Ads (728x90)

Swala linanitatiza, kisa cha mtema kuni,
Ni lipi lilomkwaza, kwa kumtaja vinywani,
Akatufanya kuwaza, mtema kuni ni nani,
Kisa cha mtema kuni, alifanyani?

Kisa cha mtema kuni, ni kauli ya zamani,
Wahenga walibaini,kisa chake kwa undani,
Sisi akhiri zamani,hatukimanyi yakini,
Kisa cha mtema kuni, alifanyani?

Katika kutema kuni, kilichomsibu nini?
Alikutana na nini,alipofika porini?
Au watu wamebuni, kufurahisha uneni?
Kisa cha mtema kuni, alifanyani?

Nilidhani akilini, alipotea mwituni,
Baada kutema kuni, katumbukia shimoni,
Hakutokea nyumbani, mwisho wa mtema kuni,
Kisa cha mtema kuni, alifanyani?

Nilibuni fikirani,alikutana na jini,
Kapelekwa baharini,akazamishwa majini,
Baada ya siku tisini,akarudishwa nchini,
Kisa cha mtema kuni alifanyani?

Mambo mengi nilidhani, juu ya mtema kuni,
Kakata mzeituni, ukanena ewe nani?
Ukamkwida shingoni,mbio akazisaini,
Kisa cha mtema kuni,alifanyani?

Swala hili si utani, limenikwaza amini,
Nalianika ugani, msawiri bloguni,
mtafakari makini, wa Mrima na wa Pwani,
Kisa cha mtema kuni, alifanyani.

Nahitimisha uneni, wasomaji bloguni,
Naomba nipokeeni, jawabu lenye mizani,
Makene wa kasirini,na wengine duniani,
Kisa cha mtema kuni asili yake ni nini?

Shairi hili niliwahi kuliandika katika magazeti ya Mwananchi Juni 23 2001 na Nipashe Juni 19 2001 lakini hadi sasa sijapatiwa jibu nimeamua kulikariri katika blogu asaa huenda nitapatiwa jibu la kuniridhisha.

Wakatabahu.

Post a Comment