Ads (728x90)




MTOTO ALIYETUMBUKIZWA CHOONI AKIPEWA HUDUMA KATIKA HOSPITALI YA WILAYA VWAWA MBOZI


WAKAZI WA VWAWA WILAYANI MBOZI WAKIWA NJE YA HOSPITALI YA VWAWA MBOZI KUSHUHUDIA MTOTO ALIYEOKOLEWA KUTOKAA SHIMO LA CHOO




CHOO AMBACHO MTOTO HUYO ALIDUMBUKIZWA



Na,Rashid Mkwinda, Mbozi

WAKATI akina mama wengine wakihaha kwa waganga kutafuta dawa kwa ajili ya kupata watoto, wengina wanaichezea bahati yao kwa kufanya matukio ya unyama kama ilivyotokea kwa msichana mmoja aliyetambulika kwa jina la Esther kuamua kumtupa mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miezi mitatu katika shimo la choo kinachotumika kwa nia ya kumuua.
Tukio hilo la kinyama limetokea mwishoni mwa wiki katika kitongoji cha Ilolo kilichopo mjini Vwawa wilayani Mbozi ambapo msichana huyo alivaa roho ya unyama na kuamua kutekeleza ukatili huo bila hata roho ya huruma huku sauti ya kitoto chake kichanga ikilia kwa kubembeleza ili kionewe huruma ya kuuliwa bila hatia.
Kama vile haitoshi msichana huyo anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 15 aliziba masikio yake kwa pamba na kuamua kukitumbukiza kitoto hicho ndani ya shimo na kutokomea kusikojulikana.
Sauti za kilio za mtoto yule zilihanikiza hewani bila kupatiwa msaada wowote ambapo hatimaye kilio chake kikasikika hadi kwa wasamaria wema ambao ndio watumiaji wa choo hicho.
Mmoja wa wasamaria hao aliyejitambulisha kwa jina la Mbwagile Kitaja mkazi wa Ilolo mjini vwawa alisema kuwa tukio hilo limetokea wakati wakiwa msibani majira ya saa 8 mchana  ambapo walikuja wajukuu zake kumueleza kuwa ndani ya choo cha jirani kuna sauti ya mtoto analia.
Alisema majirani walifika katika eneo hilo la tukio na kuamua kukivunja choo hicho ili kukiokoa kitoto hicho ambacho kwa muda huo mwili wake wote ulianza kuzingirwa na funza wa chooni.
Walibomoa choo hicho kwa tahadhari wakihofia kumdhuru mtoto ambapo mmiliki wa choo hicho aliyejitambulisha kwa jina la Orasmo Nyingi (Pompi)alitoa taarifa kwa Mwenyekiti wa mtaa huo Ephraimu Mwakiteba alisema kuwa walifanya jitihada za kumtoa kwa kutumbukiza ngazi mbili ndani ya shimo na kisha kumtoa na kumsafisha uchafu.
Alisema kuwa walimfikisha mtoto huyo katika hospitali ya wilaya iliyopo Vwawa wilayani Mbozi ambapo alipewa huduma ya kwanza ambapo katika baadhi ya sehemu zake za mwili alianza kuunguzwa na joto la uchafu wa chooni lakini hata hivyo walifanikiwa kumpa matibabu na kisha kuruhusiwa ambapo mama Kitaja alichukua dhamana ya kumlea.
Aidha katika hatua nyingine babu wa mtoto huyo ambaye alijitambulisha kuwa ni Ofisa Maendeleo ya jamii wa wilaya ya Mbozi Philimon Adrat alisema kuwa binti yake ndiye mwenye mtoto huyo na kwamba anashindwa kuelewa sababu ya kumtumbukiza chooni mwanaye kwa kuwa ni yeye mwenyewe aliyebeba ujauzito bila kushinikizwa na mtu.
Alisema kuwa mara baada ya kupata ujauzito alimtunza na kulea ujauzito wakehadi alipojifungua mwezi Julai ambapo mtoto huyo alikuw akiendelea vyema.
Alifafanua kuwa kabla ya kumtumbukiza mtoto huyo chooni binti yake alifukuzwa na mama yake na kuambiwa aje kwa baba yake ndipo alipofika nyumbani na kukaa siku mbili na kuelezea mkasa wa kutimuliwa na mama yake ambapo hata hivyo siku ya tukio hakujua kama mwanaye anaweza kuamua kufanya unyama wa aina hiyo.
Akizungumzia hatima ya tukio hilo Mwenyekiti wa serikali ya kitongoji cha  Lami mtaa wa Ilolo ambako ndiko lilikotokea tukio hilo Bw.Mwakiteba alisema kuwa mara baada ya kutokea kwa tukio hilo walipeleka taarifa kituo cha polisi ambapo hata hivyo binti huyo hajulikani aliko hadi sasa.
Babu wa mtoto huyo Bw. Adrati alisema kuwa hajui aliko binti yake na kwamba wanafanya utaratibu wa kumchukua mtoto huyo kutoka kwa wasamaria wema ambao wanamtunza mara baada ya kutokea tukio hilo.



Post a Comment