Ads (728x90)

Kikosi cha timu ya Azam FC kilichowalambisha Mbeya City bao 1-0 katika uwanja wa kumbukumbu ya Sokoine Jijini Mbeya leo jioni


Kikosi cha Mbeya City kilichokubali uteja wa kufungwa mara mbili mfululizo na timu ya Azam ya Jijini Dar







Kocha wa timu ya Mbeya City Juma Mwambusi akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mchezo kati ya Mbeya City na Azam

MABINGWA watetezi wa kombe la Ligi Kuu ya Vodacom msimu uliopita Azam FC leo imeendeleza ubabe kwa kuifunga timu ya Mbeya City ya Jijini Mbeya kwa bao 1-0.
Msimu uliopita Azam iliweza kuifunga Mbeya City mabao 2-1 katika uwanja wake waw nyumbani na kuipa tiketi ya kutwaa ubingwa huo kwa mara ya kwanza tangu timu hiyo ianzishwe.
Katika mechi ya leo timu hizo zilianza kwa kushambuliana kwa zamu huku kila mmoja akionesha uchu wa kuishinda mechi hiyo.
Azam iliyoongozwa na washambuliaji Kipre Cheche,Erasto Nyoni,Didier Kavumbagu, Himid Mao na Micheal Ballou iliutawala mchezo katika kipindi cha mwanzo huku Mbeya City ikiwategemea walinzi wake Deogratius Julius,Hassan Mwasapili, Yusuf Abdallah na Yohana Morris kuzuia mashambulizi ya wachezaji wa Azam.
Ilikuwa ni katika dakika ya 19 ya mchezo kulipotokea mashambulizi langoni kwa Mbeya City ambapo mchezaji wa Azam Salum Abubakar ‘Sure Boy’ alifanyiwa madhambi eneo la adhabu na mwamuzi Martin Sanya aliamuru upigwe mpira wa adhabu ndogo kuelekea kwa timu ya Mbeya City.
Mpira huo uliopigwa na Aggrey  Morris  ulitinga moja kwa moja wavuni kupitia juu na kumuacha golikipa wa Mbeya City David Burhan akichupa bila mafanikio.
Goli hilo la Azama lilizima nderemo na hoi hoi za mashabiki wa Mbeya City na kuibua vifijo na nderemo kwa upande wa mashabiki wachache wa Azam walioketi katika jukwaa la kusini.
Baada ya goli hilo wachezaji wa Mbeya City alionekana kutoelewana na kulazimika kucheza mipira ya juu juu na mara nyingine kupiga ovyo bila mpangilio huku wachezaji wa timu ya Azam wakicheza kwa kuonana.
Ilikuwa almanusura kwa timu ya Azam ihesabu bao la pili katika dakika ya 26 ya mchezo ambapo hata hivyo mwamuzi alinyoosha kibendera cha kuotea kabla ya mchezaji wa Azam Said Morad hajatumbukiza mpira wavuni.
Hadi mapumziko Mbeya City ilikuwa nyuma kwa 0-1 ya bao la Azam.Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Azam wakitaka kuongeza bao na Mbeya City wakijitahidi kutafuta bao la kusawazisha lakini bahati kwa Mbeya City haikuwa yao.
Kipenga cha mwisho cha mchezo kilishuhudia mashabiki wa Mbeya City wakitoka vichwa chini na kukubali kuwa vibonde wa Azam kwa mara ya pili mfululizo kwa kufungwa bao 1-0.
Mbeya City: David Burhan,Deogratius Julius,Hassan Mwasapili,Yusuph Abdallah,Yohana Morris,Antony Matogolo,Saad Kipanga,Steven Mazanda,Paul Nonga, Mwagane Yeya na Deus Kaseke.
Azam FC: Aishi Manula,Shomar Kapombe,Gadiel Mbaga,Said Morad,Aggrey Morris,Michael Ballou,Himid Mao,Erasto Nyoni,Didier Kavumbagu,Salum Abubakar na Kipre Cheche.

Post a Comment