Ads (728x90)


Na,Mwanafasihi Wetu, Tunduma.
WAKAZI wa mji wa Tunduma usiku wa kuamkia jana walijikuta wakishikwa na taharuki kwa ‘ushamba’ kutokana na taa za kisasa aina ya ‘Disco light’zilizokuwa zimesambaa katika anga la mji huo kutokana na muziki uliokuwa ukipigwa katika mji mdogo wa Nakonde uliopo nchi jirani ya Zambia.
Taa hizo za Disco Light zilisambaa anga lote la mji wa Tunduma kuanzia majira ya saa 3;00 usiku hadi usiku wa manane ulipomalizika muziki huo na kuibua hofu miongoni mwa wakazi wa mji huo uliopo mpakani wa Tanzania na Zambia.
Kuibuka kwa tukio hilo kulisababisha makundi ya watu kutoka nje ya majumba yao na kushangaa taa hizo ambapo baadaye walifahamishwa kuwa taa hizo zinatokana na burudani ya muziki iliyokuwa ikiendelea katika mji huo wa Nakonde nchini Zambia.
 ‘’Ukumbi huo ni wa wazi..wenzetu wanatumia taa za kisasa zenye uwezo mkubwa wa kusambaa angani huku midundo ya muziki ikiendelea,teknolojia hii haipo hapa kwetu Tanzania,’’alisema Diwani wa Kata yua Tunduma Frank Mwakajoka.
Mwakajoka alisema kuwa watu walipoona mwanga huo unasambaa angani walitoka nje ya majumba yao wakidhani kuwa kuna hatari imetokea katika mji huo uliopo mpakani.

Alisema kuwa hata hivyo walifanya jitihada ya kuwataarifu wananchi kuwa hakuna tatizo lolote juu ya mwanga huo ambao kwa sehemu kubwa ulieneza mwanga katika mitaa iliyopo katika mji wa Tunduma.
Naye Herode Jivava mfanyabiashara na mkazi wa mjini Tunduma alisema kuwa alipotoka nje usiku alikuta kundi la watu wakiwa nje ya nyumba zao wakiushangaa mwanga huo ambapo ulikuwa unazunguka kutoka mashariki hadi magharibi kwa sekunde kadhaa.
Hatimaye jitihada za Diwani wa kata hiyo Mwakajoka zilifanikiwa kuwatuliza wananchi ambappo waliingia majumbani mwao.



Post a Comment