuwemo ndani ya chombo ambacho kwa wakati huo kilionesha dhahiri kulemewa na misukosuko ya bahari huku Nahodha akijitahidi kwa kila hali kukinusuru chombo na mabaharia waliokuwemo kutokana na dharuba ile kuu ya Tsunami.

Kila aliyekuwemo katika chombo kile alihaha kunusuru maisha yake ilhali wasafiri ambao wengi wao walikuwa hawajui kuogelea wakiwa wamekumbatiana kila mmoja akiomba dua na uokovu na nusura ya Muumba wake ili aokolewe na gharika ile.

Hatima ya gharika ile iliwanusuru Baharia mmoja ambaye alishika kipande cha ubao na mwanamke mmoja ambaye aling’ang’ania guduria kubwa ambalo lilitumika kwa ajili ya kuhifadhia maji ya kunywa ambalo alielea nalo baharini kwa siku sita mtawalia.

Kila mmoja kati ya wahanga hawa wa Gharika la Tsunami ambalo ulikuwa ni mchafuko uliotokana na mtetemeko wa ardhi wa chini ya bahari alipata adha na shida ya aina yake ikiwa ni pamoja na kupoteza maisha na mali zilizokuwemo ndani ya Chombo.

Baharia ambaye kwa wakati huo alikuwa hoi akitarazia msaada wa kuokolewa kutoka katika Zilizala ile aliangaza pande zote kiasi cha upeo wa macho yake katika bahari kuu iliyojaa ukiwa huku Ndegemaji na wengine walao samaki wakitarazaki chochote baharini ambacho aidha kimesazwa na kizaazaa cha Tsunami au vinginevyo.

Alijaribu kutafakari maisha yake baada ya hapo na jinsi ambavyo angeweza kujiokoa katika balaa lile ambapo baadaye alijikuta akikosa nguvu na kukata tamaa ya kuendelea kuishi duniani kutokana na njaa na kiu alivyodumu nayo siku sita.

Nguvu zilimuishia, tumbole liliingia ndani kutokana na kukosa chakula, alishindwa hata kupata nguvu ya kumudu kusukuma pumzi zake,viini vyeusi vya macho yake vilianza kupanda juu, nuru ya macho yake ilianza kupotea na hivyo alianza kuona giza mbele yake….. taratibu viungo vyake vilikosa nguvu …alijiona yuko katika dakika za mwisho za uhai wake.

Baharia aliishiwa nguvu na kujikuta akikata tamaa ya kuendelea kuishi aliinama chini na kutafakari namna kifo chake kitakavyomkabili na jinsi atakavyokuwa chakula cha Papa na Nyangumi baharini alijikuta akidondokwa na machozi ambayo hata hivyo, hayakuwa na muombolezaji.

Alitafakari kwa makini mustakabali wake na kujiona ni mmoja wa watu waliokosa thamani chini ya anga hili,jambo moja pekee alilolikumbuka katika hali ile ya kufa kufa aliona ni kumuomba Mwenyezi Mungu amfishe ilhali akiwa ni miongoni mwa waja wema waliopata kuishi katika dunia hii.

Hivyo alitumia fursa hiyo kuungama makosa yake yote aliyoyafanya katika mazingira ya kidunia ili aweze kuishi vyema baada ya kifo chake.

Chini alijiinamia,
Dhambize kufikiria,
Mwishowe kuufikia,
Alilia Baharia.

Tama alijishikia,
Kwa kifo kukabilia,
Shida ilomkutia,
Ganzi alijisikia.

Kwa yake tafakuri,
Hakutarazi Saburi,
Mwokozi hakujiri,
Kwa dunia kuhajiri.

Moja alilokiri,
Kufa kifo cha bahari,
Lisionekane kaburi,
Samaki waule mwili.
.

Akiwa katikati ya mawazo na tafakuri nzito aliinua macho yake juu na kumuona kiumbe mmoja mrefu ambaye urefu wake ulitaka kukaribia kufika nusu anga mawinguni huku akiwa amesimama juu ya maji bila kuzama alimfuata baharia sanjari na muelekeo wa upepo wa bahari ulivyovuma.

Alimtazama kiumbe yule wa ajabu kwa hofu huku akitetemeka na kuendelea kutafakari upweke alionao huku akiwakumbuka wenzi wake waliohiliki katika dharuba ile ya Tsunami, kiumbe yule aliendelea kumkaribia Baharia kwa kasi ya ajabu huku baharia akiendelea kuingiwa na hofu kuu juu ya aina ya kifo chake kitakavyojiri.

Kiumbe yule alitembea juu ya maji kwa mwendo wa kasi, hatua moja sawa na hatua thelathini za binadamu wa kawaida, hofu kuu ilitanda katika moyo wa Baharia akijua mwisho wa maisha yake umewadia huku njaa na kiu vikimuandama kwa siku sita alizokuwa akielea baharini.

‘’Bora nijifie majini kuliko kufia mikononi mwa kiumbe huyu wa ajabu’’ alijisemeza Baharia huku mikono yake ikikosa nguvu na kujikuta akiachia ubao uliokuwa ukimsaidia kuelea nao majini,akajikuta akitumbukia baharini na kuanza kutapatapa majini huku akinywa maji ya bahari yaliyokoza chumvi chumvi na hivyo kumuongezea kupiga chafya mfulufulizo.

Kila alipokuwa akiachama mdomo wake kwa ajili ya kupiga chafya ndivyo ambavyo alizidi kunywa maji na hivyo kuhitimisha ile azima yake ya kuelekea safari ya kifo, taratibu alihisi Izraili mtoa roho akikaribia kuitoa roho yake alifumba macho yake ili asisikie machungu ya kutokwa roho, kwani alipata kusikia kuwa mtoa roho pindi anapotoa roho maumivu huwa ni makali kadhalika hushikwa njaa na kiu.

Kwa wakati huo yule kiumbe wa ajabu alikuwa amekwisha karibia alipo Baharia na wakati huo anajiachia kutoka katika kile kipande cha ubao ambao alikuwa akielea nao kwa siku sita alitanguliza kiganja chake kipana chini ya bahari na kukitawanya.

Baharia alijikuta akitua katika kiganja cha kiumbe yule wa ajabu na kwa kasi ileile akajikuta akipaa hewani juu na kushuka kwa kasi moyo wake ukimpaa na tumbo lake tupu ambalo lilikuwa halijapata chakula kwa siku sita likiunguruma kutokana na mshituko wa kupaa mithili ya mtu aliyepanda ndege au meli iliyokuwa ikisukwa sukwa na mawimbi.

Alipaa hewani mithili ya mtu aliyeko ndotoni ilhali akiwa amelala huku akiwa amenyoosha miguu yake ghafla akajikuta yuko katika ardhi nzuri yenye majani ya rangi ya kijani kibichi iliyokuwa na dalili ya kusheheni kila aina ya matunda na vyakula, ndege wa rangi mbali mbali waliruka huku na huko na kutoa mandhari nzuri ya sehemu ile iliyoambatana na manukato ya maua mazuri yaliyomo katika ardhi ile.

Baharia alijaribu kutafakari kama yumo ndotoni au yuko katika hali yake ya kawaida, alijaribu kurudisha fikra zake nyuma juu ya gharika waliyoipata baharini na baadaye kuokolewa kwa kujishikiza katika kipande cha ubao ambacho alielea nacho kwa siku sita na baadaye alichoka na kuamua kukiachia kibao huku akiwa amemuona kiumbe yule mrefu.

Akiwa katika tafakuri ile alihisi huenda alikuwa amekufa na yule kiumbe aliyemuona ndiye malaika mtoa roho za watu yaani Izraili na kwamba huenda pale alipo ni peponi, lakini jambo moja lilimpa shida katika mawazo yake,kwamba kwa wema gani alioufanya duniani apate malipo ya kukaa katika pepo nzuri kama ile?

Kwani ile ardhi ilikuwa inameremeta nuru ya vito vya thamani na ilipendeza kwa rangi ya maua yake sanjari na ndege, Popo wenye rangi nzuri ambao walikuwa wakivinjari huku na huko wakifurahia ardhi ile ambayo ilionekana imejaa amani na utulivu wa asili kutoka enzi na enzi tangu ilipoumbwa dunia.

‘’ Hivi mimi niko ndotoni au ni hali halisi inayonitokea hapa nilipo? Au hapa ndio peponi? Alijisemeza moyoni.

‘’Lakini peponi ni sharti kwanza ufe na baadaye ufufuke na kuhesabiwa matendo yako ikiwa ni wa kwenda peponi au motoni, lakini mimi mbona sikumbuki kama nilikufa kwanza na baadaye kufufuka, au inawezekana pale nilipokutana na yule kiumbe wa ajabu?

‘’Mhh!! Yule ndiye mtoa roho za watu Izraili….. kweli nilikufa …nilizama majini….nilijiachia majini nikafia majini…nilijikuta nikipaa hewani na kufikia hapa nilipo’’ Alijiuliza kimoyomoyo Baharia.

Alijikuta akiwa katika utata mkubwa wa fikra… ‘’Inawezekana kweli nilikufa na baadaye kufufuka lakini mbona sikumbuki kama kuna mema niliyoyafanya yanayolingana na malipo ya kuishi kwenye bustani nzuri kama hii? aliendelea kujiuliza ndani ya moyo wake.

Hatimaye alihitimisha fikra zake kwa kuamua kubaki na moja kuwa huenda alikufa na hapo ndipo pale ambapo viongozi wa dini walikuwa wakipaeleza ndani ya vitabu vya dini.

‘’Huenda yule ni malaika miongoni mwa malaika wa peponi’’ aliendelea kujisemeza moyoni mwake yule Baharia.

Akiwa katika kutafakari hali ile mara alimuona yule kiumbe wa ajabu akiwa amesimama mbele yake huku akiwa ameshika matunda yenye rangi nzuri, kwa hali aliyokuja nayo yule kiumbe wa ajabu Baharia alibaini kuwa alikuwa ni mwokozi wake na kwamba alikuwa ni miongoni mwa wa viumbe wema.

Alimsogelea yule kiumbe na kisha akapokea yale matunda na kwa haraka na pupa ya njaa aliyodumu nayo kwa takribani wiki nzima aliyatia mdomoni, baada ya kubaini ladha ya matunda yale hisia zake zikachanganyika na nguvu ya ajabu na kujiona mithili ya mtu aliyezaliwa upya.

Alijihisi kama mtu aliyeongezewa nguvu kimiujiza,alirejea na nguvu kushinda ile ya awali na kujikuta akiwa na siha nzuri kiajabu.

Pamoja na neema aliyokuwa nayo lakini katika kisiwa kile alikuwa pekee yake, hakuwepo binadamu yoyote, kisiwa kilisheheni kila aina ya matunda ambayo yalikosa mlaji, ardhi ya kisiwa kile ilisheheni madini ambayo hayakuwa na mtumiaji.

Aliishi katika upweke ule kwa takribani miaka miwili, siku moja akiwa katika matembezi yake ya kawaida kisiwani mule alitokewa na msichana mmoja mrembo ambapo kutokana na hali ya upweke aliyokumbana nayo kwa miaka miwili alidhani yule aliyemuona alikuwa si Binadamu bali ni kiumbe wa Kijini.

Alijiona kama yuko ndotoni alijaribu kufikicha macho yake na kuangalia vizuri bila kuyaamini macho yake hadi pale yule msichana alipokaribia na kumsabahi kwa lugha fasaha ya kiswahili nyororo na mwanana.

Binti yule akafarijika na kuijibu kwa pupa na kutaka kumjua yule msichana aliyemuona kama ni binadamu au Jini yule msichana alimtoa hofu baharia na kumueleza namna alivyofika pale kisiwani.

Alieleza jinsi alivyokuwa abiria katika meli iliyopata dharuba na jinsi alivyookoka kwa kushikilia guduria kubwa la maji baharini, akiwa katikati ya bahari hali ya kuwa kiu na njaa imemshika barabara alijiona tayari mtu wa kufa kwani hakutarajia msaada wowote.

Alipojiona amechoka akaliachia lile guduria la maji liende zake naye akaanza kuzama kwa kasi huku pumzi zikiwa zinampaa.

Mara akajikuta ametua kwenye kitu mfano wa godoro kubwa, alipotua tu, akarushwa juu kwa kasi na kujiona anaelea katika anga la nchi kavu, taratibu akaanza kuteremka ardhini na kutua katika nchi yenye manukato ya marashi yenye mimea mizuri rangi ya Chanikiwiti inayovutia na kila dalili ya rutuba.

Aliwaona ndege na Popo wakivinjari katika maua yenye rangi maridhawa, mara akamwona kiumbe wa ajabu mbele yake akiwa ameshika matunda katika kiganja chake kikubwa, awali alimuogopa kiumbe yule lakini kutokana na njaa aliyokuwa nayo alimsogelea yule kiumbe ambaye alikuwa mrefu kupita mnazi.

Alipomsogelea akampa matunda na kuyatia mdomoni kwa pupa, aliyala yale matunda kwa pupa kutokana na njaa aliyokuwa nayo, mara alipokula alirejea katika siha yake njema kama awali, ndipo alipoanza kuzunguka huku na kule ndani ya kisiwa bila kumuona kiumbe yoyote wa mfano wake.

Binadamu pekee aliyekuwa ndani ya kisiwa kile alikuwa ni Baharia, ingawa hawakukutana na msichana yule na hivyo kila mmoja kujiwekea makazi yake katika kisiwa kile akitarazaki kwa matunda na kuishi mithili ya mnyama kutokana na kukosa mavazi.

Binadamu wale walionekana na afya njema ingawa viungo vyao vilikuwa wazi sehemu kubwa isipokuwa katikati ya mapaja na magoti na kwamba jambo pekee lililodhihirisha utu wao ni kuweka stara kwa kuvaa majani sehemu zao za utupu.

Mavazi waliyokuwa nayo awali yalichakaa kabisa mwili laini na mororo na sura nzuri ya msichana yule ulimvutia sana baharia bila kutarajia akajikuta anamsogelea na kumshika mabega yake huku akiisawiri vyema sura yake maridhawa.

Kama mtu aliyekumbuka jambo fulani ghafla akamwachia yule msichana na kuanza kutafakari ni wapi amewahi kumuona yule msichana mwishowe akakumbuka kuwa alikuwa ni mmoja wa abiria waliokuwemo ndani ya ile meli iliyohiliki.

Msichana naye kwa upande wake aliikumbuka vyema sura ya baharia yule ijapokuwa alibadilika kutokana na nywele ndefu nyingi alizokuwa nazo wajihi wake ulimkumbusha yule msichana kutokana na ucheshi aliokuwa nao ndani ya chombo kilichohiliki.

Alikuwa na kawaida ya kuwaburudisha abiria ndani ya chombo kwa kuwakariria mashairi mbalimbali, yule msichana akamsogelea baharia na kumkumbusha baadhi ya ya beti za mashairi alizopendelea kughani;

Twaomba mola karima,
utujalie uzima,
utufikishe salama,
katika yetu safari,
kwako ndiko twaegemea,
kwa kila lililo jema.

Ewe ndiwe mwenye dhima,
kwa kila kheli na shari,
Mola wetu muadhama,
muumba nchi na sama,
tuepushe zahama,
dua kwako twaombea.

Kwa zako nyingi karama,
twatarajia salama,
tufike nyumbani vyema,
jamaa kusalimia.


Mirindimo ya sauti ile nyororo ilimvutia sana yule baharia akajikuta akitabasamu na kuyumbayumba huku na kule mfano wa mtu anayeyumbishwa na mawimbi akiwa ndani ya chombo,Baharia alifurahi upeo wa furaha yake kwani alikumbushwa enzi za kazi yake ya ubaharia.

Akainuka na kumkumbatia yule msichana kwa furaha kubwa wakiwa katika kukumbatiana mara wakasikia upepo mkali mfano wa kimbunga ukipuliza kwa kasi hali ile iliwafanya wazidi kukumbatiana wakihofia kuzolewa na kile kimbunga na kutupiwa baharini.

Mara upepo ukatoweka na viumbe wawili warefu wakawa wamesimama kwa upande wa kila mmoja,mmoja alisimama upande wa Baharia ilhali mwingine upande wa yule msichana,Baharia alimkumbuka vyema yule kiumbe mrefu kwani ndiye aliyemuokoa naye yule msichana alimkumbuka yule kiumbe kutokana na kumpa matunda yaliyomrejesha katika hali yake ya awali.

Yule msichana akaelezwa jinsi alivyookolewa wakati akizama majini, wakati msichana yule yuko hatarini alitanguliza kiganja chake kikubwa chini ya bahari ambapo mara alipo tua tu katika kiganjani alimrusha angani kisha akamteremsha ardhini taratibu na baadaye akamtokea akiwa na matunda mkononi.

Alisema alifanya vile kwa kuchelea kujitokeza machoni kwa msichana yule akiwa kule baharini kwa kuhofia kumtia kiwewe hali ambayo ingeweza kumsababishia kifo kutokana na maumbile yao wale viumbe yalivyokuwa ya kutisha pia kutokana na uchovu wa njaa na kiu aliyokuwa nayo yule msichana, vile vile kutokana na mioyo ya wanawake ilivyokuwa dhaifu.

Na kwamba hiyo ni moja ya sababu zilizo mfanya ajitokeze katika hali kama ile huku akiwa ameshika matunda ili kuonesha namna ya upendo aliokuwa nao juu yao.

Baadaye wale viumbe wakajieleza kuwa wao ni viumbe wa Kijini ambao walitokea karne nyingi zilizopita katika Milki ya Mfalme Suleiman na kwamba kutokana na kukaa muda mrefu katika kisiwa kile na jinsi walivyokula chumvi nyingi wakawarithisha Baharia na yule msichana kila kilichomo ndani ya visiwa vile na kuwaombea dua na baraka kwa kila watakacho kichuma kutokana na mikono yao.

Baadaye wale viumbe Wakijini waliowaozesha Baharia na yule msichana wakaishi wakiwa kama mtu na mkewe wakajaaliwa kupata watoto wengi ambao walikuwa mapacha wa kike na kiume nao waliendelea kuzaliana hadi kufikia kujaza kisiwa na kuwa watu wengi ambao walitokana na Baba na mama mmoja na wale viumbe wa Kijini walitoweka na kisiwa kile kikawa na watu wengi kutokana na kizazi kile cha Baharia na mkewe.

………………………………………………………………………………………….


DANGANYIKA na Fitinika ni miji iliyopo katika kisiwa kimoja ambapo Baina ya miji hiyo kulikuwa na mfereji mdogo ulioigawa miji hiyo awali watu wa upande mmoja walivuka upande wa pili kwa kutumia kidaraja kidogo kilichokuwepo hapo.

Kadri siku zilivyoyoyoma ndivyo mfereji ule ulivyoongezeka ukubwa na kuwa kama mto, daraja ya kuvukia upande wa pili ikaongezwa urefu, mto ule ulipanuka mwaka hadi mwaka na kukigawa kabisa kisiwa kile kuwa ni visiwa viwili vilivyoko umbali mrefu.

Na kadri miji ilivyozidizidi kuwa mbali uhusiano baina ya pande hizi ulipungua na kwamba ilikuwa ni nadra kutembeleana kama hapo awali seuze kujuliana hali baina ya watu wa visiwa hivi ambao kwa asili walikuwa ni ndugu wa kuzaliwa.

Jinsi ufisadi ulivyozidi katika ardhi ndivyo ambavyo umbali baina ya Danganyika na Fitinika ulivyoongezeka,baadaye ilibidi wale watu waliokuwa na uwezo ndio ambao waliweza kufanikiwa kwenda kisiwa cha pili kwa kutumia vyombo vyao vya kasi.

Hatimaye hata hivyo vyombo viendavyo kasi vilitumia siku saba majini hali hii iliwatia hofu wasafiri ndani ya bahari na hatimaye mawasiliano ya kindugu baina ya visiwa hivi yakaanza kutoeka kadri siku zilivyokwenda.

Wimbi la ugeni kutoka nchi za kigeni ulianza kuviathiri visiwa hivi taratibu wageni kutoka katika nchi za ughaibuni walivivamia kwa kasi visiwa hivi,wakiwa wamevutiwa na utajiri na mali ya asili iliyopo ndani ya ardhi ya visiwa hivi.

Maadili ya wakazi wa visiwa hivi yalianza kumong’onyoka kutokana na kufuata mila za wageni wavamizi, kutokana na utajiri uliopo wavamizi walijikuta wakilowea na kuhodhi mali zote za visiwa, ili kuwateka wakazi wa visiwa hivi wageni waliwashauri kuunda umoja baina ya pande mbili za visiwa.

Viongozi wa ngazi za juu waliupokea ushauri huu kwa mikono miwili, na hivyo kujikuta wakianza kuwatumikia wavamizi kwa kila hali ambapo walitumia fursa hiyo ya kukubalika kwao miongoni mwa Viongozi wa Visiwa hivi kupanga mbinu za uhujumu na ufisadi dhidi ya rasilimali iliyopo.

Wageni walipanga mbinu kupitia umoja huo ili kuvinjari pande zote za visiwa bila vikwazo vyovyote, ambapo walitumia mbinu hizo kuwekeza vitega uchumi baadaye wakaanza kuweka vitega uchumi mbalimbali visiwani humo kutoka Ughaibuni kila kukicha.

Tabia za wenyeji zikaanza kubadilika kwa kufuata mila za kigeni ambapo nao wakautumia mwanya huo kupandikiza fikra zao na kuhamisha kila rasilimali na kupeleka kwao huku wenyeji wakijisahau kutokana na vijizawadi vidogo vidogo.

Walibeba mali nyingi vikiwemo vito vya thamani ambavyo kwavyo walitengeneza za vidani ambavyo baadaye walikuja kuviuza kwa wazalendo wa visiwani humo kwa gharama kubwa, nchi hizo zilianza kuneemeka kutokana na rasilimali itokanayo na visiwa hivyo.

Nchi hizo zilijenga miji mikubwa yakiwemo majiji ambayo yalitokana na rasilimali hizo za Visiwani ambapo Tawala zilizokuwepo zikavunjwa na kupandikiza watu wenye itikadi na mila za kwao ili watawale kwa manufaa ya wageni hao.

Wadanganyika na Wafitinika walilaghaiwa na hatimaye vyanzo vyote vya uchumi vikawa chini ya wageni ambao nao wakawa wanaitumia ile mali kwa kunufaisha nchi zao kwa kisingizio cha kuwekeza Vitegauchumi, Dhahabu, Almasi na baadhi ya vito vya thamani vilisafirishwa kwa wingi kupelekwa Ughaibuni.

Hatimaye vidani ambavyo vilikuwa vikitengenezwa visiswani humo vikawa vinaingizwa kutoka nchi za Ughaibuni kwa fedha za kigeni na hivyo kuifanya mali ya wananchiwa visiwa hivi kupotea taratibu ilhali raia wa visiwa hivi bado hawajatanabahi.

Waliendelea kujidanganywa na vijizawadi ambavyo vilikuwa havina maana yoyote visiwa hivi walidanganywa na vijizawadi vidogovidogo visivyokuwa na manufaa yoyote zawadi ambazo asili yake inatokana na visiwa vyao.

Utamaduni wa nchi za kigeni ulizidi kujikita ndani ya visiwani hivi klabu za pombe mbalimbali zilijengwa majumba na madanguro ambayo watu hutembea uchi kama wanyama nyakati za usiku vilizidi kushamiri.

Ufukwe wa bahari ambao hapo awali ulikuwa ni sehemu muhimu kwa watu kupumzika na kupunga hewa ulibadilika na kuwa ni sehemu za maasi na uasherati na kwamba lilikuwa ni jambo la kawaida kuwakuta watu wa jinsia tofauti wakiwa pembezoni mwa bahari mithili ya wanyama walifanya vitendo vya ngono hadharani huku wakiwa kama walivyotoka matumboni mwa mama zao.

WADANGANYIKA walidanganyika na kuacha uchamungu wao kwa kuzamia kwenye maadili ya kishetani, maadili ambayo yaliacha athari mbaya kwa vizazi hadi vizazi ambapo,Wafitinika walifitinishwa na ndugu zao Wadanganyika kiasi kwamba uhusiano wao ulikuwa mbali kama mbingu na ardhi ile hali ya awali ya kukutana baina ya visiwa hivi na kujadiliana mustakabali wa visiwa vyao ilitoweka.

Inaendelea…..

Post a Comment

  1. Kazi yako imetulia Mzee. Ukiandika kitabu itapendeza zaidi ili kuwafikia waTanzania wengi wasiojua teknolojia hii.
    Unastahili pongezi kwa Fasihi hizi za ufasaha. Nimefurahi kutembelea hapa. Nimejifunza mengi.

    ReplyDelete
  2. Mkwinda kazi njema sana maana hapa kweli ulikuwa umetulia na kupanga maneno, sijaimaliza kazi hii ngoja nivute pumzi ila jitihada hizi zapaswa kuigwa, kwa nini tusiende kwa malengo ya kuchapa vitabu kabisa Mkwinda, vikiwa ni pamoja na vua ushairi pia?

    ReplyDelete
  3. Nashukuru kwa kuniunga mkono,Bwaya na Makene, mimi nadhani Bw. Makene tukiunganisha nguvu tunaweza kulifanya hili likawezekana lazima tuache historia chini ya jua hili na vizazi vijavyo vitutaje kwa mchango wetu wa kuienzi fasihi ya kiswahili,sasa naomba niseme jambo moja, unajua kuna Maprofessa wawili wa pale chuo kikuu Bw. Mugabyuso Mulokozi na Bw. K.Kahigi na Mzee mahiri kwa utunzi kule visiwani ambaye makazi yake sasa yapo jijini Dar, Shafii Adamu Shafii wana miswada ambayo inasomwa mashuleni.

    Huyu Bw. Shafii kama umehitimu shule miaka ile alikuwa na kitabu chake cha Kuli na ssa ana Vuta n'vukute ambapo kile cha Kuli nadhani bado kinasomwa kama sikosei.

    Hawa akina Mulokozi na Kahigi wana kijitabu chao kinaitwa Malenga wa Bara kipo madukani nadhani wako mbioni kukifanya kisomwe mashuleni.

    Tatizo la huku kwetu ni namna ya uchapaji na uchapishaji tunaweza kuunganisha mashairi yetu mimi, wewe na wengineo tukaandaa kijitabu chetu kibaki kiwe kumbukizi za wanaBlogu katika kuenzi Fasihi za kiswahili. tukakiita kijitabu chetu,''MALENGA WA GAZETI TANDO'' we unaonaje hili? tafadhali naomba tulifanyie kazi tukusanye kazi zetu kwa kuwa wewe uko huko ughaibuni unaweza kupata wachapishaji waaminifu wakatufanyia hii kazi mimi ninayo mashairi ambayo yanaweza kutosha hata vijitabu viwili vyenye kurasa 60 kila kimoja, tuunganishe Ugazeti Tando wetu ufahamike katika ulimwengu wa fasihi za kiswahili

    Wakatabahu.

    ReplyDelete
  4. Mkwinda nisikuahidi kitu sasa zaidi ya kuwa naamini nakuja Tanzania muda wowote na tutatumia nguvu zetu changa kufanikisha suala hili. Hicho cha ushairi kinawezekana na hata Riwaya na tamthiliya tukitaka kufanya hivi twaweza kabisa. Kinachotakiwa ni nia. Nipe taarifa za awali hapo Bongo kuchapa kopi kama 1000 za awali ni shilingi ngapi kisha nijue lipi la kufanya. Naambatanisha shukrani zangu za dhati Mkwinda Mnyezi Mungu akubariki sana.

    ReplyDelete
  5. Mkwinda kazi kama hizi nikiziona kwenye blogu ninapata furaha sana. Endelea malenga wetu.

    Nilitaka kukuuliza kwanini usitumie huduma ya ripway (http://ripway.com) kuhifadhi simulizi ndefu ili tuzisome kwenye "microsoft word"? Ni rahisi zaidi kusoma kazi ndefu kwenye "word."

    Au unaweza kutumia huduma nyingine ambazo nimezijadili hapa:
    http://tinyurl.com/pclk4

    ReplyDelete
  6. Nimerudi hapa tena. Unajua Rashid simulizi za kisayansi (kama ulivyoziita) hatujazizoea sana kwenye fasihi ya kiswahili. Hakuna sababu ya kutokuwa na aina hii ya fasihi.

    ReplyDelete