Ads (728x90)


Binti wa kwanza Marehemu Dkt. Wilbert Kleruu, Eva Wilbert Kleruu akizungumza na mwandishi wa makala haya.
Mnara wa kumbukumbu eneo la Mkungugu Isimani Iringa mahala alipofia aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Iringa Dkt.Wilbert Kleruu, mwaka 1971


Eva Kleruu akifuta machozi baada ya kukumbuka jambo juu ya mauaji ya baba yake miaka 43 iliyopita
Eva Kleruu mtoto wa kwanza wa marehemu Dkt. Wilbert Kleruu aliyeuawa akipigania siasa ya ujamaa na Kujitegemea huko mkoani Iringa

‘’NI vigumu, kuvumilia hali hii, bali naamini  haya ni matokeo na ni mipango ya Mungu kuifanya hali hii,baba yetu alikuwa ni Muumini wa Ujamaa na Kujitegemea aliyesimamia sera za Ujamaa na kujitegemea kama ilivyokuwa kwa wakati ule enzi za Mwalimu Nyerere’’
‘’Serikali ilikuwa inahimiza vijiji vya Ujamaa, ili wanananchi washiriki kwa pamoja kwenye Kilimo cha Kufa na Kupona, baba alifuatilia kwa kina maagizo ya Mwalimu, inawezekana hili ndilo lililosababisha kuuawa akiamini alichosimamia kilikuwa sahihi,’’anasema Eva Wilbert Kleruu huku akibubujikwa na machozi.
‘’Samahani umenikumbusha mbali sana miaka 43 sasa baada ya kifo cha baba yangu, nilikuwa bado binti mdogo miaka ile ya mwanzo ya miaka ya 70, baba alikuwa ni mfuasi wa Ujamaa na Kujitegemea na alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa aliyeagizwa kusimamia siasa ya Ujamaa na Kujitegemea,’’anasema.
Anasema ni hali ambayo imekuwa ngumu kuisahau kutokana na aina ya tukio lenyewe lilivyojiri na kwamba ingekuwa kifo kile kilitokana na ugonjwa jambo hilo lingezoeleka kwa haraka, bali hata hivyo anaamini kilichotendeka kilitokana na uelewa mdogo juu ya mpango wa serikali kuimarisha vijiji vya Ujamaa na kujitegemea.
Anafafanua kuwa anaamini kifo cha baba yake kilikuwa ni sawa na kujitolea mhanga katika harakati za Ujamaa na Kujitegemea kwani baba yake alikuwa ni miongoni mwa waumini wa Ujamaa ambao walisimamia na kuamini kuwa siku moja nchi inaweza kujitegemea kwa sera ya ujamaa na Kujitegemea.
Anasema serikali wakati ule ilisimamia mpango kwa nia ya kuboresha huduma za wananchi wka pamoja na kuondoa ukiritimba wa ubepari kwa mtu mmoja kuhodhi eneo kubwa la ardhi jambo ambalo baadhi ya watu wasioenda maendeleo walikuwa wakilipinga.
Aidha anasema hata hivyo anayofursa ya kuishukuru serikali kwa kuwajali na kuwasomesha kwa ngazi ya juu ya elimu ambapo yeye alisoma hadi nchini Burgaria na mdogo wake alipelekwa nchini Urusi katika nchi zilezile zilizokuwa zinaamini siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.
Anasema pamoja na tukio hilo kukatisha mapenzi baina ya baba na familia yake kwa kukatishwa maisha kikatili serikali ilikuwa bega kwa bega na  familia ya marehemu Dkt Kleruu kwa hali na mali ambapo Mwalimu Julius Nyerere, Mzee Abeid Karume ambapo kwa bahati mbaya mzee Karume aliuawa akiwa katika harakati za kuendelea kuienzi familia hiyo.
‘’Mzee Karume alikuwa upande wetu sana alijitahidi kwa hali na mali kuhakikisha tunaishi kwa upendo, amani na utulivu, lakini bahati mbaya naye aliuawa mwaka uliofuatwa kwa risasi,’’anazungumza Eva huku akibubujikwa na machozi.
Anasema hata mrithi wa Marehemu Karume Mzee Aboud Jumbe naye aliendeleza mahusiano ya kuijali familia yetu ambapo pia Mzee Rashid Kawawa na Mama Getrude Mongela nao walikuwa mstari wa mbele katika kutufariji.
‘’ Mama yetu bado yupo hai amestaafu alikuwa akifanya kazi katika ofisi ya Mkuu wa mkoa, baada ya kutoka Iringa kufuatia mauaji yale tulirudi Moshi, tukaendelea kusomeshwa na serikali Mzee Karume alikuwa mstari wa mbele kutusaidia.
‘’Mama yetu kwa sasa anaishi Moshi, niko na wadogo zangu, watatu, mmoja anaitwa Andrew, mwingine Carmen ambaye ni Bibi Afya  na Edwin ambaye ni mjasiriamali wote tulisomeshwa kwa ngazi za juu, tunaishukuru serikali kwa kutujali,’’anabainisha.
Kadhalika anasema kuwa katika kuendelea kujisahaulisha tukio lile la kikatili lililofanywa dhidi ya baba yake amepanga kukutana na familia ya marehemu Mwamwindi ambaye ndiye aliyemuua baba yake, ili wazungumze na kuanzisha ukurasa mpya wa maisha.
‘’Unajua visasi vinarithishwa kimaumbile, bila kukutana na familia ile vizazi vyetu vinaweza kujikuta vikiingia katika dhambi isiyotarajiwa, napenda nikutane na mtoto mkubwa wa Mzee Mwamwindi, ili tufungue ukurasa mpya wa maisha, hatujawahi kukutana hata mara moja wala hatujuani,’’anasema Eva.
Anasema nia ya kukutana naye ni kuanzisha uhusiano mpya ambao ulitoweka kwa zaidi ya miaka 40 huku viongozi wa wakati huo Mwalimu Nyerere, na Mzee Karume nao wakiwa wametangulia mbele ya haki hivyo anaamini kwa kukutana na wanafamilia hao utaanzishwa uhusiano chanya wenye lengo la kudumisha amani na utulivu.
‘’Sifikirii wala sijawahi kufikiria kulipiza kisasi, tulikaa kama familia tukamuomba Mungu atulinde na vitendo vya kishetani, tunaamini Mungu anaendelea kutulinda na kilichotokea kilikuwa ni dhamira iliyosukumwa na vitendo vya kishetani,’’anasema Eva.

Post a Comment