Ads (728x90)

Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro akiweka udongo katika kaburi la Shekhe wa wilaya ya Mbeya

Imamu wa msikiti wa Baraa Bin Azb Ibrahimu Bombo akimwaga machozi wakati akizungumza kwa hisia juu ya kifo cha Shekhe Mketo
Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro akitoa nasaha mara baada ya mazishi ya Shekhe wa Wilaya ya Mbeya Abubakar Mketo



SHEKHE wa wilaya ya Mbeya (BAKWATA)Abubakari Mketo amefariki ghafla mwishoni mwa wiki baada ya kuanguka wakati akitoa mawaidha makaburini.
Tukio hilo la aina yake limetokea katika makaburini ya Nonde Jijini Mbeya wakati wa mazishi ya Mayasa Salmini( Bibi Majuto) aliyefariki katikati ya wiki iliyopita na mazishi yake kufanyika katika katika makaburi hayo.
Mashuhuda wa tukio hilo wamedai kuwa mara baada ya kumaliza kuusitiri mwili wa marehemu Bibi Majuto ndani ya kaburi, Shekhe huyo alisimama na kuanza kutoa mawaidha kwa waombolezaji waliohudhuria mazishi hayo.
Imeelezwa kuwa Shekhe Mketo alianza kwa kusema kuwa ‘’kila nafsi lazima itaonja mauti’’ na kuwa si ajabu hata yeye (Shekhe) anayeongea wakati huo anaweza kufa wakati baada ya kumaliza mazungumzo mbele ya macho yao.
Shuhuda huyo anaeleza kuwa mara baada ya kumaliza kauli hiyo Shekhe huyo alianguka ghafla na kukimbizwa katika hospitali ya Rufaa Mbeya ambako ilithibitika kuwa alikuwa ameshafariki dunia.
Katika mazishi ya Shekhe huyo ambayo yalihudhuriwa na Mkuu wa mkoa wa Mbeya umati wa watu waliohudhuria walikuwa na taharuki na kuibua maswali juu ya mazingira ya kifo hicho.
Mashekhe mbalimbali waliohudhuria mazishi hayo walisema kuwa kifo hicho kinafundisha waumini kujiandaa na safari ya kifo ambacho kinaweza kukuta wakati  wowote bila kutarajia.
Shekhe wa msikiti wa Isanga Ibrahimu Bombo alisema kuwa tukio hilo ni dalili pekee ambazo zinapaswa kuwafundisha waumini wa dini hiyo kujiandaa kwa kufanya matendo mema kwa kuwa kifo kinaweza kumkuta binadamu mahala popote.
‘’Tujiwekee maandalizi ya safari ya akhera, hakuna anayejua saa wala tarahe ya kuondoka kwake duniani, kifo cha Shekhe wetu kitupe mafundisho,’’alisema Shekhe Bombo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro aliwataka kutohusisha kifo hicho na imani zozote za ushirikina bali waamini kuwa kimetokana na mipango ya Mungu na kuwa kila mtu ataondoka duniani kwa njia zake.
‘’Nawasihi ndugu zangu, tusitumie msiba huu kuleta mgongano, yatazungumzwa mengi juu ya kifo hichi lakini tuamini kuwa Mungu ndiye aliyeamua kumchukua Shekhe wetu kwa njia hii,’’alisema Kandoro.
Alisisitiza kuwa jambo linalopaswa kufanywa ni kumuenzi marehemu kutokana na matendo yake mema ambayo alikuwa akisisitiza kudumisha mshikamano amani na utulivu.

Post a Comment