Ads (728x90)

Ofisa Ufundi wa TAHA Isaac Ndamanhyilu akiwa katika moja ya mashamba ya Nyanya ambalo TAHA limesaidia mafunzo na teknolojia

Mkulima wa mbogamboga na matunda Daniel Wabare akiwaonesha wakulima wa mboga mboga na matunda namna ambavyo alifanikiwa katika kilimo cha Nyanya kwa msaada wa Shirika la TAHA

Mtaalamu wa kilimo kutoka TAHA kanda ya Mashariki Annania Bansimbile akiwaelekeza wakulima namna ambavyo umwagiliaji kwa mfumo wa matone unavyoleta tija kwa kilimo cha Mbogamboga na matunda

Katibu Tawala wa wilaya ya Mbarali Alfred Mzurikwao akiwapa nasaha wakulima kwenye kilele cha siku ya wakulima Shambani katika kijiji cha Ilaji wilayani Mbarali
Ofisa Ufundi TAHA Isaac Ndamanhyilu akiwapa zoezi la uelewa wakulima waliohudhuria katika maadhimisho ya siku ya wakulima Shambani katika kijiji cha Ilaji wilayani Mbarali.
 
WAKULIMA wa mbogamboga na matunda mkoani Mbeya wametakiwa kuutumia vyema uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Songwe kwa kuzalisha na kusafirisha  mazao yenye ubora ili waweze kujiinua kiuchumi.
Kauli hiyo imetolewa na Ofisa Ufundi wa Shirika lisilo la Kiserikali linalojihusisha na utaalamu na mafunzo ya uzalishaji mazao ya mbogamboga, matunda, maua na viungo (TAHA) Isaac  Ndamanhyilu  wakati wa kuadhimisha siku ya wakulima shambani kijiji cha Ilaji wilayani Mbarali mkoani Mbeya.
 Ndamanhyilu alisema kuwa wakulima wa mbogamboga, maua na matunda mkoani Mbeya wanayo fursa ya nzuri ya masoko kwa kuutumia uwanja wa Kimataifa wa Songwe kwa kushindana na masoko ya Kimataifa kuzalisha kwa ubora.
‘’Ardhi ya mkoa wa Mbeya ni rafiki kwa mazao yote, ikitumiwa vyema kwa kilimo cha mbogamboga na matunda itakuwa ni mkombozi wetu  kiuchumi,’’alisema.
Ndamanhyilu alisema kuwa kwa kuthamini mpango wa shirika hilo katika kuchangia maendeleo ya kilimo cha mbogamboga na matunda nchini serikali imetoa ruzuku ya sh.bilioni 1.4 ili kusukuma jitihada za wakulima kujiinua  na kuongeza tija.
Alisema matarajio ya TAHA ni kuongezeka kwa hamasa ya kilimo na matumizi ya teknolojia ya umwagiliaji na kilimo cha Matone kwa kutumia mfumo wa usambazaji maji kwa kutumia mpira katika matuta, ‘’Drip Irrigation’’ ambao humsaidia mkulima kuzalisha kwa tija.
Naye Mkulima wa mboga mboga katika kijiji cha Ilaji wilayani Mbarali Daniel Wabare alisema kuwa kwa kipindi kisichozidi miezi mitatu amemudu kuandaa shamba la nyanya kwa kutumia utaalamu unaozingatia vigezo vya maandalizi bora ya shamba la Mbogamboga.
Alisema ameweza kuandaa shamba la hekari moja kwa gharama ya sh milioni 2.5 ambapo anatarajia kukusanya zaidi ya sh. milioni 8 na kuwa mafanikio hayo yametokana na uchaguzi wa mbegu bora, maandalizi ya vitalu, matumizi ya mbolea, maji na dawa za kuulia wadudu.
Awali akizungumza katika maadhimisho hayo Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbarali Alfred Mzurikwao alisema kuwa wakulima wa mbogamboga na matunda wanapaswa kuzingatia utaalamu kutoka kwa maofisa ugani na kuwataka maofisa ugani kutokaa maofisini na badala yake watembelee mashambani kukutana na wakulima.
‘’Watumieni vyema maofisa ugani walioko katika maeneo yenu, nanyi maofisa ugani msikae maofisini watembeleeni wakulima ili mjue changamoto wanazokutana nazo katika kilimo,’’alisema.

Post a Comment